29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

LHRC CHATOA USHAURI NEC

LEONARD MANG’OHA Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuzingatia misingi ya demokrasia na kutenda haki katika chaguzi mbalimbali.

Aidha, kimetoa rai kwa mamlaka za Serikali na wananchi kuheshimu misingi ya kikatiba na kisheria katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema kituo chake kimeshtushwa na taarifa za kuondolewa kwa wagombea 30 wa vyama vya upinzani katika mchakato wa awali wa uchaguzi mdogo wa madiwani na wabunge unaotarajiwa kufanyika Julai 12, mwaka huu.

Alisema kuna hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi katika kata 30 ambazo wananchi wake wamepokwa haki yao ya ushiriki katika uchaguzi huo.

“Wananchi wamepokwa haki yao ya ushiriki katika uchaguzi mdogo baada ya baadhi ya , hususani wa vyama vya upinzani kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa sababu mbalimbali zikiwemo tuhuma za kutokidhi vigezo vya kiufundi na kisheria kama kutojua kusoma na kuandika pamoja na vigezo vya kutokua raia,” alisema Henga.

Alisema kuwa kituo hicho kimefuatilia kwa karibu taratibu za awali katika uchaguzi huo wa madiwani uliopangwa kufanyika katika kata 77, sambamba na ubunge katika Jimbo la Buyungu, Mkoani Kigoma na kushuhudia matukio mbalimbali yanayoathiri haki za binadamu hususani mchakato wa kidemokrasia unaotaka wananchi kushiriki katika uchaguzi ulio huru na haki.

“Kituo kimebaini ukiukwaji wa ibara ya 25 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966, pamoja na ibara ya tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayoweka haki ya ushiriki wa shughuli za kisiasa kwa kuainisha haki ya kupiga kura” alisema.

Kituo hicho kimekemea tukio la kuchomwa moto nyumba ya mgombea udiwani wa Kata ya Tunduma mkoani Songwe, ambaye alikihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kitendo hicho ni kunyume cha sheria kwani kila mtu ana haki ya kujiunga na chama chochote bila kujali hisia za watu wengine na kwamba kitendo cha kutishia maisha ya mgombea huyo ni tishio kwa haki ya msingi ya kuishi.

Wakati huohuo, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), limeitaka Serikali kufanya mabadiliko madogo ya katiba na sheria kabla ya kuingia katika uchaguzi wa mwaka 2020 ili kufanya uchaguzi wenye amani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda alisema mabadiliko hayo yanagusa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi.

Alisema wameamua kuja na hoja ya mabadiliko hayo baada ya Rais Dk. John Magufuli kutamka kuwa katiba mpya si kipaumbele cha Serikali ya sasa.

“Mamlaka ya uteuzi wa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi yasiwe mikononi mwa mtu mmoja ambaye mara nyingi huwa ni mgombea ama chama chake kinagombea,” alisema Mwakagenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,335FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles