29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AKAA SAA 52 MAHABUSU

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

HATIMAYE Mwanasheri Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameachiwa kwa masharti ya dhamana.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alidhaminiwa na mawakili wake Omari Msemo na Fred Kiwhelo, ambapo ametakiwa Agosti 28 Jumatatu, kwa maelezo zaidi.

Baada ya kutoka kwa dhamana alifuatwa na waandishi wa habari, lakini alishauriwa na mwanasheria wake Peter Kibatala asizungumze jambo lolote kwa sasa, kisha akaingia kwenye gari.

Lissu alikamatwa Agosti 22 mwaka huu saa saba mchana na kuachiwa jana saa 11 jioni, ambapo amekaa mikononi mwa polisi kwa muda wa sasa 52 akiwa mahabusu.

Alikamatwa wakati akitokea Mahakama ya Kisutu ambapo alikuwa na kesi ya tuhuma za uchochezi, huku akiwa wakili katika kesi inayomkabili kada wa chama hicho, Yericko Nyerere.

Mwanasiasa huyo alikamatwa siku chache baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuzuiliwa kwa ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400.

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene aliliambia MTANZANIA kwamba Lissu alihojiwa kwa makosa mawili ya kumkashifu Rais na jingine la uchochezi.

Hata hivyo wakili wake, Faraji Mangula aliwaambia polisi kwamba hajafanya uchochezi wala kumkashifu Rais.

Lissu na Bombardier

Agosti 20, mwaka huu Lissu alisema ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400, iliyotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa Julai, imekamatwa nchini Canada kwa amri ya mahakama, kutokana na deni la Dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) ambalo Serikali inadaiwa na mkandarasi iliyemfukuza nchini mwaka 2009.

Alisema amri hiyo imetolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, baada ya mkandarasi, Stirling Civil Engineers Ltd, kufungua shauri akiishtaki Serikali ya Tanzania kwa kuvunja mkataba wake wa ujenzi wa barabara kutoka Wazo Hill mpaka Bagamoyo mwaka 2009.

Alisema Serikali inadaiwa fedha hizo (dola milioni 38.7) na Kampuni ya Stirling Civil Engineers Ltd, baada ya kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka Wazo Hill mpaka Bagamoyo na kusababisha deni hilo.

Alisema awali Serikali ilipaswa kulipa Dola za Marekani milioni 25, kabla ya riba.

Alisema Desemba 2009, shauri hilo lilifunguliwa na baadaye Juni 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ilitoa tuzo ambayo imetambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania la takribani Dola za Marekani milioni 25 pamoja na riba ya asilimia nane.

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, akishirikiana na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Zoka, walikutana na mdeni huyo ambaye alikubali kuiachia ndege hiyo endapo yatafanyika malipo ya awali ya dola milioni 12.5.

Serikali yajibu

Siku moja baada ya Lissu kutoa taarifa hizo, Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa, ilijibu hoja hiyo ambapo alikiri kushikiliwa kwa ndege hiyo, huku akisema mgogoro huo umechochewa na baadhi ya wanasiasa.

“Ununuzi wa ndege ya tatu ya Bombadier umeingiliwa na mgogoro uliotengenezwa na wanasiasa na watu wasioitakia mema Tanzania, Wanasiasa waliotengeneza mgogoro huo wanahujumu maendeleo ya nchi na usalama wa raia,” alisema.

Mahakamani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,  imekwama kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema)  kwa sababu anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa aliieleza  mahakama kuwa Lissu anashikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Kishenyi, aliomba  kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea  kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka na ikapendekezwa iendelee kusikilizwa Agosti 28, mwaka huu.

Wakili Peter Kibatala, aliomba kufikisha ujumbe kwa Jeshi la Polisi kuwa walichokifanya ni dharau kwa mahakama.

Alidai  wanaomshikilia mshtakiwa wanafahamu ana kesi kwa nini wasimpeleke mahakamani aendelee na kesi yake.

Kishenyi, alidai  hadhani kama polisi waliokuwa na umuhimu wa kufika mahakamani hapo kwa kuwa yeye yupo na  dhamana yake ipo wazi, Lissu anashikiliwa na polisi. Kesi imeahirishwa hadi Agosti, 28 mwaka huu.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Anadaiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa: “Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote.

“Huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene,’’ alisema.

Katika kesi hiyo, tayari mashahidi wawili  wa upande wa mashtaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Stafu Sajenti Ndege wametoa ushahidi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles