24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AIBUKA NA BOMBARDIER

NA AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

 

MWANASHERIA Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ameibuka na madai mapya akisema ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400, iliyotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa Julai, imekamatwa nchini Canada kwa amri ya mahakama, kutokana na deni la dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) ambalo Serikali inadaiwa na mkandarasi iliyemfukuza nchini mwaka 2009.

 

Amesema amri hiyo imetolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, baada ya mkandarasi, Stirling Civil  Engineers Ltd, kufungua shauri akiishtaki Serikali ya Tanzania kwa kuvunja mkataba wake wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill mpaka Bagamoyo  mwaka 2009.

 

Jana gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ili kuzungumzia suala hilo, lakini akasema atafutwe leo kwa sababu tayari yupo nyumbani.

 

Hata hivyo, hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kwenye ukurasa wake wa twitter, alihoji ilipo ndege hiyo, iliyotarajiwa kuwasili nchini Julai.

 

Kupitia ukurasa huo, Zitto aliandika: ‘Waziri@Mbarawa Serikali iliahidi Bungeni kuwa mwezi Julai mtapokea ndege nyingine Bombardier. Leo ni August imepinduka. Ndege zipo wapi?’

 

Kutokana na ujumbe huo, Profesa Mbarawa alimjibu: “Mhe. Ni kweli kabisa ahadi ilikuwa Julai, kuna taratibu za mwisho zinafanywa kabla ya kuwasili, hivyo itawasili tu.”

 

Baada ya jibu hilo la Profesa Mbarawa, Zitto alihoji tena: “Sababu za kuchelewa ni nini? Delay (uchelewaji) ya mwezi mzima siyo dalili njema ndugu Waziri. Ni kwasababu hamjalipa au zimezuiwa na wanaotudai?” Profesa Mbarawa hakuijibu twitter hiyo.

 

Alichosema Lissu jana

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Lissu alisema Serikali inadaiwa fedha hizo (dola milioni 38.7) na Kampuni ya Stirling Civil  Engineers Ltd,  baada ya kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill mpaka Bagamoyo  na kusababisha deni hilo.

 

Alisema awali Serikali ilipaswa kulipa dola za Marekani milioni 25, kabla ya riba.

 

Alisema Desemba 2009, shauri hilo lilifunguliwa na baadaye Juni 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ilitoa tuzo ambayo imetambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania la takribani Dola za Marekani milioni 25 pamoja na riba ya asilimia nane.

 

“Licha ya jitihada mbalimbali za kutaka kulipwa deni hilo  kufanyika, hadi sasa imefika miaka saba Serikali ya Tanzania bado haijalilipa, ucheleweshwaji wa malipo umesababisha deni kuongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 38 kufikia Juni 30, mwaka huu.

 

“Kutokana na hali hiyo, kampuni hiyo ya ujenzi iliamua kuomba amri kutoka  Mahakama Kuu ya Montreal, nchini Canada, kukamata mali zote  za Tanzania zilizopo katika kampuni ya Bombardier, zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400. Sasa ndege hiyo imekamatwa na inashikiliwa Canada na wadeni wetu,” alisema Lissu.

 

Alisema ili kutafuta mwafaka wa suala hilo, wiki mbili zilizopita Serikali ililazimika kutuma ujumbe wake kwa ajili ya mazungumzo  na kampuni hiyo.

 

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, akishirikiana na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Zoka, walikutana na mdeni huyo ambaye alikubali kuiachia ndege hiyo  endapo yatafanyika malipo ya awali ya dola milioni 12.5.

 

“Endapo malipo hayo yatafanywa na Serikali, kampuni hiyo itaondoa tishio la mnada wa lazima wa Bombardier Q400, hili suala  ni la  kweli na ushahidi wa yote tuliyoyazungumza  kwa nyaraka tunazo  kama Serikali itajitokeza kubisha. Kuna Watanzania wazalendo waliomo ndani ya Serikali hii hii ambao wametupa hizi nyaraka.

 

“Mimi mwanasheria, natakiwa nisitaje chanzo, lakini mjue tuna nyaraka za kuthibitisha kila tulichokisema, mjue Mahiga alisisitiza mazungumzo haya yawe siri  kuepuka suala hili kujulikana hadharani,” alisema Lissu.

 

Alisema suala la kukamatwa kwa ndege hizo linaibua maswali mengi yanayohitaji majibu ya Serikali, ikiwamo sababu zilizofanya kuvunjwa kwa mkataba huo wa  mkandarasi huyo aliyeishitaki Serikali.

 

Alisema Serikali pia inapaswa kutoa ufafanuzi kwa nini ilishindwa kulipa deni la awali na kusababisha kuongezeka kwa sababu ya riba.

 

“Hayo maswali ni muhimu kupatiwa majibu ya kweli na sahihi, kusababisha hasara kwa mamlaka za Serikali ni kosa kubwa la jinai, kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi,” alisema Lissu.

 

Alisema kiongozi aliyevunja mkataba huo anapaswa achukuliwe hatua kama ilivyofanywa kwa mawaziri wa zamani, Daniel Yona na Basil Mramba, waliopatikana na hatia ya kusababishia Serikali hasara ya Sh bilioni tisa kwa kitendo chao cha kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart Assayers ya Marekani.

 

“Sasa tunataka kujua nani atawajibika kijinai katika suala hili la kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 87, ambayo imepeleka Bombardier yetu na mali zetu nyingine kukamatwa nchini Canada,” alisema Lissu.

 

Adai kufuatwafuatwa na polisi

 

Katika hatua nyingine, Lissu alidai kuwa kwa siku za karibuni watu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, vimekuwa vikimfuatafuata kila anakokwenda.

 

Amesema wamekuwa wakimfuata huku wakitumia gari dogo, hivyo akawataka waache kumfuata yeye, badala yake wawatafute majambazi.

 

“Hapa (kwenye mkutano na waandishi wa habari), polisi mpo, muwapelekee ujumbe mabosi zenu, muache kutufuata tunaofanya kazi ya kuiwajibisha Serikali, mkakamate majambazi,” alisema Lissu.

 

Mapendekezo

Kutokana na hali hiyo alisema, Lissu alitoa mapendekeza matatu ikiwamo kutaka Bunge kuunda kamati teule ya Bunge  kuchunguza suala hilo  na mengine ya uvunjaji wa sheria na mikataba ambayo imesababisha nchi kuingia katika hasara.

Alisema pendekezo la pili ni Bunge na vyama vya siasa kushinikiza serikali kuweka hadharani kesi zote ambazo zimefunguliwa ama zinatarajia kufunguliwa dhidi ya serikali, katika mahakama za kimataifa za usuluhishi ili wananchi wafahamu gharama na hasara ambazo nchi inakabiliana nazo.

Katika pendekezo la tatu alisema ni muhimu kurejesha mjadala wa Katiba mpya utakaodhibiti mamlaka ya watendaji wakuu wa serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles