29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lipumba agoma kusimamishwa CUF

Profesa Ibrahim LipumbaNa Patricia Kimelemeta

-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kusimamishwa uanachama yeye na wenzake 11, kiongozi huyo ametua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kudai yeye bado ni mwenyekiti halali wa chama hicho.

Profesa Lipumba alitinga katika ofisi hizo jana saa 3  asubuhi akiwa na barua ya kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi na kudai kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho, kwani uamuzi wa kumsimamisha haukufuata katiba ya chama hicho.

Alisema vikao vyote vilivyofanyika kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa kumsimamisha ni batili kwa sababu chama hicho kinaongozwa na katiba na kanuni na si vinginevyo.

Kutokana na madai hayo alimwomba Msajili wa Vyama,  Jaji Francis Mutungi,  kuingilia kati mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kwa sababu unaweza kuwagawa wanachama.

“Nimekuja hapa kupinga kile kinachodaiwa kuwa mimi nimevuliwa uanachama jambo ambalo linakwenda kinyume cha katiba ya chama chetu. Hivyo mimi bado ni mwenyekiti halali kwani hata uamuzi wa kuniondoa haukuzingatia katiba ya chama,” alisema Profesa Lipumba.

Ilipofika saa 4 asubuhi Baraza la Wazee wa  chama hicho(JUWACUF), wakiongozwa na mwenyekiti wake, Abdul Magomba,  waliwasilisha barua yao ya malalamiko kwa msajili huyo ili aweze kuingilia kati mgogoro uliosababisha Profesa Lipumba kusimamishwa uanachama yeye na wenzake 11.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha barua hiyo, Magomba alisema kilichofanyika ndani ya chama hicho ni ubabe ambao unapaswa kupingwa na kila mpenda haki.

“CUF inasimamia misingi ya haki sawa kwa wote, kwanini tunafanya uamuzi kama huu bila ya kufuata misingi hiyo, hatukubali kabisa na tunaamini kuwa, Profesa Lipumba ni mwenyekiti halali wa chama chetu kwa sababu vikao vya kumng’oa ni batili na wala havijafuata katiba ya chama,”alisema Magomba.

Kutokana na malalamiko hayo Jaji Mutungi, alitoa siku tano kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,  kujibu malalamiko ya kuwavua uongozi viongozi hao pamoja na kuwasimamisha uanachama, ili kuoana kama walifuata taratibu za kisheria au laa.

Alisema vyama vya siasa vinapaswa kusimamia misingi ya haki na utawala bora, na si kuamua kulingana na mtu anavyotaka, jambo ambalo linaweza kuwagawa wanachama.

Alisema migogoro inayojitokeza ndani ya chama inapaswa kutatuliwa kwa kufuata katiba ya chama na kanuni zake na si kutumia mamlaka binafsi kwa ajili ya kuwavuruga wengine.

“Nimetoa siku tano kwa Maalim Seif na wenzake kujibu barua yetu ya kutaka kutueleza utaratibu uliotumika kwa kuwavua uongozi na kuwasimamisha uanachama Profesa Lipumba na wenzake. Hofu yangu isiwe matatizo binafsi yakaingizwa ndani ya chama na kuleta migongano, hilo hatuwezi kulifumbia macho,” alisema Jaji Mutungi.

Aliongeza, ili chama kiwe na sifa, kinapaswa kuwa na wanachama bara na visiwani chama ambacho kitakosa sifa hiyo kwa mujibu wa sheria ya vyama vingi kitafutwa huku akionya hali hiyo ndani ya CUF inaweza kuwafikisha huko.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui, alisema kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kimewasimamisha uanachama wanachama 11 ambao ni pamoja na Prof Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya,   Ashura Mustafa, Omar Masoud, Thomas Malima, Kapasha Kapasha, Maftaha Nachumu, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Alisema, uamuzi huo umekuja kwa kuzingatia katiba ya chama hicho Ibara ya 83 (5)(c), ambapo wajumbe hao wamesimamishwa hadi watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles