25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaya ya Gethsemane watoa msaada kwa wagonjwa wa fistula CCBRT

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waimba kwaya wa Kikundi cha Gethsemane wa Kanisa la Wasabato (SDA) Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, wametoa msaada kwa wagonjwa fistula wanaotibiwa katika Hospitali ya CCBRT ikiwa ni sehemu ya kuonesha matendo ya huruma kwa wenye uhitaji.

Wanakwanya hao waliongozwa na Mchungaji wa Mtaa wa Kinondoni, Masunya Anthony, Mzee wa Kanisa, Emmanuel Mgonja na mlezi wa kwaya hiyo ambapo wametoa msaada huo leo hospitalini hapo ikiwa ni sehemu ya kuelekea Oktoba 13 mwaka huu ikiwa ni maandalizi ya kwaya hiyo kuzindua DVD mbili katika Ukumbi wa Uhuru JKT Mwenge jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia msaada huo, Mwalimu wa kwaya hiyo, Stella Malingoza amesema mwaka huu kwaya hiyo imetimiza miaka 10 na wanajiandaa kuzindua DVD hivyo wameona ni vema kabla ya kufanyika kwa uzinduzi wakatoa msaada huo ambao ni sabuni, mafuta ya kupakaa, dawa ya meno na mswaki.

“Kwaya yetu ya Gethsemane tumekuwa na utamaduni wa muda mrefu wa kujitoa kwa misaada ya aina mbalimbali, tunaweza tusiwe tumetoa msaada mkubwa lakini kile ambacho tunakipata huwa tunakipeleka kwenye jamii ambayo ina uhitaji.

“Hivyo tumekuja CCBRT kwa ajili kuwaona mama zetu na dada zetu wenye kusumbuliwa na ugonjwa fistula na kadri tukavyopata tutarudi kwao na kwa wengine.

“Thamani ya msaada wote ambao tumeutoa katika wodi hii ya wagonjwa fistula una thamani ya zaidi ya Sh milioni 2.4 na tunajua wanakabiliwa na changamoto nyingi na wanamahitaji mengi lakini hiki kidogo ambacho tunacho tumeona tuwaletee na kuwakabidhi,” amesema Stella.

Kwa upande wake Mchungaji Anthony,   ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa watu wanapokuwa wagonjwa wakati mwingine inakuwa ngumu kupata neno la Mungu kwa usahihi, hivyo kwa kutambua hilo wameona Kanisa la SDA Mtaa wa Kinondoni linawajibu wa kuwafikia wagonjwa na kuzungumza nao ikiwa pamoja na kufanya maombi.

naye Mzee wa Kanisa, Mgonja amesema wanapokwenda kutimiza miaka 10, wameona ni vema wakashiriki kuwaona wagonjwa na kuwasaidia kwa kidogo walicho nacho.

“Kabla ya kufanyika kwa uzinzudi wa DVD mbili siku hiyo ya Oktoba 13 mwaka huu tumeona ni vema tukaja hapa kwa ajili ya kuwasalimia wagonjwa hawa wa fistula , kushiriki nao kufanya mambo na kisha kutoa msaada huu ambao tumekuja nao,”amesema Mgonja.

Awali  Muuguzi katika Hospitali ya CCBRT ambaye anahudumia wagonjwa wa Fistula Theodora Masako amesema kuwa ugonjwa huo unatibika lakini changamoto iliyopo wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa huo wamekuwa wagumu kufika hospitali kupata matibabu kwasababu mbalimbali ikiwemo ya kuhofia gharama za matibabu na wengine kuamini wamepata tatizo kwasababu ya imani za kishirikina.

“Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu ugonjwa huu ambao hauna uhusiano na ushirikina, na wala matibabu yake hayana gharama yoyote ile na hapa kwetu tunatoa matibabu bila malipo.Hata hivyo tutumie nafasi hii kuishukuru kwaya hii ya Gethmane kwa kutambua umuhimu wa kutoa msaada wao kwa ajili ya wagonjwa hawa ambao tunawahudumia hapa hospitalini kwetu,”amesema Masako.

Amesema wagonjwa wanapoona wanatambelewa wanafarijika na kuwapa moyo kuwa wapo watu ambao wanawathamini na kuwajali kwani moja ya changamoto ya ugonjwa huo, wengi wao wamekuwa wakitengwa na jamii na wakati mwingine hata na familia zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles