Na Samweli Mwanga, Maswa
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewataka wananchi waishio katika vijiji vya Isulilo na Ngongwa wilayani humo kutunza miundombinu ya maji na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali pale wanapowabaini wananchi wachache wanaohujumu miundombinu hiyo.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu huyo wa wilaya wakati akiongea na viongozi wa vijiji hivyo katika kikao kilichofanyika katika kijiji cha Isulilo mara baada ya bomba la kusambaza maji kwenye vijiji hivyo kupasuliwa na watu ambao hadi sasa hawajajulikana na kusababisha kuwepo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema alipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa vijiji hivyo kuwa Jumuiya ya watumia maji ya kijiji cha Isulilo kuwa wamesitisha utoaji wa huduma ya maji kutokana na bomba hilo kupasuliwa na watu ambao hadi sasa hawajafahamika na hivyo kusababisha wakazi wa vijiji hivyo kukosa maji na kusababisha adha kubwa kwa wakazi hao.
Amesema kupasua bomba ni kuhujumu uchumi na kuwaonya watu wote wanaofanya vitendo hivyo wakikamatwa watafikishwa katika vyombo vya sheria na hivyo kuuagiza Uongozi wa vijiji hivyo hivyo kulinda miundo mbinu hiyo kwa nguvu zote.
“Kuharibu miundo mbinu ya maji huu ni uhujumu uchumi na yeyote atakayekamatwa atafikishwa katika vyombo vya sheria kwani kupasua bomba hili ni sawa na kuhatarisha maisha ya watu kwani unawazuia wasipate maji safi na salama hivyo niuagize uongozi wa kijiji cba Zanzuii kulilinda bomba hilo na toeni taarifa kwa jeshi la polisi au kwa viongozi wa serikali mtakapobaini mtu au watu wanaofanyavitendo vya kupasua bomba hili,”amesema.
Amesema kuwa kuanzia sasa miundo mbinu hiyo ya maji ikihujumiwa ataanza kuwashughulikia viongozi wa vijiji kwani ndiyo watakuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Ngongwa, Juma Kafula alikiri miundo mbinu ya maji katika mradi wa maji wa Isulilo kuharibiwa kwa kiasi kikubwa kwenye eneo lake la kijiji na kusisisitiza kuwa kwa sasa watatoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwa walinzi wa miundo mbinu hiyo.
Amesema wamejipanga kuhakikisha wanalilinda bomba hilo kwa kutumia askari wa jadi maarufu kwa jina la Singusungu na wote watakaobainika kuhujumu miundo mbinu hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.