26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AENDA RUMANDE NA FULANA YA UKUTA

*Anatetewa na mawakili 18 wakiongozwa na mtoto wa Karume

*Mawakili wa Serikali wapinga asipewe dhamana


Na Waandishi Wetu-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema),  amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi yenye kuleta chuki kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kidini, kikabila na kikanda.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mchana na kusomewa shtaka moja linalomkabili  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mshtakiwa huyo ambaye amelala Gereza la Segerea kwa kukosa dhamana hadi Julai 27, mwaka huu uamuzi wa dhamana utakapotolewa aliingia mahakamani akiwa kavalia fulana nyekundu yenye maandishi ya Ukuta.

“Mbona hamkuvaa kama mimi…..,” hayo yalikuwa maneno ya Lissu aliyokuwa akiyatoa huku akicheka kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wamejaa mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili wanne akiwamo Paul Kadushi, Mutalemwa Kishenyi na Simon Wankyo wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili 18 wakiwamo Fatma Karume na Pete Kibatala.

Kishenyi akisoma hati ya mashtaka alidai mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha ya uchochezi Julai 17, mwaka huu maeneo ya Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni.

“Mheshimiwa hakimu mshtakiwa anadaiwa kusema kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.

“Anadaiwa kusema vibali vya kazi vinatolewa kwa wamishionari wa kikatoliki tu huku madhehebu mengine yakiachwa kupanga foleni uhamiaji, viongozi wakuu wa Serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familia , kabila na ukanda…….acheni woga pazeni sauti.

“Anadaiwa kusema kila mmoja ……tukawaambie wale ambao bado wanampa msaada wa pesa Magufuli na Serikali yake kama tulivyowaambia wakati wa Serilkali ya Makaburu.

“Anadaiwa kusema hii Serikali isusiwe na Jumuiya ya Kimataifa , isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi…..yeye ni dikteta uchwara,” alidai Kishenyi kwamba maneno hayo alitamka Lissu na kwamba yalikuwa na lengo la kuleta chuki.

Alipotakiwa kujibu Lissu kama kweli ama si kweli alijibu ifuatavyo:

“Mheshimiwa hakimu haijawahi kuwa kosa la kijinai kwa hiyo sio kweli,”alidai Lissu.

Hakimu Mashauri alisema mahakama imeandika kwamba mshtakiwa kakana shtaka linalomkabili.

Wakili Wankyo alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika lakini wana hoja kadhaa za kuwasilisha mahakamani.

Alidai upande wa Jamhuri wanaomba mshtakiwa asipewe dhamana kwa sababu ana kesi nne mahakamani hapo zenye viashiria vya uchochezi.

Wankyo alidai kesi hizo za uchochezi amekuwa akitenda makosa baada ya kuachiwa kwa dhamana, chuki ambayo imetajwa mahakamani inagusa matabaka mbalimbali, hata kwa usalama wa nchi hivyo jambo hilo si la kufumbiwa macho.

“Kutokana na kujirudia kwa makosa ya kuleta chuki kwa jamii ya Watanzania ndio maana tunaomba mshtakiwa asipewe dhamana, haya matamshi yaliyosomwa mahakamani si ya kawaida, yanasababisha chuki baina ya Watanzania na madhara yake si madogo kama yataachwa na kunyamaziwa,”alidai na kuongeza kwamba asipewe dhamana kwa usalama wake pia.

Akijibu hoja hiyo wakili wa upande wa utetezi,  Fatma Karume alidai dhamana ni haki ya mshtakiwa na wala si haki ya Serikali wala mawakili wa Serikali.

“Napenda kuwakumbusha mawakili kwamba Lissu hapa hajahukumiwa, kwa maneno yao wenyewe mpaka sasa wanasema upelelezi haujakamilika, upelelezi haujakamilika halafu wanataka wewe utumie mamlaka yako kumuweka ndani.

“Wanataka mahakama imfunge Lissu, tukumbuke Mheshimiwa Lissu ni mpinzani na CCM ndio inawakilishwa, wanataka imfunge kwa sababu tu wameamua wao kuna meneno kasema ya uchochezi, kesi zote zilizopo hapa zimeletwa baada ya mwaka 2015 baada ya kuingia madarakani Magufuli.

