30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AFANYIWA UPASUAJI WA TATU

*Hadi sasa zatumika milioni 100/-, dereva wake naye atibiwa Nairobi

 

ASHA BANI Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana amefanyiwa upasuaji mwingine chini ya uangalizi wa jopo la madaktari nchini Kenya anakotibiwa.

Lissu aliyejeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi Alhamisi iliyopita na watu wasiojulikana alipokuwa akitokea bungeni Dodoma, alifanyiwa upasuaji wa kwanza nchini humo Ijumaa iliyopita kuondoa risasi zilizomwingia mwilini.

Hii inakuwa mara ya tatu kufanyiwa upasuaji baada ya Alhamisi iliyopita kufanyiwa kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi na kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu wa madaktari (ICU).

Taarifa iliyotolewa na Chadema jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mbowe, ilieleza kuwa tangu alipofanyiwa upasuaji wa kwanza juzi na jana, tayari zimetumika zaidi ya Sh milioni 100.

“Kwa mara ya kwanza, Lissu aliongea juzi jioni na mkewe Alucia na baadaye na mimi, akisema ‘Mwenyekiti, I survived to tell the tale… Please keep up the fight (Mwenyekiti, nimeokoka ili niweze kuelezea mkasa huu… tafadhali endeleza mapambano).

“Lissu ameumizwa sana, tena sana, ni ukweli usiopingika kuwa miujiza ya Mungu ni mikubwa, hata kuweza kumwokoa katika bonde la mauti.

“Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalumu na yanayohitaji wataalamu wengi, vifaa tiba maalumu na gharama kubwa na kwamba hadi sasa zaidi ya Sh. milioni 100 zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa fedha si kitu ila thamani ya Lissu ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha hizo.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini.

Pamoja na hayo, Mbowe aliwashukuru Watanzania wote kwa namna wanavyoendelea kusaidia wajibu huo aliouita kuwa ni mkubwa kwa maombi na michango mbalimbali ya fedha, huku akiwataka wasichoke kuendelea kuchanga.

 

DEREVA WAKE APELEKWA KENYA

Mbowe alisema kutokana na ajali iliyotokea, wamalelazimika kumsafirisha pia dereva wa mbunge huyo, Simon Mohamed Bakari nchini Kenya kupatiwa huduma za kisaikolojia.

“Alishuhudia shambulio lile na aliokoka kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo wa mawazo, naye hatukuona busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa.

“Ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwaua wote, mheshimiwa Lissu na hata dereva wake,” alisema Mbowe.

Juzi Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilimtaka dereva huyo afike Ofisi ya Upelelezi Mkoa au Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Dar es Salaam kwa mahojiano.

Mbowe pia alielezea sababu za kulazimika kumsafirisha Nairobi, ni pamoja na maisha yake kuwa hatarini na kuhitajika matibabu maalumu ya haraka kutoka kwa madaktari bingwa wa kutosha sambamba na vifaa tiba visivyo na shaka ili kuokoa maisha yake.

“Busara ya kiusalama ilitulazimisha kuwatoa wahanga nje ya mipaka ya nchi hadi hapo usalama wao utakapohakikishwa,” alisema Mbowe.

 

GHARAMA ZA MATIBABU NJE

Mbowe pia alizungumzia kwa upande wa uongozi wa Bunge na Serikali ambao ulisisitiza Lissu apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili na kama sivyo hawatakuwa tayari kubeba gharama yeyote inayohusu matibabu yake.

“Upande wangu na wabunge wetu wa Ukawa ulisisitiza  Lissu apelekwe moja kwa moja Nairobi na kama Bunge na Serikali hawatakuwa tayari kubeba gharama za kuokoa maisha ya Lissu, basi sisi na Watanzania wenye mapenzi mema tutachangia gharama hizo za kuokoa maisha kimatibabu na kiusalama,” alisema.

Alisema wageni mbalimbali mashuhuri kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na hata jumuia za kimataifa wamekuwa wakimtembelea Lissu.

 

ULINZI HOSPITALI

Kuhusu ulinzi, alisema umeimarishwa katika eneo anakotibiwa na hairuhusiwi wageni kumwona hadi hapo madaktari wakiridhika kuwa hali yake ya kimatibabu inaruhusu.

 

MKAKATI MAHSUSI

Mbowe alisema kunahitajika mkakati mahsusi dhidi ya haki, demokrasia na usalama wa viongozi wa upinzani nchini.

Alisema Tanzania si salama tena baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kutokana na mauaji yanayoendelea kutokea.

Alikumbushia mauaji ya Alphonce Mawazo mkoani Geita, kukamatwa kwa wanaharakati kadhaa na kuteswa kwa kilichoitwa makosa ya kimtandao sambamba na kupotezwa kina Ben Saanane.

“Wakatekwa wasanii na kufanyiwa mateso makubwa, wabunge wanafungwa na kushtakiwa kila siku, mali, mashamba na hata biashara za viongozi wa upinzani zinateketezwa au kutaifishwa… sasa tunauawa kwa risasi mchana kweupe.

“Madhila wanayofanyiwa wapinzani na sasa hata wasio wapinzani bila kufuata misingi ya kikatiba, kisheria na hata ubinadamu tunapoteza utanzania wetu.

“Hapana! Inatosha. Tutamuenzi Baba wa Taifa aliyetuasa: “tukiwa waoga tutatawaliwa ma madikteta,” alisema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa upinzani bungeni, alisema kuwa wabunge na viongozi wa upinzani ndio wanaolengwa, hivyo aliwasihi kuchukua kila tahadhari na wanachama kuwa tayari kulinda na kupigania wajibu wao, usalama wa viongozi na chama kwa ujasiri.

“Tusipochukua hatua, kesho atadhurika mwingine na kwamba tamko na agizo rasmi la chama litafuata karibuni,” alisisitiza Mbowe.

Lissu alifikishwa Nairobi kwa ndege maalumu ya kukodi na kupokewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali Kuu ya Nairobi na kukimbizwa moja kwa moja hospitali.

 

ASKOFU GWAJIMA ATAHADHARISHA

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ametahadharisha kuwa kuwapo kwa vitendo vya umwagaji damu zisisokuwa na hatia kunaweza kusababisha matatizo na laana katika nchi.

Kwamba viongozi wa kiroho, lazima wafunge na kuomba ili kukemea vitendo hivyo kwani matatizo yatakapotokea hakuna atakayekuwa salama.

Aliyasema hayo jana wakati wa ibada maalumu ya kumwombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ambaye alipigwa risasi wiki iliyopita nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

“Leo (jana), nitafanya maombi maalumu ya kuiombea nchi na Lissu ili apone haraka na kichwa cha somo kinasema ‘damu isiyo na hatia’. Kumwaga damu isiyo na hatia ni kosa kubwa mbele za Mungu na hata katika jamii. Kwenye kitabu cha Biblia, neno hili limeandikwa mara 11.

“Damu ni uhai, hivyo ukimwaga damu ya mtu ni sawa na kumwaga uhai wake. Na anayemwaga damu ya mtu na ya kwake pia itamwagwa,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema hapa nchini, damu ilishamwagika  kuanzia mauaji ya polisi, viongozi na raia katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani na kuonya kama wahusika wa vitendo hivyo wasipotubu kwa wanayoyafanya, yatawarudia.

“Sisemi kwa ajili ya Lissu tu, bali nasema ili nchi ipone, mambo haya lazima yasemwe bila woga. Mauaji yote yanayoendelea, utekaji na mengine tunatakiwa kuyakemea bila kuangalia upande wowote,” alisema.

Askofu Gwajima alisema leo ataondoka kwenda Nairobi kumjulia hali mwanasiasa huyo.

 

KUBENEA

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), ambaye pia alikuwapo kanisani hapo, alisema Lissu alipigwa risasi 38 tofauti na taarifa za awali kwamba alipigwa 30.

“Lissu hakumiminiwa risasi 30 kama Spika alivyosema, bali 38, pale kwenye gari lake polisi waliokota maganda 38 ya risasi, kati ya hizo risasi mbili hazikuwa za SMG.

“Walikuwa na SMG yenye risasi 30 wakapiga zote, kisha walichukua bastola au silaha nyingine wakapiga risasi nane.

“Walidhani Lissu ameshusha kiti amelala nyuma, ndiyo maana walipiga katika mlango wa pili wa abiria risasi 22, kumbe alikuwa amelala mbele ya kiti cha dereva,” alisema Kubenea.

Alisema Lissu aliweza kuwatambua watu waliompiga risasi na kama vyombo vya ulinzi na usalama vitawakamata atawatambua sura zao.

“Jambo moja la faraja, Lissu aliweza kuwatambua waliompiga risasi, kama vyombo vya ulinzi na usalama vikiwakamata watu wale, Lissu atawatambua. Mmoja aliyeshuka na SMG kwenye gari alikuwa amevaa kapelo na miwani meusi na walimtambua yeye na dereva wake,” alisema Kubenea.

Alisema pia kabla ya tukio hilo, Lissu alianza kufuatiliwa tangu akiwa Tegeta, Dar es Salaam, lakini aliweza kuwakimbia watu waliokuwa wakimfuatilia hadi Dodoma.

 

MDOGO WA LISSU

Kwa upande wake, mdogo wa mbunge huyo, Vincent Lissu, alisema kaka yake alianza kufuatiliwa miezi miwili iliyopita, Kwamba kulikuwa na gari lililokuwa linamfuatilia kila alikokuwa.

“Miezi miwili iliyopita alikuwa akifuatwa kila alikokuwa, akiamka asubuhi anakuta gari limepaki, akiondoka linaondoka naye, alitoa taarifa anafuatiliwa,” alisema Vincent ambaye pia ni Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Ndugu yangu Lissu alipigwa risasi nyingi, miguuni, tumboni na alivuja damu nyingi.

“Kinachonishangaza tukio lilitokea katika eneo ambalo kuna nyumba za wakubwa, nyumba za mawaziri na kuna geti na kila nyumba ina mlinzi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles