Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amesema kwa kipindi cha sasa mawakili na wanasheria wanatakiwa kujitokeza na kuielekeza jamii njia sahihi ya kufuata ikiwamo utawala wa sheria.
Pia amewataka wanasheria hao kuungana kutetea chama chao kwa sababu itakuwa nchi ya kwanza duniani kufutwa chama cha aina hiyo.
Alikuwa akizungumza jana baada ya Kaimu Jaji Mkuu, Prof. Ibrahimu Juma kuwaapisha mawakili wapya 248 katika viwanja vya Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Alisema mawakili wanatakiwa kujitokeza kuilekeza jamii njia sahihi ya kufuata ikiwamo utawala wa sheria haki za binadamu na demokrasia kutokana na mazingira ya sasa.
“TLS inakabiliwa na tishio kubwa la kufutwa lakini itakuwa ni nchi ya kwanza kufuta chama cha mawakili jambo ambalo litashangaliwa na wengi kwa vile sisi ni watu muhimu katika taifa,’’ alisema Lissu..
Alisema mawakili hao 248 walioapishwa jana ukiwajumlisha wote unapata idadi ya mawakili 6,329 hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka huduma za uwakili na sheria.
Lissu alisema Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya pili kwa uwingi wa wanasheria Afrika Mashariki, ya kwanza ikiwa Uganda hivyo hali siyo mbaya kama nchi.
Naye Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma alisema mawakili ni watu muhimu na anaamini kwa idadi hiyo kazi zitafanyika kwa uelewa na weledi katika mahakama .
“Mawakili Tanzania wengi wao ni vijana wadogo hivyo wanatakiwa kujiendeleza kusoma kwa sababu wanasheria wanaosoma sasa ni tofauti na waliopata elimu hiyo zamani.
“Muitumie nafasi hii katika kuelewa shughuli mbalimbali za mahakama kwa haki muwe wanasheria wazuri wa kusaidia nchi hata kwenye mambo mbalimbali ya sheria yakiwamo ya uchumi na mataifa,” alisema Profesa Juma.