Laini za simu kuzimwa kuuma kila upande

0
799
Wananchi wakisubiri kupata namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Ubungo, Dar es Salaam jana.

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

IKIWA zimebaki saa chache kabla ya kesho saa sita usiku kuzimwa kwa laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, imeelezwa athari za hatua hiyo mbali na watu kukosa mawasiliano, pia kutakuwa na athari za kiuchumi.

Endapo hakutakuwa na suala la kuongeza muda kama ilivyofanyika awali ambapo laini hizo zilikuwa zizimwe Desemba 31, mwaka jana saa sita usiku, kabla Rais John Magufuli hajaongeza muda, kampuni za simu na Serikali zinatarajiwa kupoteza mabilioni ya fedha.

Katika kila muamala wa simu ambao hufanywa na mteja, kampuni za simu hupata asilimia fulani huku nayo Serikali ikipata kodi.

Pia mteja wa simu akipiga simu, Serikali inapata kodi huku kampuni za simu nazo zikipata fedha.

Mbali na mapato hayo, biashara zinazotegemea simu kama za kukodi magari kwa njia ya mtandao, michezo ya kubashiri matokeo ya mpira, zote zinatarajiwa kuathiriwa, hasa ikizingatiwa zaidi ya asilimia 40 ya laini za mkononi hazijasaliwa kwa alama za vidole.

Sheria ya Fedha iliyopitishwa na Bunge la Bajeti 2016/17 ilianzisha kodi mpya ya  asilimia 10 ya ushuru wa huduma (service levy) kwenye kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu pamoja na benki.

Kodi hiyo ni tofauti na ile ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18. 

Kupitia utaratibu huo, Serikali inatoza kodi kwenye gharama za kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu au benki. 

MIAMALA YA FEDHA 

Ripoti ya takwimu za mawasiliano (Telecom Statistics) inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha miamala ya fedha iliyofanywa kuanzia Januari hadi Septemba mwaka jana ilikuwa milioni 756.3 yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 16.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kipindi cha robo ya tatu (Julai – Septemba 2019), watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi walikuwa 23,692,806.

Kampuni ya simu na idadi ya watumiaji kwenye mabano ni Airtel (4,520,774), Halo Pesa (1,564,125), Tigo Pesa (6,877,909), TTCL (582,962), M-Pesa (9,762,427) na Ezy Pesa (384,609).

Katika kipindi hicho, watumiaji wa huduma walifanya miamala 252,369,669 ambapo idadi ya miamala kwa kila kampuni ilikuwa Airtel Money (42,203,871), Halopesa (10,487,103), Tigo Pesa (77,404,291), TTCL (623,097), M–Pesa (119,161,439), Ezy Pesa (2,489,868).

Aidha katika robo ya kwanza (Januari hadi Machi) miamala iliyofanywa ilikuwa milioni 243.52 yenye thamani ya Sh trilioni 7.82.

Katika robo ya pili (Aprili hadi Juni) miamala iliyofanywa ni milioni 260.43 yenye thamani ya Sh trilioni 8.31.

Huduma za kifedha zinazotumika zaidi kupitia simu za mkononi ni kutuma na kupokea fedha, kuhamisha fedha kutoka katika akaunti ya benki, mikopo midogo midogo, akiba, bima na nyingine.

Kutokana na mchanganuo huo, Serikali ilipata mabilioni ya fedha kiasi ambacho kinaweza kuathirika kutokana na baadhi ya watumiaji kufungiwa laini zao.

WATAALAMU WA UCHUMI

Wakizungumza na MTANZANIA jana, wataalamu wa masuala ya uchumi na fedha walisema kuzimwa kwa laini ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole, kutasababisha athari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, kampuni za simu na Serikali.

Profesa wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi, alisema;  “Suala lolote la simu ni biashara, mapato yatapungua, ni sawa na uwe na mteja ananunua sukari kila siku, sasa ameamua kutokunywa chai, lazima kipato chako kitapungua.”

Profesa Moshi pia aliwataka Watanzania wabadili tabia, hasa kunapokuwa na mambo ya msingi badala ya kusubiri hadi muda unapofikia ukingoni.  

“Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) nao waongeze kasi, kuwe na ‘coordination’, bila hivyo tutakuwa tunawanyima wananchi haki zao za msingi, si kwa kupenda bali kutokana na kasi ya utoaji vitambulisho kuwa ndogo,” alisema Profesa Moshi.

Mchumi mwingine, Profesa Samuel Wangwe, alisema zoezi hilo licha ya kwamba litakuwa na athari kiuchumi, lakini kwa upande mwingine litakuwa na faida.

“Siwezi kujua watakaokosa huduma ni wangapi kwa sababu wengine wana laini zaidi ya moja, lakini athari za kiuchumi mauzo yanaweza kupungua, kutapeliwa kutapungua, nayo ni nafuu fulani,” alisema Profesa Wangwe.

MAMLAKA YA MAPATO

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kwa sasa hawawezi kutoa tathmini yoyote ya kodi hadi zoezi hilo lipite.    

“Ngoja zoezi hili lipite, nisingependa kutia neno lolote sasa hivi,” alisema Kayombo.

WAFANYABIASHARA

Anderson Haule ambaye ni dereva teksi jijini Dar es Salaam, alisema amekuwa akifanya shughuli zake kupitia programu ya Uba ambayo hukutanisha wateja na watoa huduma za usafiri huo, hivyo kuzimwa kwa laini kunaweza kumwathiri kwa sababu programu hiyo huendeshwa kupitia simu za mkononi.

“Ili utumie Uba ni lazima ‘ui–download’ (kupakua) katika simu yako ya mkononi, sasa kama mtu atafungiwa laini yake na alikuwa anatumia programu hii, tayari hapo umepoteza mteja,” alisema Haule.  

Naye Amina Maulid anayefanya biashara ya kuuza matunda, alisema anahofia atapoteza wateja kwa sababu hadi sasa bado hajajisajili.

“Yaani sijui itakuwaje kwa sababu mpaka sasa sijapata namba wala kitambulisho, wateja wangu huwa wananipa oda kupitia katika simu na wengine nawapelekea hadi ofisini,” alisema Amina. 

WANANCHI WA KAWAIDA

Huduma za kifedha kupitia simu pia zimekuwa ni mwarobaini, hasa kwa wananchi wengi wa vijijini ambao wanaishi mbali na huduma za kibenki. 

Mkazi wa Temeke, Lilian Mushi, alisema kabla kampuni za simu hazijaanza kutoa huduma za kifedha, alikuwa akilazimika kuwatumia fedha za matumizi wazazi wake walioko kijijini kupitia kwenye mabasi.

Kwa mujibu wa Lilian alikuwa akichajiwa Sh 1,000 katika kila Sh 10,000 wakati akituma kiasi kama hicho kupitia simu ya mkononi huchajiwa Sh 300.

“Kwahiyo kama nikituma Sh 30,000 lazima nilipie gharama za kutuma Sh 3,000. Halafu mama bado atalazimika kuacha shughuli zake na kuingia gharama ya kulipa nauli hadi mjini (kwenye ofisi za basi husika) kwenda kuchukua fedha.

“Kutoka nyumbani kwetu hadi mjini nauli ni Sh 1,000, hivyo kwenda na kurudi analipa Sh 2,000, gharama inakuwa kubwa zaidi na anapoteza muda,” alisema Lilian. 

Mkazi mwingine wa Tabata, Dar es Salaam, Nasoro Abdallah, alisema; “Mwezi uliopita nilimtumia baba yangu fedha kupitia M–Pesa ili afanye ‘wirering’ (kuweka mfumo wa umeme) nyumbani. 

“Kama huduma hizi zisingekuwepo, ingebidi nisubiri hadi nikienda likizo na pengine fedha ningeweza kuzitumia, si unajua tena maisha hayatabiriki,” alisema Abdallah.

LAINI KUZIMWA KESHO

Laini ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole zinatarajiwa kuzimwa rasmi kesho.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha hadi kufikia Januari 12 mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

Laini za simu 22,478,727 sawa na asilimia 46.3 bado hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole.

Aidha takwimu zilizotolewa Januari 2 mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk. Anold Kihaule, zinaonyesha watu milioni 7.6 tayari wana namba, na kila siku mamlaka hiyo inaendelea kutoa sehemu mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba, alisema zoezi hilo ni endelevu, hivyo kwa watakaositishiwa huduma, wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la kuzirudisha au kupata laini mpya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here