MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya inatarajia kutimua vumbi leo katika viwanja mbalimbali, huku mchezo ambao unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wa soka duniani ukiwa kati ya Manchester City ambao watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Etihad, kuwakaribisha Juventus ya nchini Italia.
Mbali na mchezo huo, michezo mingine ambayo itapigwa usiku wa leo ni pamoja na Galatasaray ambao watapambana na Atletico Madrid, wakati PSG wakicheza na Malmo jijini Paris, huku Wolsfburg ikipambana na CSKA Moscow, Benfica wakicheza na Astana na Sevilla ikipambana na Monchengladbach.
Mchezo wa Manchester City dhidi ya Juventus unaonekana kuwa wa kihistoria kwa kuwa timu hizo zimekuwa sikitunishiana misuli mara nyingi zinapokutana.
Septemba 30 mwaka 2010 timu hizi zilikutana kwenye uwanja huo huo na dakika 90 zilimalizika kwa sare ya bao 1-1, hata hivyo, katika mchezo wa marudiano ambao ulipigwa Desemba 12 mwaka huo kwenye Uwanja wa Juventus, bado zilitoka sare ya 1-1.
Mbali ya kuangalia rekodi hizo, pia Manchester City wanapewa nafasi kubwa ya kushinda katika mchezo huo kutokana na ubora wa kikosi chake, ambacho kinafanya vizuri kwa sasa katika michuano ya Ligi Kuu nchini England, kikiwa na alama 15 baada ya kucheza michezo mitano na kufanya waongoze Ligi.
Japokuwa Manchester City wanaonekana kukamilika, lakini katika mchezo wa leo watamkosa mshambuliaji wake hatari, Sergio Aguero, kutokana na kupata majeraha ya goti katika mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Crystal Palace.
Kwa upande wa Juventus, bado inaonekana kuwa dhaifu baada ya nyota wake watatu kuondoka na kujiunga na klabu nyingine kutokana na kumaliza mikataba yao.