“Ukitazama kesi nne hadi sasa hakuna hata moja waliyoikamilisha…wanasema tu kazi hawafanyi, wameshindwa hata moja na zote sababu Lissu kapaza sauti.

“Kila akipaza sauti wanaleta kesi kuimaliza wanashindwa, wanasema wanazuia dhamana eti kwa usalama wa mheshimiwa Lissu pia, hakuna anayetaka kumdhuru Lissu, Serikali ndio inataka kumdhuru sababu wamemshtaki mara sita.

“Wao ndio wanataka kumdhuru, hakuna mwananchi anayetaka kumdhuru… sisi hatutaki kumdhuru ila ni wao, Mheshimiwa Lissu ana haki ya kusema sio kuletwa hapa, wanasema analeta chuki za kidini…Lissu ni mkatoliki si Mwislamu.

“Kuna mambo kayaona hayaendi ndio kapaza sauti, sasa wanataka wamwweke ndani  kwa ridhaa yako mheshimiwa ili sauti yake isisikike.

“Kusema anyimwe dhamana kwa usalama wake…hiki ni kiini macho, wanajifanya wanampenda sana Lissu..eti akiwa nje ataharibikiwa,” alidai Karume na kuiomba mahakama impe dhamana mteja wake.

Akiongezea hoja Wakili Peter Kibatala alidai kama walikuwa na hoja ya kupinga dhamana walitakiwa kuwasilisha hati ya kiapo yenye hoja zote.

Alidai Lissu ni mbunge hivyo Serikali inatakiwa kuhakikisha anakuwa salama na Jeshi la Polisi ndio lenye jukumu la kumlinda.

Baada ya kuwasilisha hoja hizo Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 27,  mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa dhamana, mshtakiwa alipelekwa Gereza la Segerea hadi tarehe iliyopangwa.

Hali ya Polisi

Awali, kabla ya kufikishwa mahakamani, Jeshi la polisi liliimarisha ulinzi katika eneo lote la Kituo Kikuu cha Polisi huku wakitoa tangazo la kuwataka wananchi wakiwamo wafuasi wa chadema kuondoka eneo hilo kwa madai kuwa, hawaruhusiwi kusimama wala kupita karibu na kituo hicho.

Tangazo hilo lilitolewa na askari polisi aliyekuwa getini ambapo aliwataka wananchi wakiwamo waandishi wa habari kuondoka katika eneo hilo kwa madai kuwa, hawaruhusiwi kuingia ndani wala waandishi kuwepo katika eneo hilo.

“Mimi nafuata oda, nasema ondokeni katika eneo hili, hamruhusiwi kupita wala kusimama, kama kuna mtu atakayekiuka tutamkamata na kumweka ndani.

“Na nyinyi waandishi ondokeni katika eneo hili, hamtakiwi na wala hamruhusiwi kupiga picha katika eneo hilo, kama mnabisha tutawakamata,” alisema mmoja wa polisi kituoni hapo

Mara baada ya kutolewa kwa tangazo hilo, askari wengine walijitokeza na kuanza kuwakamata baadhi ya wafuasi wa Chadema ambao baadhi yao walionekana wamevalia sare za chama hicho na kuwaingiza ndani ya kituo.

Ilipofika saa 5:40, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alitoka ndani ya kituo hicho ambapo waandishi walimfuata na kutaka kujua kinachoendelea, ambapo  aliwajibu kuwa, muda si mrefu Lissu atapelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kusomewa mashtaka.

Ilipofika saa 5:45, Lissu alitolewa kwenye kituo hicho kupitia mlango wa nyuma na kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Habari hii imeandikwa na KULWA MZEE, PATRICIA KIMELEMETA NA SHABANI CHUWAKA

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Asante kwa Waandishi (Ripota) na jopo la wahariri wa MTANZANIA. Mnaitendea haki elimu na weledi wenu kwa kutuandikia articles zenye kufahamisha na kuelimisha kwa umakini na ufafanuzi wa kina.
    Si habari hii pekee ila 98% ya kazi zenu ninzuri.
    Nafsi za wasomaji wenu zinakuombeeni ili Mungu azidi kukulindeni na kuwaimarisha kila siku.
    Asanteni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles