27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

LATRA yatoa onyo kampuni za mabasi zilizoanza safari za saa 24

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa onyo kwa kwa baadhi ya Kampuni za Mabasi za masafa marefu ambazo zilianza kufanya safari za usiku ikiwa ni kinyume cha utaratibu na sheria.

Onyo hilo limetolewa Agosti 18, 2023 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabarani LATRA, Johansen Kahatano ambapo amesema utaratibu wa magari ya masafa marefu kuanza kutembea kwa saa 24 bado upo kwenye mchakato hivyo ni kosa kwa mabasi kufanya safari hizo bila kufuata utaratibu.

Amesema kumekuwa na baadhi ya mabasi ambayo yameruhusiwa kuanza safari saa tisa usiku kulingana na umbali wa mahali yanapokwenda.

“Hivi karibuni kumeibuka baadhi ya makampuni zinafanya safari za usiku kinyume na taratibu tumeshapokea taarifa zao ambao tumesha wapa onyo ikiwa ni pamoja na kuwapiga faini,”amesema Kahatano.

Amesema lengo la LATRA si kutoa adhabu bali ni kutoa elimu, hivyo watumizi wa barabara wanapaswa kufuata elimu inayotolewa ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea.

“Nitoe rai kwa mabasi ambayo yameanza kufanya safari za usiku lakini pia abiria ambao wanapanda gari hizo kuacha mara moja kwani wanahatarisha maisha yao na wakumbuke pia usiku huo kuna baadhi ya maeneo hakuna askari wa usalama barabarani hivyo wanaweza kupata shida na wakakosa msaada,”amesema.

Akizumgumza kuhusu utaratibu wa mabasi kuanza kutembea kwa saa 24 amesema upo kwenye mchakato na karibu utakamilika hivyo wamiliki wanapaswa kuanza kupeleka maombi.

Amesema maombi yao ni sehemu ya maandalizi kwani watachakata na kujua njia gani itaanza na huduma hiyo na gari zipi.

Amesema kuanza kwa safari hizo kunapaswa kuwa na maandalizi ikiwemo uwepo wa huduma zote muhimu njiani kama ilivyo kwenye safari za mchana ili kuondoa kero kwa abiria watakao kua safarini kwa nyakati za usiku.

“Safari za usiku zitaanza kwani mchakato wake unaendelea, hivyo tuwaombe wamiliki kuleta maombi yao lakini pia tunahakikisha miundombinu yote inakuwa rafiki kwa wasafiri ikiwemo huduma za usalama,”amesema Kahatano.

Juni, mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa agizo la kuanza safari kwa saa 24 wakati akihitimisha shughuli za Bunge hivyo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bado ipo kwenye mchakato wa kushughulikia jambo hilo ambapo LATRA watatoa ratiba ya kuanza safari hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles