29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Lipuli yaifuata Azam FC fainali

MWANDISHI WETU-IRINGA

TIMU ya Lipuli FC imetinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), baada ya kuifunga Yanga mabao 2-0, katika mchezo wa nusu fainali ya pili iliyochezwa kwenye Uwanja wa Samora, mkonai Iringa jana.

Lipuli FC sasa inaifuata Azam FC kucheza fainali ya michuano hiyo, ambayo iliifunga KMC bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza.

Fainali hiyo imepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa, mkoani Lindi.

Katika mchezo huo ulioanza kwa mashambulizi huku Lipuli wakikosa nafasi nyingi za wazi, ambapo katika dakika ya 27, Paul Nonga, aliipatia timu yake bao la kwanza, baada ya kupiga shuti lililomponyoka kipa wa Yanga, Klaus Kindoki na kuzama wavuni moja kwa moja.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwaamsha Yanga na kuliandama lango la Lipuli mara kwa mara, huku ikikosa nafasi za wazi.

Lipuli waliokuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa, waliongeza mashambulizi langoni mwa Yanga na katika dakika ya 38, Dalueshi Saliboko, aliipatia timu yake bao la pili, kwa kumalizia mpira wa Kindoki alioutema baada ya Rajab Ally kupiga shuti lililotua mikononi mwa kipa na mabeki wa Yanga kufanya makosa kama ya awali kuzembea kuokoa mpira.

Katika dakika ya 40, Ibrahim Ajibu, alipiga kona ambayo ilishindwa kuzaa matunda huku katika dakika ya 44, Lipuli wakikosa bao baada ya Haruna Shamte, kupiga shuti lililookolewa na mabeki wa Yanga.

Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Lipuli inayofundishwa na kocha Selemani Matola, ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko katika dakika ya 46, kwa kumtoa Mohamed Banka na nafasi yake kuchukuliwa na Amissi Tambwe.

Katika dakika ya 56, Jimmy Mwaisondola wa Lipuli alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea faulo  Feisal Salum, wakati katika dakika ya 66, Abdalah Haji, alionyeshwa kadi ya njano, baada ya kumchezea faulo Nonga wa Lipuli.

Yanga walifanya tena mabadiliko katika dakika ya 70, kwa kumtoa Haji Mwinyi na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Yondani.

Lipuli nao walifanya mabadiliko katika dakika ya 80, kwa kumtoa Zawadi Mauya na kuingia Steve Mganga, wakati huo huo, Miraji Athuman, alikwenda benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Nolfant Lufunga.

Yanga waliongeza juhudi ya kulishambulia lango la Lipuli ambapo katika dakika ya 86, Feisal Salum, alipiga faulo ambayo iliokolewa na mabeki wa Lipuli.

Yanga hawakuishia hapo, waliendelea kulishambulia lango la Lipuli, katika dakika ya 89, Papy Tshishimbi, alipiga shuti lililotua mikononi mwa kipa wa Lipuli, Mohamed Yussuf.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, Lipuli ilitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 na hivyo kwa mara ya kwanza, timu hiyo kutinga fainali ya michuano hiyo.

Bingwa wa michuano hiyo kati ya Azam FC na Lipuli, ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles