23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Lema, Gambo waanza kutambiana ubunge

NA GRACE MACHA-ARUSHA

KINYANG’ANYIRO cha ubunge Jimbo la Arusha Mjini kinaelekea kuwa na ushindani mkali baina ya wagombea wawili, Godbless Lema (Chadema) na Mrisho Gambo (CCM), baada ya kila mmoja kumtambia mwenzake kuwa ataibuka na ushindi wa kishindo.

Wakati Lema akitumia kauli ya Rais John Magufuli wakati akitengua uteuzi wa Gambo nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kama fimbo ya kumshughulikia kwa wapigakura, Gambo amedai Lema amemweleza  aligombea kupima upepo na kwa hali ilivyo amebaini wananchi wamemchoka.

Wagombea hao walitoa tambo hizo  juzi jioni wakati walipokutana  kwenye ofisi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi Arusha Mjini, walipokuwa wakifuatilia endapo wameteuliwa kugombea.

Baada ya kutangazwa kuteuliwa kila mmoja kwa nyakati tofauti alizungumza na waandishi wa habari.

Wa kwanza kufika eneo hilo, alikuwa Gambo ambaye alikuwa na msafara mrefu wa magari, bodaboda na bajaji huku akiwa ameambatana na wafuasi na viongozi wa CCM ambao tangu asubuhi walikuwa wakipita mitaa mbalimbali ya kata za Jiji la Arusha.

Lema alifika akiwa ameambatana na mke wake, Neema na viongozi wa chama chake ambao kwa idadi yao hawazidi 10.

Baada ya kufika, Lema alisalimiana na Gambo kisha wakapiga picha ndipo kila mmoja alipoanza kumtambia mwenzake ataibuka mshindi.

LEMA

Lema aliwaeleza waandishi wa habari kuwa atamshinda Gambo kwa kura nyingi zaidi ya zile alizowahi kuwashinda wagombea wengine wa CCM.

Alimshinda Batilda Buriani kwa zaidi ya kura 18,000 mwaka 2010 na Philemon Mollel kwa kura zaidi ya 40,000 mwaka 2015.

“Kwanza sijaona nyomi na mimi nilikuwa katikati ya huo msafara na gari ndogo tu IST. Nimeona magari mengi yakiwekewa mafuta hapa Oryx (kituo cha mafuta) na pikipiki na vijana wetu wengi wa Chadema walienda kuweka mafuta, tuliwaruhusu kwa sababu walikuwa wanawekewa mafuta bure.

“Watu wengi wamebebwa kwenye kata mbalimbali, mwanzo nilifikiri ni msiba, kilichonifanya nijue si msiba ni bendera za CCM,” alisema Lema.

Alisema kwa mara ya kwanza tangu aanze kugombea ubunge jimbo hilo mwaka 2005, msafara wa CCM uliowahi kuwa na watu wengi kidogo ni wa Dk. Batilda.

“Msafara wa Gambo ulikuwa na vyombo vingi vya moto, amebeba watu kutoka maeneo tofauti, nilikuwa nafuatilia huku mjini nione atapokelewaje, hakukuwa na shamrashamra, nafikiri majibu amepata,” alisema Lema na kuongeza.

“Nilimwacha Dk. Batilda kwa kura 18,900 nikamuacha Monaban kwa kura 40,000 mpango wangu kwa huyu ni kumuachia kura 21,000 au 18,000. Nina mkakati wa kumpiga kwa asilimia 90.

“Kuna watu wanaosema Gambo alishinda kwa asilimia kubwa ndani ya CCM. Hawajui data, Dk. Burian alishinda kwa wanachama wa CCM kwa zaidi ya kura 10,000 akishindana na Felix Mrema, nilimshinda.

“Gambo ni mwepesi, hana watu. Watumishi wa Serikali hawamtaki, wananchi waliona maringo yake, bodaboda hawamtaki wanafahamu alivyofanya mambo ya ajabuajabu, hivyo ni mgombea ambaye namsubiri.”

GAMBO 

Gambo alidai alitumia muda mwingi kuongea na Lema wakati wakisubiri muda wa uteuzi ufike ambapo alimweleza aligombea kupima upepo na ameshaona wananchi wamemchoka.

“Lema ameniambia amegombea ili kupima upepo, na kwa namna ambavyo ameshapima upepo ameona watu wa Arusha wameshamchoka. Nikaona kama mgombea mwenyewe ameshajihakikishia amechokwa, kwa nini nisijiamini kwamba nina nafasi nzuri ya kushinda,” alisema Gambo.

Alisema ameangalia orodha ya watu 24 walioteuliwa kugombea ubunge jimbo hilo, hajaona atakayeweza kumpa upinzani.

“Naona pale mbunge nipo mmoja na wasindikizaji 13. Niwaahidi ya kwamba ninakwenda kifua mbele kufanya kampeni za kistaarabu, nitakwenda kifua mbele nikijivunia kazi zilizofanywa na Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli,” alisema Gambo.

WAGOMBEA 14

Akitangaza majina ya wagombea, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, Dk. John Pima alisema wagombea wa vyama 14 wameteuliwa kugombea baada ya kukidhi vigezo.

Alisema wagombea wa vyama viwili vya ADC na UMD walishindwa kutimiza masharti kwa kutorejesha fomu zao.

Aliwataja walioteuliwa na vyama vyao kwenye mabano ni Husna Kundi (AAFP), Shayo John (ACT Wazalendo), Zuberi Halisi (Ada Tadea), Mathayo Membi (CCK), Mrisho Gambo (CCM), Godbless Lema (Chadema), Magdalena Shangay (Cuf), Elisante Mjema (Demokrasia Makini).

Wengine ni Elizabeth Sembuche (DP), Hefsiba Kiwelu (NCCR Mageuzi), Mkama Japalya (NRA), Simon Bayo (SAU), Alfred Mollel (UDP) na Happy Sumari (UPDP).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,642FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles