31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu amtakia heri Lowassa

LNa NORA DAMIAN DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema anamtakia kila la heri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye amerudi katika chama chake cha zamani cha CCM.

Lowassa alijiunga Chadema Julai 2015, baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mchakato wa kutafuta mgombea wa urais ndani ya CCM na baada ya kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani, alipambana na Rais Dk.  John Magufuli ambapo alikuwa nyuma 6,072,848 na Magufuli  huku Rais Dk. John Magufuli akishinda kwa kura 8,882,935.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Lissu alisema walimkaribisha Lowassa na kumpatia majukumu ya kuwaongoza kwenye mapambano ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 na aliweza kutekeleza majukumu hayo vizuri. 

“Nimeulizwa na watu wengi sana juu ya maoni yangu kuhusu Mzee Edward Ngoyai Lowassa kurudi CCM. Nilisema nasubiri hili vumbi la hizi siku chache zilizopita litulie kwanza ndipo niweze kusema maoni yangu. Sasa ni muda mwafaka kufanya hivyo.

“Mzee Edward Lowassa mwenyewe amesema amerudi nyumbani. Maana yake ni kwamba alikuwa ugenini tangu Julai 2015. Hakutuhonga wala hakununua chama chetu kama tulivyotukanwa huko nyuma. 

“Tulimkaribisha na kumpatia majukumu ya kutuongoza kwenye mapambano ya 2015. Na alitekeleza majukumu hayo vizuri kwa kadiri alivyoweza na kadiri tulivyomwezesha. Matunda ya kazi yake na ya kazi yetu yanajulikana.

“Sasa mwendo wa ugenini umemshinda. Misalaba ya upinzani imekuwa mizito sana. Ameamua kurudi ‘nyumbani’ kupumzika,” alisema Lissu.

Alisema badala ya kumlaani kuondoka katika chama chao, anamtakia mapumziko mema nyumbani kwake na kwamba wao wataendelea na safari yao ya Kanani.

“Mimi namtakia kila la heri na mapumziko mema ‘nyumbani’ kwake. Sisi tutaendelea na safari yetu ya Kanani,” alisema.

Naye mwanahabari nguli, Ansbert Ngurumo, alisema waliomkaribisha Lowassa, walifanya jambo la maana kwa wakati ule na kwamba amefanya jambo la maana kuondoka kwa wakati huu.

“Ukifanya siasa na harakati kwa fomula za kifizikia utakwama. Ni suala la kujitazama, uwe mwanasiasa, mwanahabari, mwanasheria, mfanyabiashara, mkulima, mhadhiri, kiongozi wa dini na hata mchawi. Tunatafuta ukombozi ule ule kila mmoja kwa kutumia karama yake. Hatutafuti sifa ya mtu au kundi fulani,” alisema Ngurumo. 

KUREJEA CCM

Lowassa alihama CCM wakati wa vuguvugu la kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 baada ya kushindwa katika kura za maoni za kuwania nafasi ya kuipeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa urais.

Alipata fursa hiyo kupitia Chadema kwa mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Lowassa ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, aliwahi kusema kuwa Rais Dk. John Magufuli alimuomba arejee CCM wakati wa mazungumzo yao walipokutana mwanzoni mwa mwaka jana.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema ujio wa mwanasiasa huyo mkongwe hapa nchini unaashiria kwamba, chama hicho kinaanza kazi ya kujenga Taifa.

“Kama alivyosema Waziri Mkuu Mstaafu, Lowasa amerudi nyumbani, tunaanza kazi ya kujenga taifa letu na kulinda udugu wetu,” alisema Dk. Bashiru.

Uamuzi huo wa Lowassa kurejea ndani ya CCM unaonekana kuivuruga kimkakati Chadema ili  kufikia malengo yake ya kisiasa kuelekea Ikulu mwaka 2020.

Tukio hilo ambalo limeingia katika orodha ya mambo ambayo yanaonekana kutibua mipango ya kisiasa ya chama hicho kikuu cha upinzani kushika dola, ni uamuzi wa kushtukiza alioufanya aliyekuwa mgombea wao wa urais mwaka 2015.

Lowassa ambaye katika uchaguzi huo wa 2015 alitoa upinzani mkali kwa Rais Dk. John Magufuli akishika namba mbili kwa wingi wa kura, kurejea kwake CCM kunakuja katika wakati ambao Chadema inapitia katika hali tofauti na ngumu kisiasa.

Waziri Mkuu huyo wa zamani ameondoka ndani ya Chadema katika kipindi ambacho Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, yuko mahabusu kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kufutiwa dhamana.

Pamoja na hilo, pia ameondoka wakati ambao viongozi wa juu wa chama hicho karibu wote wakiwa wanakabiliwa na kesi mahakamani.

Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na manaibu wake, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na makamu wake ambaye pia ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Matiko aliye mahabusu pamoja na Mbowe tangu Novemba mwaka jana kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Viongozi wengine ni wabunge, Ester Bulaya (Bunda), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na John Heche wa Tarime Vijijini.

Viongozi hao wanakabiliwa na kesi ya jinai ya kufanya maandamano bila kibali yaliyoshuhudia  kuuawa kwa kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi  mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Wanakabiliwa na kesi hiyo ya jinai yenye mashtaka 13 yakiwamo ya uchochezi, uasi na kuhamasisha wafuasi wao kuandamana. 

Uamuzi wa Lowassa kurudi CCM ambao umeonekana kuacha midomo wazi kwa pande zote na zaidi kushtua Chadema kutokana na viongozi wake wengi kutokuwa na taarifa, umefanyika katika wakati ambao pia Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu akiwa nje ya Tanzania akiendelea kuuguza majeraha aliyoyapata kutokana na kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles