26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AFYATUKA TENA

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM


WAKATI Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akiwa bado anakabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi, amefytuka tena na kutoa maneno mazito juu ya viongozi wa Serikali, huku akisema kwa mujibu wa sheria za nchi, anaweza kukamatwa, lakini si kufungwa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Lissu pia alisema amepata taarifa kutoka kwa mmoja wa askari polisi kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atafikishwa mahakamani wakati wowote kutokana na kauli alizozitoa juu ya  masheikh wa Uamsho. Gazeti hili halikuweza kujiridhisha juu ya usahihi wake.

Lissu ambaye baadhi ya kauli zake gazeti hili haliwezi kuziandika kwa sababu za kimaadili, alisema pia watu ambao wanataka rais aongezewe muda wa kuongoza baada ya miaka 10 ya kikatiba, wabaki na kile alichokiita ni ujinga wao.

“Kuna watu wanaongea habari za kuongeza muda wa urais, tuwaambie tu huo wanaoleta ni ujinga, hivyo kaeni na ujinga wenu nyumbani kwenu,” alisema Lissu.

 

LOWASSA MAHAKAMANI

Akizungumzia taarifa za Lowassa kufikishwa mahakamani, alisema amezipata kutoka kwa mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.

Lissu alisema kuwa aliwasiliana na ofisa huyo jana asubuhi na kumtaka ajiandae kwa kesi hiyo ambayo ipo mbioni kupelekwa mahakamani.

“Nina taarifa nimeambiwa leo na lipolisi likubwa kabisa, maana hata wao hawafurahi sana, nimeambiwa jiandaeni mheshimiwa Lowassa atafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa uchochezi kwa sababu ya kuzungumzia uonevu wanaofanyiwa masheikh wa Uamsho,” alisema Lissu.

Alipoulizwa endapo kinga za kushtakiwa kwa viongozi, inawahusu pia mawaziri wakuu wastaafu, alisema kinga inamuhusu rais aliyepo madarakani pekee na mambo aliyofanya wakati akiwa Ikulu.

Hata hivyo, alisema kinga hiyo kwa marais, imechangia viongozi wengi wakiwa madarakani kufanya mambo mabaya.

“Kuna marais ambao ni wahalifu wakiwa marais, tunatakiwa tuwe na usawa ndani ya sheria, ikiwa muhalifu ukiwa Ikulu tukushughulikie au ukitoka tukushughulikie,” alisema Lissu huku akitolea mfano kwa Rais wa Brazil, Lula Da Silva.

Alisema Da Silva, sasa amehukumiwa kifungo cha miaka tisa baada ya kutoka madarakani kwa makosa ambayo aliyayafanya akiwa rais.

Alisisitiza kiongozi anapaswa kuwa na kinga kwa sababu ni msafi na si sababu ya uongozi wake.

Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifika kwa mara ya kwanza polisi Juni 27, mwaka huu kwa wito wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kuhojiwa kwa saa nne.

Aliripoti tena Makao Makuu ya Polisi Juni 29, Julai 13 na ametakiwa kuripoti Julai 20.

 

MAHABUSU SI PAZURI

Alipoulizwa kuhusu kauli anazozitoa ambazo mara nyingi huwa zinatafsiriwa ni uchochezi na huwa zinamtia hatiani, Lissu alisema hapendi kukamatwa, lakini mazingira yanamfanya aishi hivyo.

“Mimi sipendi kukamatwa, niwaambie mahabusu si mahala pazuri pa kwenda, hasa ukiwa huna kosa, inafika mahali inabidi uamue.

“Nipige magoti na kupelekwa machinjioni kama mwanakondoo mtiifu au nipelekwe machinjioni nikiwa napiga kelele dunia nzima isikie? Sitanyamaza na wenzangu hawatanyamaza,” alisema Lissu.

Alisema wapinzani wataongea na kufanya kile wanachopaswa kwa mujibu wa katiba na sheria na si kunyamaza kwa sababu ya mtu.

“Tutafanya kile tunachotakiwa kufanya, tutasema yanayohitajika, kama kuna mtu anafikiria wajibu wake kutukataza tusiseme ama tukisema tuadhibiwe na yeye atimize wajibu wake,” alisema Lissu.

 

MAKOSA YA UCHOCHEZI

Akifafanua kuhusu makosa ya uchochezi ambayo watu wamekuwa wakishtakiwa nayo, alisema yanatokana na sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 1953.

“Ukweli wa Mungu ni kwamba sheria ya huduma ya vyombo vya habari ambayo inawapa mamlaka ya kuwaumiza someni vifungu vyote vinavyohusu uchochezi, tumetoka navyo kwenye sheria zetu tangu mwaka 1953.

“Ukisikia mtu ameshtakiwa kwa uchochezi, anahukumiwa kwa vifungu vya sheria ya mwaka 1953 na kuanza kutumika  mwaka 1958, vikaanza kutumika kwa waandishi wawili na baadae vikawekwa kwenye sheria ya magazeti,” alisema Lissu.

Alisema vitu ambavyo sheria hiyo inavitaja kuwa si uchochezi ni pamoja na kauli za kupinga Serikali, matendo ama programu za Serikali.

Kitu kingine alichokitaja ni kufanya vitendo ambavyo vina lengo la kuondoa  Serikali madarakani kwa kufuata njia zilizowekwa.

“Hivyo watatukamata tu, lakini sheria haiwezi kutufunga,” alisema Lissu.

 

KESI ZINAZOMKABILI

Akizungumzia kesi zinazomkabili, Lissu alisema hadi sasa anazozikumbuka ni nne.

“Nimefutiwa moja, imebaki kesi ya uchochezi one (namba moja) na two (mbili), dikteta uchwara one (namba moja), two (mbili). Hizi zote ni kuanzia Juni 28 kabla sijawa Rais wa TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika),” alisema Lissu.

 

KAMATA KAMATA

Akizungumzia mwenendo wa wakuu wa wilaya na mikoa wanaoamuru viongozi wa kisiasa wawekwe ndani kwa saa 48, Lissu alisema wameanza kuwashughulikia.

Alisema katika jimbo lake, amemfungulia mkuu wa wilaya mmoja kesi mbili, na kumdai fidia ya Sh milioni 200 kwa kila kesi.

“Kuna Mkuu wa Wilaya anaitwa Milanzi (Francis) ni mkuu wa wilaya kule jimboni kwangu Singida Mashariki, alijaribu kugombea ubunge mwaka 2010, tangu ameletwa alishakamata wenyekiti wa vijiji 11.

“Nimemfungulia kesi mbili za madai, kila moja namdai Sh milioni 200 na tisa nyingine zinamfuata kwa kila aliyemkamata atalipa, na tunamfungulia yeye peke yake, hatutaki ugomvi na Serikali,” alisema Lissu.

Alisema kesi zinazohusu Serikali mara nyingi huwa zinachelewa na wao hawataki hivyo.

“Ukitaka ugomvi na Serikali utaambiwa toa notisi ya siku 90, hatutaki kucheleweshwa na ukitaka ugomvi watamuwekea mawakili kwa hiyo atatetewa na mawakili wa Serikali na Mwenyekiti pia (Freema Mbowe) ameshaanza uko Hai (kumshtaki mkuu wa wilaya),” alisema Lissu.

 

KUFUTWA KWA TLS

Akizungumzia taarifa za kutaka kufutwa kwa TLS, ambayo yeye ni rais wake, alisema ameshangazwa na hatua hiyo na kwamba Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kufanya uamuzi huo.

“Wanasema kuna mpango wa kuifuta TLS na kuwafanya wawe idara chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, tutakuwa nchi ya kwanza duniani kufuta chama huru cha mawakili hata Idd Amin Dada hajawahi kufuta chama kama hiki cha Uganda.

“Mandela alikuwa wakili, lakini Nelson Mandela na Oliver Tambo wakati wanapigania uhuru waliruhusiwa kuwa wanasheria binafsi,” alisema Lissu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles