32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AKAMATWA KWA BOMBARDIER

Na Tunu Nassoro

-DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kufanya mkutano na waandishi wa habari, Polisi jijini Dar es Salaam imemkamata mwanasiasa huyo na kumhoji kwa makosa mawili.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walipotafutwa ili kuzungumzia sababu ya kukamatwa kwa Lissu, hawakuwa tayari baada ya Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum, Lucas Mkondya, kusema hayupo ofisini huku Mkuu wa Upelelezi Kanda, Camillius Wambura, simu yake ikipokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni dereva  na kusema bosi wake hayupo.

Kauli ya Chadema

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, aliiambia MTANZANIA kwamba, Lissu alikamatwa jana saa 7:30 mchana wakati akitoka mahakamani.

Muda mfupi baada ya kuanza kusambaa taarifa za kukamatwa kwa Lissu, Makene aliandika kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa. “Tumetoka Mahakama ya Kisutu muda huu ambapo Lissu alikuwa na kesi ya tuhuma za uchochezi (uchochezi one) lakini pia alikuwa ni wakili kwenye kesi inayomkabili Yericko Nyerere hapa hapa Kisutu.

“Wakati gari la Lissu likiwa liko getini tayari kwa kuondoka likazuiwa, lilipokuwa likirudi nyuma gari jingine likiwa na polisi wenye silaha likasimama.

“Walimwamuru ashuke kwenye gari lake na apande gari jingine la kwao kwa ajili ya kuelekea Central Police,” alisema Makene.

Akizungumza na MTANZANIA jana jioni, Makene alisema Lissu amehojiwa kwa makosa mawili ya kumkashfu Rais na jingine la uchochezi.

Makene alisema Lissu aliyekuwa na wakili wake, Faraji Mangula, aliwaambia polisi kwamba hajafanya uchochezi wala kumkashfu Rais.

Alisema Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, hakutoa taarifa zaidi polisi na badala yake alisema atazitoa mahakamani.

“Kwa sasa uwezekano wa kumpa dhamana leo ni mdogo sana, tunachofanya ni kujiandaa kama kesho hawatampeleka mahakamani mapema, tutaiomba mahakama iamuru polisi kumfikisha mahakamani,” alisema Makene.

Akifafanua zaidi jinsi Lissu alivyokamatwa, Makene alisema polisi walifika na gari tatu, mbili zikalizuia gari la mwanasheria huyo na jingine likambeba kumpeleka kituoni.

Alisema awali walipofika polisi, walizuiwa kwa maelezo kwamba, hairuhusiwi kwa mtu yeyote hata kama ni wakili kufika kwenye kituo hicho.

Polisi

MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema. “Sijui lolote kuhusu kukamatwa kwake kwa kuwa niko ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku,” alisema Mkondya.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camillius Wambura ambapo simu yake ilipokewa na dereva wake na kusema kuwa hawapo jijini Dar es Salaam.

“Mimi ni dereva wake sisi (pamoja na Wambura) hatupo Dar es Salaam kwa sasa tupo Rufiji kwa shughuli za kiofisi,” alisema Dereva huyo.

Juhudi za kumtafuta msemaji wa jeshi la polisi zilikwama kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila majibu.

Lissu  na Bombardier

Agosti 20, mwaka huu Lissu alisema ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400, iliyotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa Julai, imekamatwa nchini Canada kwa amri ya mahakama, kutokana na deni la Dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) ambalo Serikali inadaiwa na mkandarasi iliyemfukuza nchini mwaka 2009.

Alisema  amri hiyo imetolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, baada ya mkandarasi, Stirling Civil  Engineers Ltd, kufungua shauri akiishtaki Serikali ya Tanzania kwa kuvunja mkataba wake wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill mpaka Bagamoyo  mwaka 2009.

Alisema Serikali inadaiwa fedha hizo (dola milioni 38.7) na Kampuni ya Stirling Civil  Engineers Ltd,  baada ya kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill mpaka Bagamoyo  na kusababisha deni hilo. Alisema awali Serikali ilipaswa kulipa dola za Marekani milioni 25, kabla ya riba.

Alisema Desemba 2009, shauri hilo lilifunguliwa na baadaye Juni 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ilitoa tuzo ambayo imetambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania la takribani Dola za Marekani milioni 25 pamoja na riba ya asilimia nane.

“Licha ya jitihada mbalimbali za kutaka kulipwa deni hilo  kufanyika, hadi sasa imefika miaka saba Serikali ya Tanzania bado haijalilipa, ucheleweshwaji wa malipo umesababisha deni kuongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 38 kufikia Juni 30, mwaka huu.

“Kutokana na hali hiyo, kampuni hiyo ya ujenzi iliamua kuomba amri kutoka  Mahakama Kuu ya Montreal, nchini Canada, kukamata mali zote  za Tanzania zilizopo katika kampuni ya Bombardier, zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400. Sasa ndege hiyo imekamatwa na inashikiliwa Canada na wadeni wetu,” alisema Lissu.

Alisema ili kutafuta mwafaka wa suala hilo, wiki mbili zilizopita Serikali ililazimika kutuma ujumbe wake kwa ajili ya mazungumzo  na kampuni hiyo.

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, akishirikiana na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Zoka, walikutana na mdeni huyo ambaye alikubali kuiachia ndege hiyo  endapo yatafanyika malipo ya awali ya dola milioni 12.5.

“Endapo malipo hayo yatafanywa na Serikali, kampuni hiyo itaondoa tishio la mnada wa lazima wa Bombardier Q400, hili suala  ni la  kweli na ushahidi wa yote tuliyoyazungumza  kwa nyaraka tunazo  kama Serikali itajitokeza kubisha. Kuna Watanzania wazalendo waliomo ndani ya Serikali hii hii ambao wametupa hizi nyaraka.

“Mimi mwanasheria, natakiwa nisitaje chanzo, lakini mjue tuna nyaraka za kuthibitisha kila tulichokisema, mjue Mahiga alisisitiza mazungumzo haya yawe siri  kuepuka suala hili kujulikana hadharani,” alisema Lissu.

Alisema suala la kukamatwa kwa ndege hizo linaibua maswali mengi yanayohitaji majibu ya Serikali, ikiwamo sababu zilizofanya kuvunjwa kwa mkataba huo wa  mkandarasi huyo aliyeishitaki Serikali.

Alisema Serikali pia inapaswa kutoa ufafanuzi kwa nini ilishindwa kulipa deni la awali na kusababisha kuongezeka kwa sababu ya riba.

“Hayo maswali ni muhimu kupatiwa majibu ya kweli na sahihi, kusababisha hasara kwa mamlaka za Serikali ni kosa kubwa la jinai, kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi,” alisema Lissu.

Alisema kiongozi aliyevunja mkataba huo anapaswa achukuliwe hatua kama ilivyofanywa kwa mawaziri wa zamani, Daniel Yona na Basil Mramba, waliopatikana na hatia ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni tisa kwa kitendo chao cha kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart Assayers ya Marekani.

Serikali yajibu

Siku moja baada ya Lissu kutoa taarifa hizo, Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa, ilimjibu akikiri kushikiliwa kwa ndege hiyo huku akisema mgogoro huo umechochewa na baadhi ya wanasiasa.

“Ununuzi wa ndege ya tatu ya Bombadier umeingiliwa na mgogoro uliotengenezwa na wanasiasa na watu wasioitakia mema Tanzania, Wanasiasa waliotengeneza mgogoro huo wanahujumu maendeleo ya nchi na usalama wa raia”- alisema Zamaradi Kawawa

Alisema  ndege hiyo ambayo ilikuwa inatarajiwa kuingia nchini Julai sasa itaingia muda si mrefu na kuwataka Watanzania waiamini serikali ya Tanzania iliyopo chini ya Rais John Pombe Magufuli “Ndege ya tatu ya Bombardier ipo na inakuja kwahiyo wananchi waiamini Serikali yao ila serikali imesikitishwa na ushiriki wa wanasiasa na baadhi ya watu kuhujumu maendeleo ya nchi.

“Watanzania tuwe wazalendo kulinda, kutetea na kukabiliana na hujuma zozote zinazorudisha nyuma maendeleo ya Nchi, tuunge mkono jitihada za Rais Magufuli  katika kuleta maendeleo bila kujali itikadi ya chama, kabila au dini” alisema Zamaradi Kawawa.

Kwa siku za karibuni, Lissu Tundu Lissu alikamatwa  Julai 20, katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akijiandaa kuelekea nchini Kigali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles