27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Kwanini Kaseja, Banka ‘beach soccer’?

kaseja_clipNA ZAINAB IDDY

TANZANIA tumebarikiwa kuwa na vipaji vingi vya soka ambavyo vikitumika vizuri vinaweza kusaidia kuipeperusha vema bendera ya taifa letu.

Licha ya vipaji vingi kuwepo mitaani, lakini pia kwenye ligi mbalimbali za soka wapo wanasoka ambao kwa sasa hawapati nafasi kwenye timu zao kutokana na ushindani wa namba uliopo.

Mfano mzuri wapo akina Pato Ngonyani, Said Makapu, Mohamed  Ibrahim, Said Ndemla, Beno Kakolanya, Benedict Tinoco na wengineo ambao wana uwezo wa kuipa mafanikio timu ya taifa kama wakipewa nafasi na kutunzwa vizuri.

Licha ya hao, klabu ya Azam FC ina kituo kinachozalisha wachezaji kuanzia miaka minane hadi 20, lakini siku zote vijana hawa wanaomba kwa Mungu ili wapate nafasi ya kulitumikia taifa.

Pamoja na kuwepo kwa chipukizi hao, bado kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni ‘beach soccer’, alishangaza wengi hivi karibuni baada ya kutangaza kikosi cha wachezaji 17 wakiwamo kipa mkongwe, Juma Kaseja na beki Mohamed Banka.

Kwa mujibu wa maelezo ya kocha huyo, amewaita ili waweze kuongeza nguvu kwenye kikosi chake ambacho awali kilifungwa mabao 7-3 na wapinzani wao   Ivory Coast katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kocha John Mwansasu, anaamini uwepo wa Kaseja na Banka unaweza kusaidia timu hiyo kutimiza ndoto za kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na hata kutwaa ubingwa.

Si jambo la ajabu kwa Banka na Kaseja kuitwa kwenye timu hiyo, lakini ni kwanini wachaguliwe hao ambao hawapati nafasi katika timu zao kutokana na kuzidiwa uwezo na vijana.

Inafahamika wazi kwamba Kaseja aliyecheza Simba na Yanga miaka ya nyuma, si huyu wa sasa ambaye anakipiga katika timu ya Mbeya City, huku upande wa  Banka ukiwa hivyo hivyo.

Kiufundi sijui Mwansasu ametumia kigezo gani kuwaita wakongwe hao, lakini ukweli utabaki kuwa hawakustahili kuwepo kwenye kikosi chochote kinachowakilisha nchi wakiwa kama wachezaji.

Lisingekuwa jambo la kushangaza kusikia Kaseja na Banka wameitwa ili kuliongezea nguvu benchi la ufundi la timu ya taifa ya ufukweni, kama ilivyo kwa upande wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’.

Wasiwasi wangu juu ya uteuzi wa wachezaji hawa unalenga kutaka kujua ukweli kama wameitwa kwa mapendekezo ya Mwansasu mwenyewe au kuna mabosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wametia mkono wao.

Naamini vijana wa Tanzania hususani upande wa soka walistahili kupewa nafasi hii kwani wangeweza kufanya makubwa ambayo yangeleta maendeleo kwenye soka la ufukweni na kuondokana na hali mbaya ilivyo kwa mchezo huo sasa.

Ni wakati wa kufanya uamuzi sahihi pale linapokuja suala la uteuzi wa timu ya taifa kwa kuangalia uwezo wa mchezaji na si matakwa ya watu wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles