33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lipumba, Sakaya wafukuzwa CUF

Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

Na Kulwa Karedia,

HATIMAYE Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limemvua uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu- Bara, Magadelena Sakaya.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata jana usiku kabla ya kwenda mtamboni, zinasema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika    Zanzibar.

Wengine waliovuliwa uanachama ni Mjumbe wa Baraza Kuu  na Katibu wa CUF Wilaya ya Handeni, Masoud Mhina, Mjumbe wa Baraza Kuu, Ashura Mustapha, Mjumbe wa Baraza Kuu na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenzi na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma.

“Kwa kauli moja Baraza Kuu limeazimia viongozi hawa wavuliwe uanachama wao kutokana na kuwa na mwenendo wa kutoridhisha ndani ya chama,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema kwa kauli moja baraza hilo liliazimia  na kumteua Julius Mtatiro  kuongoza Kamati ya Uongozi ambayo awali ilikuwa chini ya Twaha Taslima.

Habari zinasema kutokana na uamuzi huo, nafasi ya Kambaya, imechukuliwa na Mbarara Maharagande, wakati nafasi ya Sakaya imejazwa na Joran Bashange.

“Baraza Kuu limeagiza Kamati ya Utendaji   ambayo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kuwashughulikia wanachama wote walioonekana kuvuruga  Mkutano Mkuu uliofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita,” kilisema chanzo chetu.

Alipoulizwa, Mkurugenzi wa  Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Biman juu ya mabadiliko hayo, hakukubali wala kukataa.

“Tumekuwa na kikao cha Baraza Kuu, lakini ndugu yangu siwezi kusema lolote, kesho (leo) saa 5.00 tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari tutajulisha umma maazimio tuliokubaliana,”alisema Bimani.

Wiki iliyopita, Mkutano Mkuu Maalumu wa  chama hicho ulivunjika baada ya wafuasi wa Lipumba, kupinga uamuzi uliouita wa kura za kutengenezwa za kuridhia kuondoka kwa mwenyekiti wao aliyejiuzulu katika nafasi yake, Agosti  mwaka jana.

Hata hivyo, Julai mwaka huu, Profesa Lipumba aliutangazia umma kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na kutaka kurudi katika nafasi yake ya uenyekiti hali iliyolazimu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuingilia kati na kuwatawanya wafuasi hao.

Uamuzi huo uligeuka kaa la moto baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya wafuasi wa Profesa Lipumba na kundi linalomuunga mkono Maalim Seif.

Dalili za vurugu zilianza kuonekana baada ya wajumbe kumchagua Mtatiro, ambako baada ya kueleza namna atakavyoendesha kikao hicho, baadhi ya wajumbe walianza kumrushia vijembe na kudai kuwa ameteuliwa kwa mkakati maalumu na viongozi wa juu wa chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles