33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AWAAMBIA TLS WASICHAGUE MAADUI

NA WANDISHI WETU


WAKATI wajumbe wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) hii leo wakitarajia kumchagua rais wao, mmoja wa wagombea wa kiti hicho Wakili Fatma Karume anatazamwa kubeba kivuli cha kiongozi aliyemaliza muda wake, Tundu Lissu.

Mazingira ya Fatma kubeba kivuli cha Lissu katika uchaguzi huo yamejionyesha wazi kutokana na mamia ya wanachama wa TLS wanaomuunga mkono Lissu, kuonyesha dhamira ya kumpigia kura.

Jana Rais anayemaliza muda wake, Tundu Lissu alipata wasaa kuzungumza na mawakili wenzake hao waliokushanyika Arusha kupitia tamko lake lenye maneno 4096 alilolitoa kwa maandishi kutoka Ubelgiji anakoendelea na matibabu.

Lissu licha ya wakuwashukuru wanataaluma wenzake kwa kushirikiana na wasamaria wema wengine kumsaidia kutokana na matatizo aliyoyapata, aliwakumbusha mawakili hao kwamba wakati wanapiga kura leo watambue kwamba wapo wenzao ambao wamekumbwa na madhira mbalimbali kama ilivyo kwa wananchi wengine ikiwamo kuwekwa ndani na kwamba uhuru uko shakani kwa kila mmoja kuanzia kwa waandishi wa habari hadi kwa wanamuziki.

Lissu ambaye katika tamko lake hilo alikumbusha matukio ya watu kutekwa, kupotea kuuawa aliwataka mawakili wenzake hao kuwachagua wagombea ambao wanaamini wanauwezo wa kutetea uhuru wao na kuwataka kuwakataa wale wote ambao wanashirikiana na maadui wa utawala wa kisheria.

Wakati Lissu akisema hayo, tayari kampeni za Fatma zimeonyesha kuungwa mkono kwa ushabiki wa hali ya juu kutoka kwa wanachama wa TLS ambao tangu mapema wiki hii walianza kuwasili mjini Arusha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa leo.

Udadisi wa gazeti hili uliofanywa jana kwenye viunga kadhaa vya Jiji la Arusha umebaini kuwapo makundi mengi ya mawakili wanaomuunga mkono Fatma, ambapo baadhi walionekana wamevaa fulana zilizokuwa na picha yake.

Gazeti hili limedokezwa kwamba Fatma anaungwa mkono na mawakili wengi vijana ingawa anakabiriwa na upinzani kutoka kwa mawakili wa serikali ambao nao wanatajwa kuunga mkono mgombea mwingine.

Kiti cha urais wa TLS kinawania na wagombea wanne, ukiachia mbali Fatma, yupo Makamu wa Rais wa anayemaliza muda wake, Godwin Ngwilimi, Godwin Mwapongo pamoja na Godfrey Wasonga.

 Inaelezwa uamuzi wa Fatma kujitosa kwenye kinyanganyiro hicho umeamsha joto la uchaguzi huo kuliko ilivyokuwa ikitegemewa awali.

Fatma anapewa nafasi kubwa kutokana na misimamo yake kutoyumba kufahamika vyema pia si mkimya pale panapofaa kuzungumzia ukweli.

Hata hivyo duru za mambo kutoka kwenye mifumo ya chama hicho zinadai kwamba Fatma atakumbana na ushindani mkubwa kutoka Makamu Rais wa sasa Godwim Ngwilimi.

Pia wagombea wengine kama Wasonga na Mwampongo nao si wa kupuuzwa katika kinyanganyiro hicho kutokana na kuwa wanasheria nguli na wenye ushawishi mkubwa ndani ya taaluma ya sheria.

Mbali na rais pia wanachama wa TLS watachagua safu mpya ya uaongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza TLS, wajumbe watakaochaguliwa leo, watakuwa na dhamana ya kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Katika hatua nyingine, mchakato mzima wa kufikia uchaguzi wa leo ulikumbwa na hali ya sintofahamu miongoni mwa wanachama kutokana na kanuni mpya ya uchaguzi ambayo ilipitishwa mapema mwezi uliopita, kuchomekewa kipengele chenye masharti magumu kwa wagombea wa nafasi ya urais.

Kipengele hicho ni (e) kinasema ; “inatoa masharti kuwa mwanachama kuwa hatakuwa na sifa ya kugombea nafasi ya urais kama hatakuwa mtumishi wa umma, mbunge, diwani au kama ana nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi aliwahi kutolea ufafanuzi suala hilo kwa kusema kanuni hizo hazitatumika katika uchaguzi wa mwaka huu, kwamba uchaguzi wa leo utatumia kanuni za zamani.

Wasemavyo wagombea

Kampeni za kuwania urais wa TLS zilifunguliwa jana mchana na zilianza kwa msisimuko wa hali ya juu kutokana na wapiga kura hususani mawakili vijana wake kwa waume kutambiana.

Akijinadi jana jioni mbele ya wajumbe wa TLS, Fatma alisema aliamua kugombea nafasi ya Rais kutokana na kusukumwa kuwatetea wanasheria na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

“Pamoja na nguvu kinzani dhidi ya taaluma ya wanasheria na kazi ya kuhudumia jamii kisheria hivyo ni lazima ajitokeze mtu sahihi wa kuongoza taasisi na huyo mtu ni mimi Fatma Karume,” alisema na kuongeza:

“Sisi ni wanasheria tunazo zana zote, spana, nyundo nk. Ninajua ni zana ipi nitatumia kwa wakati gani kwa hiyo mkinichagua nitahakikisha tunaendelea kufanya kazi zetu za kujitetea wenyewe,kuitetea jamii inayotuzunguka, wananchi wa kawaida na taifa kwa ujumla.

“Tunapata vitisho hata kutaka kufutwa nafikiri ni kwasababu hata sisi tumejiweka mbali na jamii.Kwa mtazamo wangu nafikiri tumepungukiwa katika eneo hili la kuhudumia jamii ya Watanzania.”

“Mkinichagua nitarejesha uhusiano na ushirikiano mzuri baina yetu na jamii,” alisema

Kwa upande Wakili Gwilimi akiomba kura kwa wajumbe hao alisema, imani aliyonayo ni kuwa yuko mbele ya wajumbe ili wamuidhinishe tu kwani tayari wanajua alichowafanyia wakati uliopita.

“Pamoja na kuomba kura yangu nawaombea pia kura timu yangu niliyofanya nayo kazi.

“Ninawahakikishia mimi ni kiongozi imara na madhubuti katika nafasi hii, sisi ni wana taaluma tunaoheshimika, hata wakoloni walipokuja waliitambua taaluma hii kuliko nyingine,” alisema

Kwa upande wake Wasonga alipoitwa kuomba kura mbele ya wajumbe hao hakuweza kujitokeza wala kujulikana kwanini hakuomba kura.

Akiomba kura, Mwamponga alijikuta akilazimika kukatiza hotuba yake kutokana na kujielekeza kulaumu taratibu alizodai kuwa ziliwapendelea baadhi ya wagombea.

Katika madai yake hayo Mwamponga aliwakumbusha wajumbe kuwa ni yeye aliyependekeza utaratibu wa kupanga bajeti ya matumizi nyakati za uchaguzi.

“Nitahakikisha ninawapeleka katika hatua nyingine, mtakuwa na kadi za bima ya afya kwa kutumia fedha ndogo mnazochanga, mimi si kama baadhi ya wagombea unaona kabisa katika kampeni zao kuwa wanatumika na kundi jingine nje ya hii taasisi,” alisema alisema bila kufafanua na kuongeza:

“Nitarejesha uhusiano mzuri kati ya mawakili na polisi, kwa kukutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), ili nimueleze ni namna gani mawakili wanapaswa kukamatwa, pamoja na vyombo vingine vya maamuzi halikadhalika,” alisema Wakili Mwamponga.

Wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ni Makamu wa Rais Rugemeleza Nshala, Mweka Hazina Nicolaus Duhia na wagombea zaidi ya 10 wanaowania nafasi Saba za Baraza la uongozi la TLS,ambapo zaidi ya wajumbe 4000 wanatarajiwa kupiga kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles