LIGI KUU BARA: Yanga, Simba mzigoni

ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba leo inashuka uwanjani kuvaana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mjini Tanga, wakati Yanga itakuwa ikiumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Michezo hiyo itachezwa mchana kupisha michezo ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa vijana inayoendelea nchini katika viwanja vya Taifa na Azam Complex vya Dar es Salaam.  

Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ikitafuta pointi tatu muhimu mbele ya Wagosi ili kufuta ndoto za Yanga kushinda taji la Ligi Kuu msimu huu, licha ya kuongoza ligi hiyo kwa sasa.

Simba mara ya mwisho kukutana na Coastal ilikuwa msimu wa 2015/16, kabla ya Coastal Union kushuka daraja msimu huo.

Machi 19 mwaka 2016 ilikuwa mara ya mwisho Simba kuifunga Coastal Union mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, baada ya mzunguko wa kwanza kushinda bao 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Simba itaivaa Coastal Union ikiwa na hasira ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe hatua ya robo fainali kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1.

Simba ipo nafasi ya tatu baada ya kushuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 57, wakishinda michezo 18, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.

Coastal Union wapo nafasi ya nane baada ya kufikisha pointi 41, huku wakiwa wameshinda michezo tisa, sare 14 na kupoteza michezo tisa.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alisema amejipanga vema kuchukua pointi tatu katika mchezo huo, baada ya kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza  katika michezo iliyopita.

“Kila mechi ina programu yake, nimekuwa nikiwafundisha vijana wangu kulingana na makosa yaliyojitokeza nyuma,” alisema Aussems.

Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema: “Tupo katika maandalizi ya mwisho na vijana wangu, sina hofu, lakini zaidi hakuna mchezaji majeruhi, jambo ambalo linaweza kuwa na faida katika mchezo huu ambao naamini utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu.”

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema licha ya kuwakosa walinzi wawili, Kelvin Yondan na Feisal Salum ‘Fei Toto’, bado kikosi chake kinaweza kuhimili vishindo vya Mtibwa Sugar na kuhakikisha wanapata pointi tatu.

“Ni mchezo mgumu, lakini vijana wangu wapo vizuri kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Zahera.

Yondan atakosekana baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu wiki iliyopita kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera, ambako Yanga ilishinda mabao 3-2.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, imeshuka dimbani mara 32 na kujikusanyia pointi 74, imeshinda michezo 23, sare tano na kupoteza michezo mitatu.

Mtibwa Sugar ipo nafasi ya tano baada ya kushuka dimbani mara 31 na kujikusanyia pointi 45, wakishinda michezo 13, sare sita na kupoteza michezo 12.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here