23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

KWANINI JIM REEVES NI KIVUTIO MSIMU WA KRISMASI?

original

Na Markus Mpangala,

DESEMBA 25, kila mwaka waumini wa imani ya Kikristo wanaadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Siku hii ni muhimu sana kwao kujifunza mambo mbalimbali ya kimaisha.

Wapo watu wanaokubali kuwa Krismasi huunganisha baadhi ya familia. Msingi wa siku hii kwa kila Mkristo anatakiwa kuamini kuwa ni siku ambayo inatakiwa kuifanya familia iishi kwa amani na upendo.

Miongoni mwa wanaofanikisha kuifanya siku ya Krismasi kuwa na upendo na amani ni mwimbaji maarufu, Jim Reeves. Mwanamuziki huyo amefanikiwa kuziunganisha familia kutokana na uwezo wake wa kimuziki na kuwaimbia waumini juu ya kuheshimu na kuzingatia imani zao pamoja na kuilinda, kuipenda na kuzithamini jamii zinazowazunguka.

Kimsingi Jim Reeves jina lake halisi ni James Travis Reeves, amezaliwa mjini Texas nchini Marekani, aliiteka dunia kutokana na umahiri wa kuimba na kutunga nyimbo za Krismasi. Miondoko yake ilikuwa ya muziki wa ‘Country’.

Historia ya mwanamuziki huyo nguli inasema katika maisha yake ya kimuziki alivutiwa na Jimmie Rodgers, Moon Mullican, Bing Crosby, Eddy Arnold na Frank Sinatra. Aidha, katika kipindi chake cha awali akianza muziki alivutiwa na nyimbo za ‘Each Beat of my Heart’ na ‘My Heart’s Like a Welcome Mat’ zilizotamba katika miaka ya 1940 hadi  mwanzoni mwa miaka ya 1950.

Baadaye Jim Reeves alianza kutoa nyimbo zake muhimu za muziki. Nyimbo zilizotamba ni ‘I Love You’ ambao alishirikiana na Ginny Wright. Pia nyimbo za ‘Mexican Joe’ na ‘Bimbo’. Baadaye alitamba na kibao cha  “Four Walls” ambao ulitamba kwa muda mrefu sana kisha kuwavutia watu wengi kutokana na umahiri wake wa kimuziki.

Nyimbo nyingine zilizobamba zaidi ni kama vile “Adios Amigo”, ‘Welcome to My World’ na ‘Am I Losing You? Lakini zinazopendwa zaidi na wapenzi wa muziki wake ‘C-H-R-I-S-T-M-A-S’, ‘Blue Christmas’ na ‘An Old Christmas Card’.

Hakuishia hapo kwani alifanikiwa kutengeneza vibao vingine vikali vilivyopendwa sana na mashabiki wa muziki wake kama ‘We Thank Thee’, ‘Take My Hand, Precious Lord’, ‘Across The Bridge’ na mwingine wa ‘Where We’ll Never Grow Old’.

Baadaye Jim Reeves, alishirikiana na  Joe Allison, kutengeneza wimbo wa ‘He’ll Have to Go’, uliowapatia umaarufu mkubwa sana. Mwaka 1963 alifanikiwa kutoa albamu yenye nyimbo za Krismasi iitwayo ‘Twelve Songs of Christmas’.

Kwa umaarufu, Jim Reeves alimfikia mwanamuziki mkongwe, Elvis Presley na alifanikiwa kutengeneza baadhi ya nyimbo kwa lugha ya Afrikaans inayozungumzwa Afrika Kusini ambako alikuwa na soko kubwa kama ilivyokuwa kwa wengine, Elvis Presley na Slim Whitman.

Baadaye alifanya ziara za kimuziki na wanamuziki wa kundi la Blue Boys nchini Ireland Mei 1963. Nyimbo nyingine zilizotesa kwa utunzi bora ni “Juanita”, “I Love You Because”, “I Won’t Forget You”, “Make the World Go Away”, “Missing You” na “Is It Really Over?, “I Can’t Stop Loving You”,  “I’m a Hit Again”.

Hizo ni baadhi ya nyimbo za mwanamuziki huyo ambazo zilitesa sana wakati wake na sasa zinaendelea kuwafurahisha wapenzi wake. Pia nyimbo zake zimekuwa na ujumbe mzito sana kwa jamii ndiyo maana kila ifikapo wakati wa Krismasi wengi humkumbuka mwanamuziki huyo.

Kila familia huwa inatakiwa kukumbuka ujumbe wake wa mwaka 1992 ambao ulitolewa kutokana na mashairi ambayo hakuwahi kuyatumia. Ujumbe huo uliimbwa katika wimbo wa ‘Don’t Mind If I Do’ kwa kusisitiza amani, upendo na ukarimu kwa watu wote kama maagizo ya mwenyezi Mungu yanavyosema.

Sababu za Jim Reeves kuwa kivutio msimu wa Krismasi

Jim Reeves alikuwa mahiri wa kuisoma jamii yake, ilimpa sifa ya kutazamwa kama miongoni mwa manabii waliotumia muziki kuwaunganisha watu bila kujali rangi, kabila, nchi au mipaka ya nchi yoyote.

Muziki wake uliifanya jamii ifikirie zaidi kupendana na kuzifanya familia kuwa chachu ya amani duniani. Kila muumini wa Kikristo huu ni wakati wa kutafakari ujumbe wake na jinsi alivyoipenda dunia.

Bila shaka Mwenyezi Mungu alimleta mwanamuziki huyo kama nyenzo na mfano wa kuonyesha namna gani wanadamu tunatakiwa kuishi. Miondoko yake ya kimuziki na mashairi aliyotunga yalilenga kugeuza chuki kuwa upendo na penye dhiki pawe na faraja.

Penye uchungu pawe na furaha na penye amani izidi kudumishwa. Jim Reeves ni mkali wa nyimbo za Krismasi na amefanikiwa kuifanya siku kama ya leo kuwa ya amani na upendo zaidi duniani.

Ni wakati wa waumini wa dini ya Kikristo na wengine kuamini kuwa hakuna jambo zuri maishani kama upendo na amani miongoni mwao na wengine na katika wimbo wa “Blue Christmas” anatukumbusha mambo ya msingi kuhusu imani na maisha yetu, hivyo lazima mwanamuziki huyu aheshimiwe na ataendelea kudumu miaka mingi ijayo kutokana na ujumbe wake kwa jamii ya dunia hii.

Jim Reeves alifariki dunia Julai 31, 1964 katika ajali ya ndege. Licha ya kutokuwapo duniani nyimbo zake zenye ujumbe mzito zinafanya mwanamuziki huyo aonekane yupo hai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles