30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

LIPULI FC MNAELEWA SOKA NI BIASHARA ?

Na ZAINAB IDDY


WAKATI timu ya Singida United, ikiwa kwenye harakati zake za kukiimarisha kikosi chake  kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Lipuli FC wao  hadi sasa hawajawa na uhakika wa vipi wataiendesha timu hiyo.

Lipuli ni moja kati ya timu tatu zilizopanda daraja na kupata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania msimu ujao, nyingine ni Mji Njombe ya Njombe.

Timu hiyo ya mkoani Iringa, ndio iliyokuwa ya kwanza kupanda daraja ikitoka kundi A, baada ya kukutana na msoto wa misimu mitatu wakiwa Daraja la Kwanza, tangu iliponunua nafasi ya iliyokuwa Polisi Iringa mwaka 2013 Daraja la Kwanza.

Kupanda kwa timu hiyo kulionekana ni wazi kunaweza kurejesha heshima ya mkoa wa Iringa katika soka, heshima iliyotoweka tangu mwaka 2001 takribani miaka 16 tangu ‘Wanapaluhengo’ kushuka daraja.

Wadau wengi wa soka wa Iringa, walikuwa na imani kuwa timu yao itakuja kuwatoa kimasomaso, lakini jambo la ajabu ikiwa ni miezi miwili tangu wapande daraja, badala ya kufanya vitu vya kuijenga wamejikuta wakiingia kwenye mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe.

Mgogoro huo unawahusisha viongozi wa Lipuli waliokuwa madarakani pamoja na wanachama, umetokana na kurejea kwenye uongozi kwa mwenyekiti wake, Abuu Changawa ‘Majeki’ aliyekuwa amesimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Kufuatia mgogoro huo Chama cha Soka mkoa wa Iringa (IRFA) kupitia kwa mwenyekiti wake mkuu, Cyprian Kuyava, waliamua kuichukua timu kwa lengo la kuisaidia kujiandaa na msimu ujao wa ligi, ikiwemo kuweka kambi pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wapya hadi pale maelewano yatakapopatikana.

Hili ni jambo baya kwa timu iliyopanda daraja, baada ya muda mrefu kwani kipindi cha migogoro ndicho wanachotakiwa kujenga kikosi cha ushindani kwa lengo la kuleta changamoto.

Ni vizuri kwa uongozi wa Lipuli kufahamu soka ni biashara na huu ni muda wa kutafuta uwekezaji kwenye timu, kabla ya kuanza kwa ligi msimu wa 2017/18 badala ya kuendekeza migogoro isiyo na tija ndani ya kikosi.

Suala la nani ameipandisha timu si la muhimu kwa hivi sasa, badala yake wanatakiwa kupita huku na uko kutafuta wadhamini ndani na nje ya mkoa, watakaowawezesha kupata fedha za usajili, kambi pamoja na mahitaji ya uendeshaji.

Ni ukweli usiofichika soka ni biashara  na hili limejidhihirishwa na Singida United, waliotambua umuhimu na majukumu yao kwa kufanya mambo yatakayokuwa na tija katika kikosi cha msimu ujao.

Si kitu cha kupendeza hata kidogo kuona msimu ujao Lipuli inakuwa ya kwanza kurejea ilipotoka, huku ikiacha simanzi kwa wakazi wa Iringa, ambao kwa sasa wanafuraha kubwa kuona ligi kuu ikichezwa katika aridhi yao.

Kiroho safi inahakika kama viongozi wa Lipuli wakiamua kuisimamia timu, wanaweza na hili litawezekana tu kama wakitambua soka ni biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles