WANAMUZIKI nyota wa Bongo fleva nchini, Estelina Peter Sanga ‘Linah Sanga’ na Feza Kessy, leo watapanda jukwaa moja na nyota kibao wa Nigeria, katika tamasha kubwa la mwaka la muziki lijulikanalo kwa jina la Soundcity Urban Festival, litakalofanyika Lagos, Nigeria.
Tamasha hilo pia litawashirikisha wasanii wakali nchini humo kama vile Davido, Kiss Daniel, Iyanya na Olamide, huku wengine wakiwa Victoria Kimani, Runtown, Sound Sultan, Lil Kesh, Ycee, Sean Tizzle na Phyno.
Wanamuziki hao waliondoka nchini Jumatano usiku chini ya Doreen Noni, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni mpya ya kusimamia wanamuziki nchini, Panamusiq Limited, ambaye alisema kampuni yao ndiyo iliyowawezesha wanamuziki hao kuweka historia kwa kuwa wanamuziki wa kwanza nchini kushiriki katika tamasha.
“Tumejiandaa kufanya kweli katika tamasha hilo, Linah na Feza walikuwa katika mazoezi makali ya kuimba, kucheza hasa kwa kutawala jukwaa, lengo ni kuacha historia katika tamasha hilo,” alisema Doreen.