Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Agnesta Lambert, ameitaka Serikali ijipange kwa kukaa na watalaamu wenye weledi katika sheria kabla ya kupeleka muswada huo katika kamati za Bunge.
Lambert amezungumza hayo Bungeni, Dodoma juzi wakati akichangia muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba (2)za mwaka 2021 uliowasilishwa kwa wabunge kwa ajili ya kuupitishwa.
‘’Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria niliiupitia huo muswada ambao uliletwa kwetu na Serikali, nikiri muswada huo haukuwa na taswira ya maslahi mapana ya nchi kutokana na sheria hizo kuwa na mapungufu,’’ amesema mbunge huyo.
Amesema Serikali ilipoleta muswada wa sheria alikuwepo, ilichukua maoni na mapendekezo yao na kufanyia kazi lakini yale mambo yaliyoandikwa humo kamati isingekuwa na weledi wa kutosha yangetokea majanga makubwa.
‘’Ule muswada ulipoletwa katika kamati yetu kama tungekuwa tumeamka vibaya yangetokea kama
mambo ya tozo za kwenye miamala ya simu, lakini kwa kuwa tuliamka vizuri tuliweza kuchambua huo muswada na kufanya marekebisho’’, amesema.
Lambert amesema Serikali ilileta sheria nyingi ambazo zilitakiwa kufanyiwa marekebisho, hivyo ameshauri wangetafuta wataalamu wenye weledi ili kuandika sheria hizo ndipo zipelekwe kwenye kamati ili kusiwe na kazi kubwa kuzirekebisha.
‘’Nashauri Serikali kabla ya kuleta muswada huo watafute wabobezi katika sheria, watalaamu wakae chini na Serikali kuleta muswada wenye maslahi mapana kwa Taifa, ili hata sisi wanakamati tusipate shida katika kurekebisha baadhi,’’ amesema mbunge huyo.
Amesema kinachotakiwa kwa kamati wanapopelekewa muswada, wanatakiwa kurekebisha vitu vidogo na si kuufumua wote, kitu ambacho kinaweza kugharibu baadae,” amesema Lambert.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kufanyia kazi mapendekezo yao licha ya kuwa walifanya kazi kubwa kufanya marekebisho ya sheria hizo.
Pia ameipongeza Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba chini ya mwenyekiti wao, waliofanya kazi kubwa kwani Sheria 12 zote zilizoletwa na Serikali wamezifanyia marekebisho hakuna sheria hata moja ambayo haikuguswa.
Naye Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama ametoa taarifa kuwa anakubali ushauri na maoni ya wabunge na kuomba aweke vizuri taarifa hiyo lakini Mbunge anaposema kuwa kamati imeiondoa sheria iliyowekwa na Serikali siyo sahihi.
Amesema Serikali imeleta sheria ndogondogo, isipokuwa sehemu ya sheria iliyoletwa katika kamati imeondolewa ili wasiwachanye watu.