26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

KWANINI NAPE SI SHUJAA WANGU

KILA mtu atavuna alichokipanda. Huu ni msemo wa Kiswahili ambao Waswahili tumebahatika kuwa nao kwenye lugha yetu ya Kiswahili.

Hii inamaanisha kwamba kama ulipanda mema basi utavuna mema na kama ulipanda ubaya, basi usitarajie mema bali utavuna huo huo ubaya.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa aliyekuwa Waziri wa Habari ambaye uwaziri wake ulitenguliwa Machi mwaka huu na Rais John Magufuli.

Binafsi simsikitikii Nape japo kwa watu wengine alionekana kama shujaa na anaonekana kama mtu anayestahili kuonewa huruma, lakini kwangu mimi si shujaa na siungani nao na simsikitikii hata kidogo kwa kuwa kila mtu atavuna alichokipanda na yeye anavuna alichopanda.

Tangu uwaziri wake utenguliwe, Nape anaonekana kama mtu ambaye ana msongo wa mawazo na unaweza kuliona ili kama unafuatilia mitandao ya kijamii haswa mtandao wa Twitter.

Anaonekana akiweka mabandiko kadha wa kadha yenye kuonesha ni kwa namna gani alikipigania chama chake na baadhi ya matatizo ya Watanzania aliyoyaona ambayo hayaonekani kupatiwa ufumbuzi, ni kama mtindo fulani wa kutupa jiwe kizani akitegemea yeyote aliyeko uko likimpata basi atatoa sauti.

Kwanini kwangu Nape si shujaa

Anaweza kuwa shujaa wa nafsi yake au kwa nafasi yake lakini si kwa Watanzania, nasema hivi kwa sababu tangu mwanzo kwenye sakata la dawa za kulevya, baada ya kutajwa ile awamu ya kwanza ya orodha ya wauzaji na watumiaji wa maadwa ndipo nilipoiona vita ya mafahari wawili ambayo baadaye ilikuja kuchagizwa na tukio la kuvamia kituo cha redio na runinga cha Clouds.

Ni vita ambayo ilipata watu walionekana kama mwamvuli wa upiganiaji wa haki lakini kulikuwa na masuala binafsi, kweli nimuite Nape shujaa kisa alisema ‘brand’ za watu hasa wasanii zilindwe wakati yeye mwenyewe ni mtuhumiwa wa kuchafua ‘brand’ za watu; rejea kauli ya Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa kuhusu watu kuzunguka na fedha za chama kumchafua, hilo peke yake linatosha kutomuona kama shujaa.

Kwanini simsikitikii Nape

Ni nani kati yetu ambaye anapenda kuona mtu akilipwa mshahara usioendana na kazi aliyofanya? Sisi sote tunapenda haki na ili haki itendeke, kila mtu anatakiwa apate kulingana na kazi aliyofanya. Kama ni hivyo je, tuna sababu gani ya kumhurumia Nape?

Nape huyu huyu aliyekuwa na kauli za kibabe wakati wanatuzimia bunge ‘live’, huyu huyu aliyepeleka muswada wa habari kibabe na kwa majigambo, Nape huyu huyu aliyekuwa na majigambo dhidi ya Watanzania waliokuwa wakilalamika juu ya kauli yake ya kuwa watashinda hata kwa bao la mkono tena akiisema hadharani pasi na woga wowote, huyu ndiye tumhurumie?

Huyu ndiye tumuite shujaa? Hivi mtu akifuga majini halafu yakaja kumuua naye tutamuita shujaa kwa kuwa alipambana sana wakati anatetea nafsi yake kabla ya mauti kumkuta, akifa naye tulie na kumhurumia?

Tatizo la Watanzania tumekuwa wasahaulifu sana na ndiyo miaka yote tumekuwa madaraja ya wanasiasa, huku hali zetu za uchumi zikiendelea kuwa mbaya, usahaulifu ni ugonjwa mbaya sana.

Wanasiasa wengi hasa ambao huwa na nafasi za uongozi hujisahau na kuona kama nafasi hizo huwa za kudumu na ziliandikwa majina yao na wanasahau kuwa hadi kufika hapo, kuna ngazi walipanda ambayo kwa kawaida ukifika juu hamna mahala pa kwenda tena lazima ushuke, hivyo nawaasa kuheshimu wananchi bila kujali nafasi uliyonayo.

Hivi nani aliwahi kudhani kama Lowassa na Sumaye wanaweza kulalamika kuhusu askari kama alivyowahi kulalamika aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa? Madaraka hayadumu msijisahau.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles