25.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

Lissu akoleza moto Ukuta

Pg 1Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI hofu ikiendelea kutanda kuhusu hatma ya kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Septemba mosi mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu amesema dhamira ya kufanya mikutano hiyo ipo pale pale hata kama wamezuiwa.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, ametoa kauli hiyo  ikiwa tayari kuna kauli kadhaa za viongozi Chadema kuhusu msimamo wa kufanyika mikutano hiyo ikiwamo ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Meshack Micus.

Onyo la kuzuia kufanyika   mikutano hiyo, lilitolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli  wakati akiwa kwenye ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambako alizungumza na wananchi  wa Manyoni Singida na kutoa onyo kwa watakaoanzisha maandamano.

Akizungumza nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  Dar es Salaam jana, Lissu alisema   hakuna anayekubaliana na maagizo yaliyotolewa kwamba wasifanye mikutano ya  siasa.

Lissu ambaye alifika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi   inayomkabili ya kutoa lugha na chapisho la uchochezi, alisema Rais Magufuli na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), hawana mamlaka ya kuzuia mikutano ya  siasa.

Mbunge huyo aliyekuwa akizungumza kwa kujiamini, alisema kauli zinazotolewa za kuzuia kufanyika  mikutano ya  siasa nchini zina taswira ya udikteta uchwara wa kiongozi aliyepo madarakani.

“…ukitaka kujua huyu ni dikteta uchwara angalia hata kauli anazozitoa, zimekaa kiuchwara uchwara tu.  Mbona yeye kachaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM na anafanya mikutano yake, kwa nini mingine izuiwe?” alihoji Lissu na kusema:

“Kama kuna polisi wanaonisikia wakati nazungumza  haya, basi wanisikilize vizuri anachosema, kwa sababu  msimamo wao upo pale pale,” alisema.

Alisema ingawa kuna kesi kadhaa mahakamani,  haziwazuii kufanya kitu wani maisha yapo pale pale.

“….nyie anagalieni hata mashtaka yenyewe katika kesi zinazofunguliwa ndiyo haya yaliokaa Kimagufuli…Magufuli tu,” alisema.

Hata hivyo,   baadhi ya wafuasi na viongozi wa Chadema walionekana kumzuia Lissu kutoendelea kuporomosha maneno hayo ambayo yalionekana kuwa makali na kuigusa serikali moja kwa moja.

Lissu alionekana kukubaliana na jambo hilo, kabla ya kuondoka na viongozi hao ambao walimtaka watoke katika eneo hilo la mahakama.

Upelelezi kesi yake wakamilika

Wakati huohuo, upelelezi wa kesi inayomkabili mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wenzake watatu umekamilika.

Mbali ya Lissu (Chadema), wengine katika kesi hiyo ni mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bernad Kongola alisema Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Alidai  licha ya kukamilika  upelelezi wa kesi hiyo,  mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Idrissa hajafika mahakamani kutokana na taarifa walizozipata kwamba bado anaumwa.

Hata hivyo, Wakili Kongola aliiomba mahakama itoe hati ya wito wa kumwita Idrissa    kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kuunganishwa na wenzake katika kesi hiyo.

Baada ya kueleza hayo, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo na kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kuwasomea maelezo ya awali.

Hakimu Mwijage aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 29, mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles