NYOTA wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi, amemgaragaza mpinzani wake, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid katika tuzo za Globe Soccer, ambapo Messi amefanikiwa kuchukua mchezaji bora wa mwaka.
Tuzo hizo ambazo zimetolewa juzi mjini Dubai, Messi aliibuka kinara wa tuzo hizo huku Ronaldo akishika nafasi ya pili.
Wakati huo huo, klabu ya Barcelona ilifanikiwa kuchukua klabu bora ya mwaka kutokana na kukusanya mataji mengi msimu uliopita, huku Josep Bartomeu akichukua rais bora wa klabu hiyo.
Frank Lampard na Andrea Pirlo, wameibuka wachezaji bora ambao wamecheza katika kiwango chao vizuri, huku Jorge Mendes akichukua tuzo ya wakala bora na Marc Wilmonts akiwa kocha bora ambaye anaifundisha timu ya Taifa ya Ubelgiji.
Katika tuzo hizo msimu uliopita, Ronaldo alifanikiwa kuchukua huku Messi akishika nafasi ya pili, wakati mwaka huu Messi ametwaa tuzo hiyo na Ronaldo akishika nafasi ya pili.
“Nimekuwa na furaha kubwa kuchukua tuzo hii, lakini naweza kusema kuwa timu ndiyo imenifanya niwe hapa, huu umekuwa ni mwaka wenye mafanikio ndani ya klabu,” alisema Messi.
Klabu ya Barcelona imekuwa na mafanikio makubwa msimu huu ambapo imechukua mataji matano ambayo ni Ligi Kuu nchini Hispania, Copa del Rey, Ligi ya Mabingwa, European Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia.