31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Lipumba ahukumiwe kupitia sanduku la kura

profesa-ibrahim-lipumba-640x559Na Tobias Nsungwe

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinapitia wakati mgumu. Kiini hasa cha tatizo ni mgogoro wa uongozi unaodhaniwa kugubikwa na baadhi ya wanachama waandamizi kuweka masilahi binafsi mbele kuliko chama.

CUF ndicho chama kikongwe cha upinzani chenye nguvu zaidi na mchango wake katika ukuzaji wa demokrasia nchini Tanzania ni wa hali ya juu.

Chama hiki kimepitia changamoto mbalimbali hasa katika kupambana na watani wao wa jadi, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini wanasema hatima ya CUF sasa inategemea mazungumzo na maridhiano baada ya kuvunjika kwa mkutano maalumu ulioitishwa kujaza pamoja na mambo mengine nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho. Sababu kubwa ya mkanganyiko ule ni kitendo cha uongozi wa muda wa chama hicho kumzuia Profesa Ibrahim Lipumba kugombea nafasi hiyo.

Kwa nini? Kwa sababu Profesa Lipumba aliomba kujiuzulu nafasi hiyo Agosti mwaka jana, huku akidai dhamira yake ilikuwa inamsuta kushiriki kumpitisha Edward Lowassa kugombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa).

Lowassa ambaye vyama vya upinzani vikiwamo Ukawa, vimekuwa vikimtuhumu kwa ufisadi kwa muda mrefu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana CUF ilipoungana na Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD kumpitisha Lowassa kugombea urais kupitia Chadema. Hili halikumfurahisha Profesa.

Bado wanachama wengi  wa CUF wanamtaka Profesa Lipumba arejee kukiongoza chama chao. Nadhani viongozi wa muda wa CUF walikosea kukata jina la Profesa Lipumba kugombea uenyekiti.

Ni kweli aliomba kujiuzulu nafasi hiyo. Lakini hiyo si sababu ya msingi ya kumzuia kurejea ulingoni. Kumbuka sababu zilizomfanya Lipumba aondoke hazipo tena.

Watanzania wote wanajua kwamba Lowassa aligombea na kushindwa urais mwaka jana. Kilichobaki sasa ni kwa vyama kujipanga upya.

Upepo unaonesha wazi kwamba salama ya CUF ni kumruhusu Lipumba agombee tena nafasi yake na jukumu la kumchagua au kumtosa waachiwe wanachama kupiga kura.

Ni vyema sauti za wanaomtaka Lipumba zikasikilizwa kwani kujiuzulu kwake mwaka jana hakumzuii kuomba tena nafasi ya uongozi hasa ukizingatia kuwa ana wafuasi wengi.

Changamoto kubwa waliyonayo viongozi wa muda wa chama hicho ni kuoanisha kati ya masilahi binafsi na maslahi mapana ya chama.

Kama kweli, kuna wanachama hawamtaki Lipumba, basi wafanye hivyo kupitia sanduku la kura, si vinginevyo.

Tusahau habari ya Profesa kuomba kujiuzulu mwaka jana. Hizo ni habari zilizochacha. Habari mpya ni kwamba anataka kurejea katika uongozi wa chama.

Profesa Lipumba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, yafaa wakae chini na kumaliza tofauti zao zilizoanza wakati wa kumpitisha mgombea urais kupitia Ukawa mwaka jana.

Kwanza waanze na kuondoa hisia za u-bara na u-visiwani zilizoanza kujitokeza miongoni mwa wanachama. Nasema Lipumba bado anafaa kuwa mwenyekiti wa CUF.

Profesa huyo amejitolea muda wake mrefu kukijenga chama hicho hadi baadhi ya vijana wasomi wakavutiwa kujiunga nacho.

Amekuwa mstari wa mbele kutetea demokrasia na mapambano dhidi ya ufisadi nchini. Amepambana na Serikali ya CCM mara kadhaa na kupigwa virungu na polisi.

Mchango wake kwa CUF si wa kubezwa. Tangu enzi ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, Profesa Lipumba amekuwa kama ‘nembo’ ya chama hicho.

Hivyo apewe nafasi nyingine. Uamuzi wanao wanachama wenyewe kwani ndiyo wenye chama chao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles