24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI RUGE

Na Bakari Kimwanga -DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Vipindi na Uzalishaji wa Kampuni ya Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49.

Ruge alifariki dunia usiku wa jana katika hospitali alikokuwa akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.

Taarifa za kufariki dunia kwa Ruge zimetangazwa katika taarifa ya habari ya ITV, huku Rais Magufuli akituma salamu za pole kwa wafiwa kupitia akaunti yake ya Twitter.

Kwa muda mrefu Ruge alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya figo na kulazwa hospitali nchini Afrika Kusini kwa miezi kadhaa.

TAARIFA CLOUDS

Jana usiku uongozi wa Clous Media Group, ulitoa taarifa fupi kuhusu kifo hicho.

 “Tunasikitika kutangaza kifo cha mmoja wa waasisi na Mkurugenzi wetu wa Vipindi na Uzalishaji hapa Clouds Media Group, Ndugu Ruge Mutahaba.

“Ruge ametutoka leo (jana) huko Afrika Kusini alikokuwa ameenda kwa ajili ya matibabu. Mioyo yetu imejeruhiwa. Tutaendelea kuwapa taarifa zote kuhusiana na msiba huu mzito,” ilieleza taarifa hiyo.

RAIS MAGUFULI

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli ameandika; “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu, Ruge Mutahaba.

“Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema, Amina.”

DK. NDUGULILE

Akizungumzia kifo cha Ruge, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema msiba huo ni mzito hasa kwa familia, ndugu jamaa na marafiki.

“Ruge wakati wa uhai wake alikuwa rafiki wa watu wengi tukiwamo sisi viongozi wa Serikali. Na alikuwa na mchango mkubwa kwenye kukuza na kuibua vipaji vya wasanii wakiwamo ambao tunawasikia sasa.

“Alikuwa mdau mkubwa wa afya na alishirikiana nasi katika kampeni mbalimbali za wizara kwa lengo la kuifikia jamii, kwa kweli tutamkumbuka Ruge kwa wema wake, Mungu ailaze roho yake mahali pema amina,” alisema Dk. Ndugulile.

KABAKA

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudentia Kabaka, alisema msiba wa Ruge ni pigo kwa familia kwani hata CCM itamkumbuka kwa michango yake ikiwamo namna alivyoipenda nchi yake wakati wote.

Alisema alikuwa akishirikiana na Watanzania wengi ikiwamo kuibua vipaji na kuwa mdau mkubwa katika tasnia ya habari nchini.

“Ninachoweza kusema kwa kweli Ruge kila siku nilikuwa nikimwombea nikiwa na imani atapona, lakini mapenzi ya Mungu hatuna budi kuyapokea. Kwa kweli Ruge ‘tutam-misi’ sana kwa uchangamfu wake na kuipenda nchi yake,” alisema Kabaka.

NAPE

Katika akaunti yake Twitter, muda mfupi baada ya taarifa ya kifo cha Ruge, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), aliandika; “Pumzika kwa amani kaka! Huna mfano wako duniani, maisha yako yameacha alama kubwa, utaishi milele kwa wema wako! Ndugu, rafiki na mzalendo wa kweli!”

NIKKI WA PILI

Kutokana na msiba huo msanii wa muziki wa kizazi kipya Nikki wa Pili aliandika “R.I.P master/teacher/genius/philosopher/ writer/ visionary/leader/midas touch… Pumzika Mutahaba.”

MCHUNGAJI MSIGWA

Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa kupitia akaunti yake ya Twitter aliandika: “Haijalishi mwanadamu anakufa kifo cha namna gani, lililo la mhimu ni namna alivyoishi. Kifo ni tendo la muda mfupi sana. Ni mjinga tu anaweza kupuuza mchango wako kwenye tasnia ya habari! R I P Ruge.”

MATIBABU MIL 5/- KWA SIKU

Februari 18, mwaka huu ndugu wa Ruge waliomba msaada wa fedha kulipia gharama za matibabu yake.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha Clouds, Mbaki Mutahaba ambaye ni kaka wa mkurugenzi huyo, alisema Ruge anapatiwa matibabu Afrika Kusini ambako kwa siku gharama ni Sh milioni 5.

“Alianza kuumwa mwaka 2018, alilazwa katika Hospitali ya Kairuki kisha akapelekwa India, ‘sapoti’ ni kubwa tunashukuru na hata Rais Dk. John Magufuli ametoa mchango na anaendelea.

“Ana figo ambayo haipo sawasawa, ilikuwa lazima wambadilishe. Madaktari wa Hospitali ya Kairuki na Muhimbili wakashauri apelekwe Afrika Kusini maana ni karibu zaidi, lakini gharama ni kubwa.

“Kule (Afrika Kusini) mfumo wao wa malipo ni tofauti, unapaswa kulipa fedha taslimu. Kuna namba rasmi imeandikishwa kwa jina la mdogo wetu Kemilembe Mutahaba, unaweza kutusaidia kwa namba hiyo ni  0752 222210,” alisema.

JPM ATOA DOLA 20,000

Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alitoa Dola za Marekani 20,000 ambazo ni wastani wa Sh milioni 50 ili kuchangia matibabu ya Ruge.

Akizungumza katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, mmoja wa wafanyakazi wa Clouds Media, Sebastian Maganga, alisema hatua hiyo ya Rais Magufuli imefikiwa baada ya kusikia taarifa kuwa Ruge anaumwa kwa muda na zilimsikitisha.

“Aliamua kumshika mkono kama baba afanyavyo kwa mwana wa kumzaa, kumshirikisha katika maombi na alinyoosha mkono kwetu akituambia changamoto za kiafya ni kubwa na la awali ambalo anataka kulifanya ni kuchangia mfuko wa kiafya na changamoto zisiwe gharama za kimatibabu,” alisema Maganga.

Mbali na Rais Magufuli kutoa mchango wa matibabu, pia Maganga alibainisha kuwa wameamua kuweka wazi juu ya afya ya Ruge kutokana na kuwepo kwa maneno mengi katika mitandao ya kijamii.

“Yalizungumzwa mengi na sisi tuliona wakati haukuwa mzuri sana kuzungumza na tuliona tukifanya yoyote tutaleta maswali mengi ambayo hata yeye hakupenda.

“Katikati ya Mei kuelekea Juni hali ya Mkurugenzi haikuwa nzuri, akatuomba kupata muda kidogo ili ashughulikie afya yake, tuliona hili litakuwa dogo tu na tukatoa baraka zote.

“Lakini ripoti za kitabibu zikasema muda wa kupumzika ni mdogo, hivyo akaongezewa muda na katikati ya Juni na Julai alirejea na kasi ya kawaida kwenye kazi na wiki mbili tatu tukawa naye na hapo ndiyo tulikuwa tunakaribia kuanza Tigo Fiesta Moro.

“Akatuambia anabidi aelekee kwenye taratibu za kimatibabu na nikiri bado changamoto hizo zipo na madaktari wanakiri kiongozi wetu ni mpambanaji na bado anahitaji muda wa kupumzika na ni kweli hizo changamoto zilikuwepo.

“Tunashukuru mara nyingi ukipata changamoto A ya kiafya changamoto B inajitokeza na tunashukuru taratibu hali yake inarudi na kuna hatua kubwa ya kimaendeleo,” alisema Maganga.

MZAZI MWENZIE AZUNGUMZA

Februari 21, mwaka huu mtangazaji maarufu nchini, Zamaradi Mketema, alisema kuwa Babu Tale ndiye alimkutanisha kwa mara ya kwanza na Ruge.

Zamaradi ambaye ni mzazi mwenzie na Ruge aliyezaa naye watoto wawili; Juju na Shuby, aliyasema hayo katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Clouds.

Kipindi hicho kwa siku kadhaa kilikuwa kikiwaita watu mbalimbali walio na mahusiano ya karibu na Ruge wakati akiwa Afrika Kusini kwa matibabu.

Akisimulia jinsi walivyokutana kwa mara ya kwanza, Zamaradi alisema ilitokea baada ya Babu Tale ambaye ni meneja wa msanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ kumuona akiwa anatangaza kituo cha televisheni cha C2C na kumtambua ana kipaji ambacho anatakiwa awe sehemu nyingine watu wakione zaidi.

“Nakumbuka siku hiyo Babu Tale alinipa namba ya Ruge nimtafute na akaniambia nisiseme kama ni yeye kanipa na mwisho wa siku tukaonana, nikamweleza nia ya kwenda kufanya kazi Clouds,” alisema Zamaradi

Akielezea namna walivyoingia kwenye mahusiano naye, alisema ilitokea tu kama binadamu japokuwa alikiri ilikuwa kazi ngumu kumkubalia kwa kuwa alikuwa amejiwekea malengo yake.

Zamaradi alisema mwisho wa siku walijikuta wakikubaliana na ikatokea hivyo wakazaahadi watoto wawili.

Kuhusu watoto kujua kama baba yao anaumwa, alisema wanajua na walishaenda kumuona Afrika Kusini.

Akizungumzia Ruge kuwa ni baba wa aina gani, alisema anashukuru ni mtu ambaye anatekeleza wajibu wake kwa watoto na pia amekuwa akipata muda huenda kushiriki shughuli mbalimbali za shuleni kwao.

DK. MENGI KUCHANGIA MATIBABU

Februari 23, mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile, alisema Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi yuko tayari kuchangia matibabu ya Ruge.

 Mhavile alitoa ahadi hiyo katika mahojiano maalumu na Kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds Tv.


Alisema tayari alimpa taarifa Dk. Mengi kuhusu kuugua kwa Ruge na ameahidi kumsaidia pindi kamati maalumu iliyoundwa kukusanya michango itakapokamilisha taratibu.

“IPP media inaungana na familia na ndugu jamaa na marafiki kuchangia fedha kwa ajili ya matibabu ya Ruge ili asimame tena. IPP ipo tayari kumchangia Ruge baada ya kumati kutoa maelekezo ya nini kifanyike,” alisema Mhavile.

Alisema taarifa za kuugua kwa Ruge alizipata mwaka jana akiwa India na alipomwona, alimpa pole na anaamini Ruge atapona na kuendelea na majukumu ya kujenga taifa.

HISTORIA YA RUGE

Ruge Mutahaba alizaliwa mwaka 1970 huko Brooklyn, New York nchini Marekani.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Arusha kuanzia darasa la kwanza hadi la sita kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Mlimani, Dar es Salaam kukamilisha elimu yake ya msingi.

Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam kwa masomo ya awali ya sekondari na kisha masomo ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha San Jose nchini Marekani kusomea shahada za kwanza katika masoko na fedha.

Wakati akiendelea na masomo nchini Marekani, bosi mwenzake katika CMG, Joseph Kusaga alikuwa akiendesha Klabu ya Disko la Usiku (Night Club Disco), ambayo pia ilijulikana kama Clouds Disco.

Hivyo, Ruge akawa mgavi pekee wa vifaa vya kuendeshea klabu hiyo ya usiku, yaani akiifanya kazi hiyo akiwa nchini Marekani.

Wakati aliporudi Tanzania baada ya kukamilisha masomo yake ya chuo kikuu, aliunganisha nguvu na Kusaga kuanzisha CMG wakati huo ikiwa katika Jiji la Arusha.

CMG hulenga kuchochea na kuwezesha vijana wa Kitanzania chini ya miaka 35 kupata fursa zitakazowawezesha na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa lao.

Ruge hajaoa rasmi, lakini alikuwa akiishi na Zamaradi Mketema na wana watoto wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles