MGOMBEA ubunge wa Chadema, Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, jana amekamatwa na polisi akidaiwa kuzidisha muda katika mkutano wake wa kampeni na kufanya maandamano bila kibali.
Tukio hilo lilitokea baada ya mkutano huo wa kampeni katika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro ambapo Lema alihutubia hadi saa 12:06 badala ya saa 12:00, na aliposhuka jukwaani na kuanza kuondoka, wafuasi wake walianza kumfuata na kusukuma gari lake.
Baada ya hatua chache kutoka uwanjani hapo, polisi walianza kuwatawanya wafuasi hao na baadaye kumkamata Lema na kwenda naye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha.
Awali katika hotuba yake, Lema alimshukia mpinzani wake, Philemon Mollel wa CCM, kwamba anafanya kampeni zake kwa kutumia mbinu chafu za ukabila na udini.
Katika uzinduzi wake wa kampeni Agosti 23, mwaka huu, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alizidisha dakika 36, lakini hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa.