Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
BEKI wa Yanga, Lamine Moro amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo, baada ya kurejea nchini na kusema amerudi kufanya kazi, akipania kuwaonyesha kazi watani wao wa jadi, Simba.
Yanga wanatarajiwa kukipiga na Simba Januari 4, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hivi karibuni Lamine aliondoka nchini na kwenda kwao Ghana, akidaiwa kuvunja mkataba na Wanajangwani hao kutokana na kutolipwa mishahara yake ya miezi mitatu.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Azam TV, Lamine alisema amerejea kuungana na wenzake tayari kufanya kazi itakayowapa raha mashabiki wa timu hiyo.
“Mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwani nimerejea nchini kufanya kazi, hivyo nitaungana na wenzangu katika maandalizi ya mechi zinazotukabili mbele yetu,” alisema.
Akizungumzia mechi yao dhidi ya Simba, Lamine alisema michezo yote ni sawa ila anaamini watafanya vizuri kutokana na maandalizi watakayofanya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli, alisema timu yao inatarajia kurejea Dar es Salaam leo ikitokea Kigoma ilikokwenda kucheza mechi mbili za kirafiki.
“Baada ya timu kuwasili, wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja na baada ya hapo, wataendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Iringa United, mchezo utakaochezwa Desemba 22, mwaka huu, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam pamoja na mechi za ligi,” alisema.
Juu ya Lamine, alisema kuwa ataungana na wenzake mazoezini baada ya mapumziko waliyopewa.