30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Lala salama VPL chungu pande mbili

Azam-vs-Yanga-3NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuanza Jumamosi hii huku ushindani mkubwa ukiwa kwa pande mbili ambazo ni timu zinazopigana vikumbo kuwania ubingwa na zile zinazopambana kuepuka kushuka daraja.

Mabingwa watetezi Yanga na Azam FC ndio wanaonekana kukamiana zaidi katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu, ambapo zimemaliza mzunguko wa kwanza katikati ya wiki iliyopita zikiwa hazijafungwa mchezo hata mmoja huku zote zikiwa na pointi sawa.

Licha ya timu zote kujiwekea kibindoni pointi 39 kutokana na mechi 15, Yanga ipo kileleni kutokana na tofauti ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga tayari wamepachika wavuni mabao 36 ikiwa ni tofauti ya mabao sita dhidi ya wapinzani wao Azam FC, huku Simba iliyopo nafasi ya tatu wakifikisha mabao 23 ya kufunga.

Kwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga ndiyo timu iliyofungwa mabao machache kwa kuruhusu nyavu zake kutikisika mara tano na kufuatiwa na Simba na Mtibwa Sugar ambazo zimefungwa mabao tisa kila moja huku Azam ikikubali kufungwa mara 10.

Simba ambayo imeonekana kubadilika na kushinda michezo yake miwili ya ligi tangu Jackson Mayanja achukue mikoba ya Dylan Kerr, imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 33 wakifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye pointi 28.

Msimu huu, Stand United ya Shinyanga imeimarika zaidi tofauti na msimu uliopita, ambapo inashika nafasi tano kwenye msimamo baada ya kufikisha pointi 28 sawa na Mtibwa Sugar iliyoanza ligi vizuri na nyuma yake kwa pointi moja ni Tanzania Prisons.

Coastal Union wamejiweka katika mazingira mgumu kutokana na kupata matokeo yasiyoridhisha msimu huu, ambapo wamemaliza duru ya kwanza wakiwa nafasi ya 14 kwa kufikisha pointi 10 ambazo ni ushindi wa mechi moja kati ya 15 walizocheza.

Halikadhalika, Kagera Sugar msimu huu si wazuri kutokana na nafasi waliyopo ambapo ni timu ya mwisho baada ya kushinda mechi mbili, kutoa sare tatu na kufungwa mechi 10 hivyo kujikusanyia pointi tisa.

Timu ya African Sports iliyopanda daraja msimu huu nayo pia imepata matokeo mabaya mzunguko wa kwanza baada ya kujikusanyia pointi tisa na kuizidi Kagera Sugar kwa tofauti nzuri ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindani wa kuwania ubingwa unazikabili zaidi Yanga, Azam FC na Simba, lakini kwa upande wa timu zinazopigana zisishuke daraja mambo ni magumu zaidi kutokana na kuwa na tofauti ndogo ya pointi

Timu mbili zitashuka daraja na upinzani mkubwa kwenye kuepuka kushuka daraja upo kati ya Ndanda FC, JKT Ruvu, Majimaji FC, Coastal Union, Kagera Sugar na African Sports.

Makocha wanaozinoa timu hizo wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha wanazinusuru timu zao na janga la kushuka daraja, kwa kuanza kupata matokeo mazuri katika mzunguko wa pili unaoanza Jumamosi hii.

 

 

MSIMAMO LIGI KUU BARA

 

P     W   D    L    GF GA        PTS

Yanga                15   12   3     0     36   5     39

Azam FC           15   12   3     0     30   10   39

Simba                 15   10   3     2     23   9     33

Mtibwa Sugar          15   8     4     3     17   9     28

Stand United            15   9     1     5     17   12   28

Prisons        15   8     3     4     16   15   27

Mwadui FC              15   7     4     4     18   14   25

Toto Africans           15   4     5     6     13   18   17

Mgambo JKT           15   4     4     7     13   16   16

Mbeya City              15   3     5     7     13   19   14

Ndanda FC        15   2     6     7     13   17   12

JKT Ruvu          15   3     3     9     16   27   12

Majimaji FC             15   3     3     9     9     29   12

Coastal Union          15   1     7     7     8     17   10

African Sport           15   2     3     10   4     15   9

Kagera Sugar           15   2     3     10   5     19   9

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles