22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Leicester City wanaweza kutetea taji kama watafanya haya

king power mirror

MARTIN MAZUGWA NA MITANDAO,

LIGI Kuu nchini England imeanza kwa kasi kubwa na ushindani wa hali ya juu kwa ajili ya kuwania taji ambalo lilichukuliwa na klabu ya Leicester City msimu uliopita.

Ujio wa makocha wapya katika ligi hiyo unaonekana utazidi kuleta ushindani wa hali ya juu kwa msimu huu, hivyo hali ambayo ilitokea msimu uliopita inawezekana isitokee tena msimu huu.

Makocha ambao wanaangaliwa sana msimu huu kuleta changamoto kubwa kwa makocha wa msimu uliopita ni pamoja na Jose Mourinho wa Manchester United, Pep Guardiola wa Manchester City, Antonio Conte wa Chelsea, Jurgen Klopp wa Liverpool na wengine.

Makocha hao wanaweza kuleta changamoto kubwa kwa kocha ambaye alitwaa ubingwa wa msimu uliopita, Claudio Ranieri wa Leicester City.

Mabingwa hao licha ya kushinda taji la ligi pia walitoa mchezaji bora, Riyad Mahrez na kocha bora wa msimu wa 2015-16.

SPOTIKIKI leo hii imekufanyia uchambuzi kwa klabu ya Leicester ambao ni mabingwa watetezi kama wanataka kutetea ubingwa huo wanatakiwa kufanya yafuatayo:-

Wasiruhusu mchezaji mwingine kuondoka

Mara baada ya kuondoka kwa kiungo wake mkabaji aliyekuwa mhimili wa klabu hiyo aliyetimkia uwanja wa Stanford Bridge katika klabu ya Chelsea, Ng’olo Kante, mchezaji mwingine ambaye amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka ni Riyad Mahrez ambaye  amekuwa akisakwa na klabu ya Arsenal.

Hata hivyo, mchezaji huyo tayari amejitia kitanzi ndani ya klabu hiyo kwa kuongeza mkataba mwingine mpya ambao utamfanya akae kwa muda mrefu.

Kati ya wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika ubingwa wa Leicester ni mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 17 na kutoa pasi 11 za mwisho kwa mshambuliaji, Jamie Vardy aliyefunga mabao 24 msimu uliopita.

Kuondoka kwa kiungo Kante ambaye ndiye aliyekuwa roho ya timu msimu ulipita na uwezo wake mkubwa kufananishwa na mchezaji wa zamani wa nchini Ufaransa, Claude Makelele, kutaipa tabu timu hiyo.

Wapunguze presha

Wanapaswa kupunguza presha kutoka kwa mashabiki wao ambao watakuwa wanahitaji kuona klabu yao hiyo ikiendelea kupata matokeo mazuri pia msimu huu kama msimu uliopita waliochukua ubingwa.

Hawatakiwi kushusha kasi yao ya uchezaji ya msimu uliopita ukizingatia aina ya wachezaji walioongezwa msimu huu katika  nafasi ya ushambuliaji, Ahmed Musa kutoka CSKA Moscow na Demarai Gray kutoka Birmingham City, ni wachezaji wenye kasi na nguvu na tayari wamemwonyesha kocha wao Ranieri kuwa wana kitu cha ziada.

Ni wazi kwamba kwa sasa klabu hiyo itakuwa na msimu mgumu zaidi mara baada ya kuchukua ubingwa kwa kuwa watakuwa wanashiriki zaidi ya mashindano manne, Ligi Kuu ya England, Klabu Bingwa Ulaya, Kombe la FA na Caring Cup ambapo kocha Ranieri anapaswa kupunguza presha kwa vijana wake kwa kuwa wana mashindano makubwa zaidi tofauti na mwaka jana.

Awape nafasi vijana

Kikosi hicho chenye wakongwe wengi akiwamo nahodha, Wes Morgan (32), Robert Huth (31), Danny Simpson (29), Christian Fuchs (30), Marcin Wasilewski (36), ni muda mwafaka kwa kocha huyo kuanza kuwaamini na  kuwapa nafasi  vijana waliopandishwa katika kikosi chake.

Ranieri ni kati ya makocha wanaowaamini vijana hivyo haishangazi mara baada ya kumpa nafasi  ya kumwanzisha kiungo, Andy King katika pambano lake dhidi ya Manchester United walilopoteza kwa mabao 2-1 na miamba hiyo ya Old Trafford kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mpya kutoka Nice, Nampalys Mendy.

Kocha   huyo amewaamini na kuwapa nafasi vijana wanne katika kikosi chake msimu huu ambao ni Jeff Schlupp, Andy King, Liam Moore na Ben Chilwell ambao wameonyesha uwezo mkubwa hivyo anapaswa kuwapa nafasi zaidi  vijana  hawa ambao watakuwa na mchango zaidi katika kikosi hicho.

Waliosajiliwa waoneshe uwezo

Wachezaji walioongezwa msimu huu wanapaswa kuonyesha thamani yao kwanini walinunuliwa na mabingwa hao ambao wanasifika kwa soka lao la kushambulia kwa kushtukiza.

Tayari miamba hiyo imefanya usajili kwa baadhi ya wachezaji ambao imewaongeza katika kikosi chake kama vile Demarai  Gray kutoka Birmingham City, Ahmed Mussa  kutoka CSKA Moscow, Nampalys Mendy kutoka Nice, Raul Uche kutoka Rayo Vallecano, Daniel Armatey kutoka  Cf Copenhagen na Luis Hernandez kutoka Sporting Gijon.

Wachezaji hao ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika mechi za kujiandaa na msimu mpya wa ligi,  wanatarajia kudhihirisha thamani yao msimu huu na kukisaidia kikosi hicho kutetea taji walilochukua msimu uliopita.

Hata hivyo, kocha huyo bado ana nafasi ya kuendelea kusajili kwa kuwa dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa kesho kutwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles