31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI WAPIGAKURA WANAPUNGUA?


NA MARKUS MPANGALA  |  

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro, yamenikumbusha ya mwaka 2010 katika nafasi ya urais. Kwanza nawapongeza wabunge, Dk. Godwin Mollel na Maulid Mtulia kwa kuibuka washindi katika kinyang’anyiro ambacho hakijashangaza kukabidhiwa vyeti vya ushindi.

Matokeo hayo yamenifikisha kwenye hitimisho la kwamba jukumu ‘tulilonalo’ sasa na tuendako ni kuwabembeleza watu (wananchi) kupiga kura. Namba zinashuka kwa kasi mno!

Kwa mfano kutoka wapigakura 70,337 wa mwaka 2015 waliompa ushindi Mtulia wa Chama cha CUF hadi kura 30,247 ambazo mbunge huyo huyo amezipata mwaka 2018 katika uchaguzi mdogo na kumpatia ushindi kupitia chama chake kipya cha CCM.

Swali ni kuwa wako wapi wapigakura 40,000 waliomchagua Mtulia mwaka 2015? Kama jawabu letu litakuwa  wamempa kura mgombea wa chama cha Chadema, Salum Mwalimu, basi namba zinaonyesha alipata kura 11,353. Hivyo basi nakisi yetu inakuwa wapigakura 28,647 wamekwenda wapi?

Nitafafanua zaidi. Katika Jimbo la Kinondoni, wapigakura walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ni 264,000, waliojitokeza kupiga kura ni 130,000. Kwahiyo swali la jumla linaanzia hapo, wako wapi wapigakura 134,000?

Kuna watu watasema majibu yafuatayo; baadhi ya wapigakura wamehama makazi (Kinondoni). Wengine wamefariki dunia. Na wengine hawakupiga kura au kura zimeharibiwa.

Kutokana na upungufu wetu wa kutunza taarifa, sina uhakika kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi-NEC inayo idadi ya wapigakura waliofariki dunia kati ya mwaka 2015 hadi 2018 katika jimbo hilo.

Sina uhakika kama NEC  inayo idadi ya wapigakura waliohama makazi au kubadilisha vituo vya upigaji kura. Zaidi tutakuwa na majibu ya haraka haraka tu.

Nakumbuka Januari 15, 2013, niliandika suala hili kwa kuonyesha takwimu za upigaji kura tangu zama za uongozi wa Mwalimu Nyerere hadi Jakaya Kikwete.

Idadi za upigaji kura zinashuka sana na kwa kasi mno. Wakati fulani tunapolisema jambo hili tunadhaniwa kuwa tuna wivu, kijiba cha roho na kadhalika, lakini mambo hayaendi vizuri katika zoezi zima la upigaji kura.

Ni vema tukajikumbusha jambo hili kwa kuanzia ngazi ya matokeo ya urais. Matokeo ya mwaka 2005 mgombea urais wa CCM, Kikwete, alipata asilimia 80 ya kura zote. Matokeo ya mwaka 2010, mgombea huyo huyo alipata asilimia 61.17 ya kura zote.

Waliojiandikisha kupiga kura ni 20,137,303, waliojitokeza kupiga kura ni 8,626,283. Kura zilizoharibika ni 227,889.

Matokeo ya urais mwaka 2015, mgombea wa CCM, John Magufuli, alipata kura 8,882,935 asilimia 58.46, huku mpinzani wake wa karibu, Edward Lowassa, kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi-Ukawa akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.

Jumla ya wapigakura kwa jumla wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa ni 23,253,982. Ukijumlisha kura za wagombea urais wote, utagundua kuwa hazifiki idadi ya jumla ya wapigakura. Je, wapigakura wanakwenda wapi au wameacha kushiriki zoezi hilo?

Natambua tunaweza kujibu kuwa kura zingine zilikwenda kwa wagombea wa vyama vya upinzani. Lakini hilo ni jibu la upande mmoja.

Naziona namba zinashuka kwa kasi mno, hali ambayo inatulazimu kuwa na jukumu la ‘kuwabembeleza’ wapigakura kushiriki zoezi hilo, ikiwa na maana elimu ya uraia inatakiwa kupelekwa kwao haraka iwezekanavyo.

Kupeleka elimu ya uraia kwa wananchi wiki mbili kabla ya kupiga kura, haisaidii chochote kwa sababu inaonyesha kuna ‘vuguvugu’ ambalo linakwenda mwendo wa taratibu mno juu ya zoezi zima la ushiriki wa kupiga kura.

Mbinu za elimu ya uraia kutolewa fasta fasta hazitatusaidia chochote. Nina hisia (si za kisayansi) zoezi la upigaji kura linaanza kupoteza umuhimu na au maana machoni mwa wananchi. Si ishara nzuri.

Nihitimishe kwa kuweka maneno ya mwanahabari mkongwe na mwanasheria, Emmanuel Kihaule: “Nimepata bahati ya kushiriki kupiga kura toka mwaka 1995, wakati nchi yetu ilifanya uchaguzi mkuu wenye kuhusisha vyama vingi kwa mara ya kwanza. Sitasahau namna gani ushindani ulikuwa mkubwa hususan miongoni mwa vyama vikuu vya siasa bara na visiwani.

“Pia sitasahau mapungufu mengi yaliyojitokeza na kulazimisha zoezi la upigaji kura kurudiwa kwa baadhi ya nafasi; ubunge na udiwani. Nakumbuka sisi wapigakura wa Mbezi Beach (Dar es salaam) ilibidi turudie tena upigaji kura wa wabunge pale Mwenge, Kituo cha Mabasi badala ya Tangi Bovu tulipopiga kura awali.

“Lakini pamoja na mapungufu yote, sikumbuki vurugu zozote kubwa zilizotokea. Chaguzi nyingine zote zilizofuata nilishiriki kuanzia 2000, 2005 na 2010. Nilikuwa mmoja wa watu wanaofika kwanza kituoni. Alfajiri nilikuwa nimeshapanga mstari! Lakini niwe mkweli hamu ya kushiriki imekuwa ikishuka jinsi siku zinavyokwenda.

“Nadhani pia ongezeko la matukio ya vurugu pia yamechangia sana kunikatisha tamaa kushiriki michakato ya kisiasa ikiwepo upigaji kura. Mwaka 2010 kwa mfano, Watanzania waliokuwa na sifa za kupiga kura walikuwa milioni 21, lakini waliopiga kura ni milioni 8 tu ambayo ilikuwa sawa na asilimia 42 tu ya wote wenye sifa ya kupiga kura.

“Sasa naambiwa huko Siha na hata Kinondoni idadi ya wapiga kura hazikuwa sawa kama zilivyotarajiwa. Kinondoni naambiwa kati wa wapigakura 240,000 na ushehe waliojiandikisha, ni chini ya 50,000 waliojitokeza. Tunapokwenda kuna hatari wagombea wakajipigia kura wao wenyewe na familia zao tu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles