28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu ateta kwa uchungu na kaka yake

*Awatumia TLS ujumbe mzito, Familia yaishangaa Serikali, Ummy ajibu, Polisi wakataa uchunguzi kufanywa na mataifa ya nje

Na WAANDISHI WETU -ARUSHA/DAR

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kurejea nchini na kueleza mwenendo wa afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kaka yake mkubwa, Alute Mughwai, amesema ameteta naye kwa njia ya simu na kumweleza atarejea kwenye mapambano.

Mughwai ambaye pia ni msemaji wa familia, alisema hayo jana wakati wa mkutano wa nusu mwaka wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) uliofanyika jijini Arusha.

“Kwanza niwaambie tu Rais wetu wa TLS anaendelea vizuri sana, anawatakia mfanye mkutano huu kwa mafanikio. Kabla sijaingia katika ukumbi huu, nilijaribu kumpigia (simu) mke wake ambaye ni shemeji yangu, lakini badala ya kuipokea, alimpatia Lissu nikazungumza naye,” alisema Mughwai ambaye pia ni wakili.

Alisema jambo la kushangaza na kutia faraja ni kwamba mvumo wa sauti ya Lissu ni ule ule unaojulikana na wengi.

“Ujasiri, hamasa na kujiamini hakujaondoka. Ameniambia piganieni haki zenu na haki za Watanzania, piganieni uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa maoni na hakikisheni kunakuwa na demokrasia na utawala wa sheria katika Tanzania,” alisema Mughwai akimnukuu Lissu.

Alisema wakati alipokuwa akizungumza naye kwa simu, Lissu alimhakikishia kuwa afya yake imeimarika, isipokuwa maumivu katika majeraha ya risasi katika eneo la nyonga na miguuni.

“Rais wetu ufahamu wake umerudi katika hali ya kawaida, anajieleza vizuri, maana yake ni kuwa eneo lote la kiunoni kwenda kichwani yuko sawa, isipokuwa kuanzia kiunoni kwenda miguuni ndilo eneo lililoumizwa sana.

“Sote tunawalaani majahili hawa wasiojulikana, ambao walikusudia kupoteza uhai wake. Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani basi aliye juu yetu? Bila shaka hakuna, tunaamini siku chache zijazo ataungana nasi kuendelea kuipigania nchi yetu,” aliongeza.

 

AZUNGUMZIA KAULI YA SERIKALI

Katika hatua nyingine, Mughwai, alizungumzia kuhusu kauli iliyotolewa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kwamba Serikali ipo tayari kugharamia matibatu ya Lissu popote nje ya nchi, ikiwa tu familia yake itapeleka maombi.

Katika hilo alisema hadi sasa familia  haijaelewa kwa uwazi masharti na nia iliyo nyuma ya tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Alisema kauli ya waziri huyo haieleweki, hivyo inahitaji kufafanuliwa zaidi.

Mughwai, alishangazwa na wito wa Serikali kupitia kwa Waziri Ummy juu ya matibabu ya mbunge huyo, ambaye anastahili haki zote za kutibiwa na Serikali, hasa ikizingatiwa alishambuliwa na kuumizwa akiwa katika eneo lake la kazi.

“Familia haielewi masharti haya yana lengo gani, kwanza hatujui mgonjwa aombe mkopo, nafuu ya mkopo au ya msaada wa matibabu. Hatuelewi na kwa sasa hatutaki masharti katika kumrejesha ndugu yetu katika afya yake.

“Tunashirikiana tangu mwanzo wa tukio hili na Chadema, TLS na wasamaria ambao wengi ni wananchi na watu wengine wa kawaida, wacha tusiwakatishe tamaa hawa waliojitokeza mwanzo kuwa nasi, hawa wenye masharti wasubiri,” alisema Mughwai.

 

UMMY AFAFANUA KAULI YAKE

Jana, Waziri Ummy alilazimika kufafanua kauli yake kupitia mtandao wa Twitter, akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kugharamia matibabu ya Lissu pasipo kupata ridhaa ya familia kwakuwa kiongozi huyo alitolewa katika utaratibu wa matibabu baada ya kupelekwa Nairobi.

Kauli hiyo ya Ummy, ilikuja baada ya Mbowe kukaririwa na vyombo vya habari juzi na jana akihoji utaratibu unaotakiwa na Serikali ili iweze kumtibia Lissu, jambo ambalo alidai kuwa halikuwahi kufanyika kwa wabunge wengine.

Ummy alitoa ufafanuzi huo wakati akimjibu kada wa Chadema, Yericko Nyerere aliyehoji kama endapo wote waliochangia na wanaoendelea kuchangia matibabu ya Lissu wameandikiwa barua kama alivyosubiri yeye.

“Mgonjwa alitolewa kwenye utaratibu wa Serikali alipopelekwa NRB (Nairobi). Sasa gharama/tiba zaidi yahitajika. Serikali inaingiaje bila ridhaa ya familia?” alihoji Ummy kupitia akaunti yake ya Twitter.

Aliongeza kuwa mgonjwa ni mbunge na anahitaji matibabu zaidi, lakini kwa kuwa sasa yupo nje ya utaratibu wa Serikali, ili washiriki, lazima wapelekewe maombi.

 

TLS: WANASHERIA SHAKANI

Akifungua mkutano mkuu wa nusu mwaka, Makamu wa Rais wa TLS, Godwin Ngwilimi, aliwaambia kuwa usalama wa wanasheria uko shakani kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

“Tunawalaani majahili na waovu hawa waliokusudia kuangamiza maisha ya rais wetu, tunahimiza vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi wa tukio lile. Sisi ni chombo ambacho kinahitajika na jamii, Serikali inatuhitaji na hata hawa wauaji wanatuhitaji.

“Kwa nini wajitokeze watu kutuangamiza? Lissu ameshambuliwa kwa risasi, ofisi za IMMMA zilivunjwa na jambo la kushangaza wezi hao hawakuchukua vitu vingine isipokuwa nyaraka, tena walilenga ghorofa ambayo ofisi hizo zipo, lakini wakiziacha ofisi zingine katika ghorofa za chini kwenye jengo hilo,” alisema Ngwilimi.

Kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo, mawakili hao waliomba dua maalumu iliyoongozwa na Wakili Mchungaji Loita Lengai kuwalaani wote walioshiriki katika tukio la kumshambulia kwa risasi Lissu.

 

POLISI: TUTACHUNGUZA WENYEWE

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limeonyesha kutokuwa tayari uchunguzi wa tukio la Lissu kufanywa na vyombo vya mataifa ya nje, likisema linaendelea na uchunguzi wake.

Jeshi la Polisi limefikia hatua hiyo, ikiwa ni siku moja tu tangu Mbowe kutoa wito wa Serikali kukubali vyombo vya nje vifanye uchunguzi dhidi ya watu waliohusika kumshambulia kwa risasi, Lissu ili ukweli ujulikane.

Jana gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa  kuhusu kauli hiyo ya Mbowe, ambaye alisema suala la kuchukua wachunguzi kutoka nje ni la mwenyekiti huyo na kwamba wao wanafanya kazi kitaaluma.

“Sisi tunaendelea na uchunguzi, suala la mtu kuchukua watu wa nje ni yeye. Sisi tunaendelea kufanya uchunguzi, sisi ni ‘professional’ (wataalamu). Hatuwezi kumzuia mtu kuongea, kuna mtu mwingine anaweza kusema mimi siwezi kuendelea mahakamani au siwezi kuendelea na uchunguzi. Ana haki kikatiba kutoa maoni yake kusema lolote, yeye ni mwanasiasa, lakini sisi kama polisi tunaendelea na uchunguzi,” alisema Mwakalukwa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi baada ya kurejea kutoka nchini Kenya alikokuwa kwa siku 15 kufuatilia kwa karibu matibabu ya Lissu,  pamoja na mambo mengine, Mbowe alieleza shaka waliyonayo dhidi ya vyombo vya ulinzi na usalama vya hapa nchini katika kuchunguza suala hilo.

Alikwenda mbali akisema kuwa wanavishuku vyombo hivyo na hata kuwaona ni watuhumiwa namba moja katika tukio hilo kwa kile alichodai kuwa  viashiria vyake vyote tangu linatokea, kauli za baadhi ya viongozi, kusita kwao, kujiosha na mazuio yasiyo na mantiki, vinaweza kumwelekeza mtu yeyote mwenye akili timamu kudai hayo.

Ingawa Mbowe alisema hamjui ni nani ndani ya vyombo hivyo, lakini alidai kuwa si jambo la afya kwa watuhumiwa kujichunguza wenyewe.

Alisema hata wao Chadema pamoja na kwamba kuna mkakati unatengenezwa wa kusema wamehusika kwa sababu ya kugombania vyeo, pia watakuwa tayari kuchunguzwa na hata kuchukuliwa na vyombo hivyo vya nje  ili ukweli ujulikane.

Akijibu madai ya Mbowe ya kuvituhumu vyombo vya ulinzi na usalama kuwa ni watuhumiwa namba moja wa tukio hilo, Mwakalukwa alimtaka awataje wahusika au apeleke taarifa kwa siri ndani ya jeshi hilo.

“Kama ana-suspect, he can mention them, (anaweza kuwataja) because he knows them (kwa sababu anawajua), so its very easy to him even to (kwa hiyo ni rahisi sana kwake hata ku..) kuwatajia hata waandishi wa habari. If you have information deliver those information (kama una taarifa, toa),” alisema Mwakalukwa.

Mwakalukwa alisitiza kuwa kitendo cha kuendelea kulizungumza jambo hilo kunaweza kuharibu mwenendo wa uchunguzi.

Kuhusu namna wanavyofanya kazi na kutumia mbinu za kisayansi, Mwakalukwa alisema: “Sisi polisi tunafanya kazi kisayansi, tunazingatia weledi, tunafanya kazi kwa kuzingatia usasa, usasa inamaanisha nini, tuna tovuti yetu, tuna nini, we are professional.  “Tumepeleleza kesi nyingi kwa kushirikiana na mataifa mbalimbali, leo hii unasema kwamba unataka kufanyaje, ni mawazo yake na hatuwezi kuzuia mawazo ya mtu,” alisema Mwakalukwa.

Juzi Mbowe alisema wamezungumza na vyombo vya uchunguzi kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na vyote viko tayari kuja kutoa msaada.

Alisema vyombo hivyo vinachohitaji sasa ni maombi kutoka Serikali ya Tanzania.

“Kama mnajiamini hawa watu waje kufanya uchunguzi, msibaki tu mnasema ni Chadema wenyewe kwa wenyewe, ruhusuni watu wenye utaalamu wao waweke vielelezo hapa,” alikaririwa Mbowe.

Alisema hapingani na kauli ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuwa vyombo vya ndani havijashindwa kufanya uchunguzi, lakini mtuhumiwa namba moja ni vyombo vya ulinzi na usalama.

Mbowe alisema hadi wao kudai vyombo huru vya uchunguzi kunatokana na madhila ya muda mrefu ambayo vyombo vya ndani vya ulinzi na usalama vimeonyesha havina msaada katika hilo.

Katika hilo, Mbowe alikumbushia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye alidai waliomshambulia wanajulikana na hakuna aliyefikishwa mahakamani.

Zaidi alikumbushia kupotea kwa msaidizi wake, Ben Saanane na kwamba alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu Serikali kuruhusu uchunguzi huru kutoka Scotland Yard, lakini alikataa.

Kauli hiyo ya sasa ya Jeshi la Polisi inafanana na ile iliyotolewa kabla ya hapo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma na Mkuu wa Majeshi nchini, Venance Mabeyo.

 

LISSU ANAPITIA HATUA TATU NGUMU

Wakati polisi wakitoa kauli hiyo, Lissu ambaye alishambuliwa Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma na watu ambao hadi sasa vyombo vya dola havijawabaini, inaelezwa anapitia katika hatua tatu za matibabu katika Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya ambayo baadae yatamwezesha kurejea katika afya yake.

Hatua hizo kwa mujibu wa Mbowe ni mbali na ile ya matibabu ya awali ya kumuimarisha, aliyofanyiwa akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi nchini Kenya aliko hivi sasa.

Matibabu ya awali ya Dodoma, yalielezwa kuweza kumuimarisha Lissu na kumwezesha kusafirishwa hadi Hospitali ya Nairobi ambako bado anaendelea na matibabu.

Kwa mujibu wa Mbowe, hatua ya pili ambayo ndiyo ilikuwa ngumu zaidi, ni ile anayopitia Lissu sasa, kuokoa maisha yake.

Hatua hii inaelezwa kuhusisha kutibu na kufanya upasuaji wa maeneo yaliyoshambuliwa kwa risasi na kuhakikisha kuwa anatoka akiwa salama na kurudi katika hali ya utimamu.

Pamoja na kwamba bado yuko kwenye hatua hii, lakini kwa mujibu wa Mbowe, fahamu zake ziko sawa na akili yake iko timamu kwa asilimia 100.

Hilo lilisaidiwa pia na namna Lissu alivyotoka katika tukio hilo pasipo kuharibika mishipa ya fahamu, jambo ambalo lilielezwa kuwashangaza hata madaktari wanaomtibu.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa itakamilika katika hospitali hiyo hiyo ya Nairobi kwa kuwa kundi la madaktari wanaomhudumia, waliwahakikishia kuwa wana vifaa, uwezo na utaalamu wa kukamilisha awamu hiyo ya matibabu.

Baada ya awamu hiyo, huenda sasa Lissu akawa imara zaidi na kuhimili mikikimikiki ya safari ya kupelekwa nchi nyingine kwa hatua ya tatu ambayo itahusisha mazoezi.

Tayari Mbowe alieleza kuhusu jitihada za watu mbalimbali kutaka Lissu atibiwe katika nchi sita tofauti, akiwamo Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.

Nchi ambazo baadhi ya makundi hayo yanataka Lissu akatibiwe ni Afrika Kusini, India, Ubelgiji, Ujerumani, Uingereza na Marekani.

 

Habari hii imeandaliwa na ABRAHAM GWANDU (ARUSHA), AGATHA CHARLES Na AZIZA MASOUD (DAR ES SALAAM)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles