KWAHERI NDESA PESA

0
926

*Maelfu wamuaga, Gwajima aliamsha ‘dude’ msibani

*Moshi yazizima, viongozi wa Serikali waingia mitini


Na WAANDISHI WETU-MOSHI

NI simanzi. Ndivyo unaweza kusema baada ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, hasa mji wa Moshi na miji ya jirani kufurika katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini, marehemu Philemon Ndesamburo (82).

Tukio hilo la kuaga mwili wa Ndesamburo maarufu kama Ndesa Pesa, lilifanyika jana mjini hapa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, huku maduka na shughuli za kijamii zikisimama kutwa.

Kusitishwa kwa shughuli hizo kulitokana na msiba huo mzito wa Ndesamburo.

Mwili wa marehemu uliagwa katika Uwanja wa Majengo mjini hapa, huku jeneza lake likibebwa katika gari maalumu mithili ya Mfalme.

Ndesamburo, mmoja wa waasisi wa Chadema aliyeliongoza Jimbo la Moshi Mjini kwa miaka 15 akiwa mbunge, alifariki ghafla wiki iliyopita katika Hospitali ya KCMC ambako alikimbizwa kwa matibabu baada ya kuanguka ofisini kwake.

Mwili wa mwanasiasa huyo nguli uliokuwa umehifadhiwa KCMC, ulisafirishwa hadi Uwanja wa Majengo mjini hapa kwa kuagwa na wananchi na leo unatarajiwa kuhifadhiwa nyumbani kwake eneo la Kiboriloni.

 

MAELFU WAJIPANGA

Kuhudumu kwa miaka 15 kwenye ubunge alioamua kustaafu mwaka 2015, kisha kugombea uenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, kulisababisha maelfu ya wananchi wa mji wa Moshi kusimama barabarani kuaga mwili wake.

Mamia ya watu walisimama barabarani maeneo ya kona ya kuingilia KCMC, Longuo, Madukani, Chuo cha Ushirika Moshi, mzunguko wa YMCA na maeneo mengine kuelekea Uwanja wa Majengo kupitia Kituo cha Polisi.

Kutokana na kuguswa na maisha ya Ndesa Pesa, baadhi ya vijana wakiwa katika makundi na pikipiki zaidi ya 500, waliamua kuusindikiza mwili huo huku wengine wakilazimika kutembea kwa miguu hadi Uwanja wa Majengo.

Wingi wa magari ya msafara na pikipiki, zilisababisha mji wa Moshi kuelemewa, hivyo baadhi ya magari ya abiria na watu wengine kushindwa kufika maeneo waliyokuwa wakienda kwa wakati.

 

UWANJANI

Kutokana na mazingira ya tukio la kuaga mwili wa Ndesamburo kugubikwa na sintofahamu baada ya Serikali kuhamisha shughuli za kuaga kutoka Uwanja wa Mashujaa hadi Majengo, baadhi ya wananchi waliamua kukesha Uwanja wa Majengo ili kuulinda.

Mamia ya wananchi walianza kuingia uwanjani hapo jana saa 12 asubuhi na hadi msafara wa magari zaidi ya 100 yakiongozwa na gari lililobeba jeneza la mwili wa Ndesa linawasili uwanjani hapo, tayari uwanja ulikuwa umefurika.

 

VIONGOZI

Viongozi waliofika uwanjani hapo jana ni Mwasisi wa Chadema, mzee Edwin Mtei, Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, Makamu Mwenyekiti Bara, Professa Abdallah Safari, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar,  Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara,  John Mnyika na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,  James Mbatia.

 

LOWASSA NDANI YA GWANDA

Wengine waliofika uwanjani hapo ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakiongozwa na mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa ambaye jana kwa mara ya kwanza alionekana hadharani akiwa katika magwanda meusi ambayo huvaliwa kama sare ya chama hicho.

Kwa muda wote Lowassa hakuwahi kuonekana akiwa katika gwanda hata alipokuwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Wengine ni John Heche, Mbunge wa Mikumi Joseph Haule, Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel, Mbunge wa Rombo Joseph Selasini, Halima Mdee, Ester Bulaya na Joshua Nassari.

Hata hivyo, viongozi walioingia na kushangiliwa ni pamoja na Lowassa, Godbless Lema, Mdee, Bulaya na Mchungaji Peter Msigwa.

 

MWILI KUWASILI

Mara baada ya kuwasili kwa jeneza uwanjani hapo, lilipokewa na kubebwa na madiwani wa Chadema Manispaa ya Moshi na  halmashauri nyingine za Mkoa wa Kilimanjaro.

Kisha jeneza hilo liliwekewa joho kama heshima kutoka kwa wahitimu wenzake wa Sahahada ya Uzamivu waliotunukiwa Desemba 17 mwaka jana na Chuo cha Japan Bible School.

Ilikuwa ni Saa 6:38 mchana, gari namba T. 830 DEW aina ya Toyota VX, likiwa limebeba mwili wa Dk. Ndesamburo lilipoamsha vilio na mayowe, huku nyuma ya gari hilo kukiwa na wanafamilia akiwamo mke, watoto, wajukuu na ndugu zake.

Baada ya kufika uwanjani, wabunge wa Chadema wakiongozwa na Joseph Haule na  Dk. Mollel, walibeba jeneza lenye mwili wa marehemu hadi katika eneo maalumu lililotengwa kwa ibada.

Baada ya kuwasili katika eneo hilo, ibada fupi iliongozwa na Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.

 

MBOWE

Akizungumza uwanjani hapo, Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisema: "Sina hakika nizungumze nini kwani jambo hili kwetu ni gumu sana kulizoea, utahitaji muda mwingi sana kumwelezea Ndesamburo ni nani, unaweza kumaliza hata siku nzima au wiki nzima, ni baraka tosha huyu mzee si wa kawaida.

“Inafika mahali tunapita hakuna mahali pa kulala kwa sababu wote wenye nyumba za kulala ni watu ambao pengine ni wa chama kingine, chama kile au pengine ni watu wao wanatunyima mahali pa kulala, tumelala kwenye magari na Ndesamburo mara nyingi kwa kunyimwa mahali pa kupumzika tukiwa katika harakati za kisiasa,” alisema.

 

WANYIMWA BENDI YA POLISI

Akizungumzia magumu waliyokutana nayo katika msiba huo, Mbowe alisema ni pamoja na kunyimwa uwanja na bendi ya polisi.

“Kwanza tuliamini kwa tukio hili la kihistoria ni vema mzee wetu tungemsindikiza kwa ‘Brass Band ya Polisi’, tukaenda Chuo cha Polisi Moshi ambacho Mzee Ndesamburo amewafanyia mambo mbalimbali.

“Brass Band hiyo hukodishwa kwa Sh 300,000 na kama wafiwa tayari tulishajiandaa kulipia gharama hizo.

“Wanaogopa kutoa Brass Band, wananiambia niongee na IGP, yaani Mbowe nimpigie IGP simu kumuomba Brass Band, mimi?

“Band hii hukodishwa kwenye Send off za maharusi eti leo polisi wanaogopa hata kufanya kazi kwa sababu hawajui bwana mkubwa atafurahi ama atakasirika.

“Tukahitaji kiwanja tukiamini kwamba Majengo si kwamba hapakuwa panafaa bali tuliamini historia ya Moshi, Uwanja wa Mashujaa kama unavyoitwa unastahili kuwa uwanja wa kumuaga Mzee Ndesamburo, polisi wameweka vigingi,” alisema.

 

LOWASSA

Kwa upande wake, Lowassa, alisema zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kudidimiza demokrasia kwa kujengea Watanzania uongo, huku akisisitiza kwamba wataendelea kusimamia haki na sheria katika kufanya siasa za mageuzi.

 “Nampongeza sana mzee wangu, Edwin Mtei kwa kuanzisha chama hiki kikuu cha upinzani chenye nguvu kubwa hapa nchini, hivyo tutaendeleza jitihada zilizofanywa na waasisi hao katika kuhakikisha uchaguzi mkuu kinashika dola,” alisema Lowassa.

 

SUMAYE

Naye Sumaye ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, katika hotuba yake alisema kuondokewa na Dk. Ndesamburo ambaye ni mwasisi, ni pigo kubwa kwa Chadema na kwamba watayaendeleza yale yote aliyoanzisha ili kuleta ukombozi na kufikia malengo ya kuiongoza nchi ifikapo mwaka 2020.

“Mzee Ndesamburo ameondoka, lakini mbegu aliyoipanda itaendelea kustawi na waliodhani kwamba kutakuwa na anguko wataaibika kwani Chadema ni chama imara,” alisema Sumaye.

 

MTEI ATOA NENO

Akimzungumzia marehemu, mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, alisema kwa miaka mingi walishirikiana na Ndesamburo kuijenga Chadema tangu chama hicho kikiwa hakina mwanachama hata mmoja, hatua iliyowawezesa kupata wanachama nchi nzima.

“Namshukuru sana Mwenyekiti wetu na kijana wangu, Freeman Mbowe kwa ushujaa wake, lakini pia Lucy Owenya na wanafamilia wote nawapeni pole Mungu awasaidie, awaimarishe ili muweze kuendeleza hii familia,” alisema Mzee Mtei.

 

GOLUGWA

Akizungumza uwanjani hapo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, aliwalaani wale wote wenye chuki na roho mbaya iliyolenga kuzuia tukio la kuagwa kwa mwasisi huyo.

“Maadui wote waliopanga kuvuruga tukio hili walegee na washindwe kwa Jina la Yesu na mawakala wao waliopo hapa duniani nao washindwe,” alisema Golugwa.

 

RC AINGIA MITINI

Katika hali ya kushangaza, viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro hawakuonekana uwanjani hapo zaidi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kilimanjaro,  Ester Mmasi (CCM).

Kushindwa kutokea kwa viongozi hao wa Serikali na chama tawala kumeendelea kuwaacha wananchi katika mshangao mkubwa, kwani hata uwanjani hapo kiti alichokuwa ameandaliwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mrisho Gambo kiliendelea kuwa wazi.

 

GWAJIMA ALIAMSHA DUDE MSIBANI

Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amelazimika ‘kuliamsha dude’ msibani kwa kutoa kile alichokiita matibabu ya kulaani vitendo vya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania na kuingiza siasa kwenye misiba.

Gwajima aliyewasili uwanjani hapo na kupokewa kwa shangwe, alitoa kauli hiyo baada ya kupewa nafasi ya kusalimia kama mmoja wa viongozi wa dini.

“Kwanza naomba nikusahihishe, mimi si kiongozi wa dini, kiongozi wa dini huwa anazungumza na watu wake tu. Mimi ni kiongozi wa kiroho, nazungumza na watu wote wenye roho.

“Sitazungumza mambo mengi leo (jana), lakini napenda kuanza kwa kutoa matibabu misibani hasa kwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambayo hivi karibuni imekumbwa na misiba,” alisema Gwajima.

Alisema ameshangazwa na kitendo cha Serikali chini ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gambo kuzuia kuagwa mwili wa Ndesamburo katika Uwanja wa Mashujaa kwa kisingizio cha shughuli za kiserikali ikiwamo mahakama na shule.

“Niliposikia hizi taarifa nilishangaa sana, nimewahi kufanya mkutano pale kuanzia mchana. Hivi vyombo vilivyofungwa hapa vina namna yake ya kufunga sauti isiweze kwenda mbali wala kuwa na usumbufu kwa watu wengine.

“Hii tabia ya kuingia siasa kwenye misiba tumeiona hata kule Arusha wakati wa kuaga miili ya watoto wetu, eti mbunge wa jimbo lililopatwa na msiba hakupewa nafasi ya kuzugumza kabisa.

“Hii sasa ni tabia inaonekana kuota mizizi. Ikiwa ni yeye ndiyo anafanya mambo haya namwambia hatoi taswira nzuri kwa jamii wala taifa. Nimwombe Rais Dk. John Magufuli kumchukulia hatua za haraka Gambo kwa kitendo cha kuingiza siasa kwenye misiba,” alisema Gwajima.

Alisema yeye kama kiongozi wa kiroho, alitumia nafasi hiyo kuitibu Moshi kwa kutoa matibabu ya dakika chache, huku akitaka kutoambiwa kwa nini amefanya hivyo.

 “Nilipata taarifa za msiba, lakini nikasikia ama kiongozi mmoja anayeongozwa na kiongozi mwingine, lakini tetesi tetesi nasikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa maelekezo kuwa haiwezekani kutumia Uwanja wa Mashujaa.

“Ni mtu (Gambo) watu walimshirikisha kuanzia mwanzo, hajawazuia, wamefanya shughuli zote, kwenye hatua za mwisho ikiwa ni yeye (Gambo) kama ambavyo wanasema, basi nasema jambo alilolifanya halifai na akome, aache mambo ya siasa kwenye misiba,” alisema Gwajima.

 

CUF WAFUNGUKA

Akizungumza baada ya ibada hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Severine Mwijage, alikemea vikali siasa za chuki akisema zitaliangamiza taifa katika siku zijazo.

“Siasa zinazopandikizwa kwa watu ni siasa mbaya, hivi tungeamua kuingia pale Mashujaa wasingetuzuia,” alisema Mwijage.

 

ZITTO

Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, aliitaka Manispaa ya Moshi kutafuta kitu chochote kitakachopewa jina la Ndesamburo kama heshima ya kuendelea kumuenzi.

“Marehemu alikuwa ni zaidi ya jabali, hakuna maneno bora ya kumwelezea mzee wetu, umati huu unaonyehsa mapenzi makubwa kwa watu wake aliowawakilisha bungeni. Hakika alikuwa mbunge wa watu. Funzo kubwa hapa ni kwamba duniani ukifanya kazi ya watu, watu watakusindikiza kwa heshima.

“Tuweke kumbukumbu ili ijulikane Tanzania aliwahi kutokea jabali la demokrasia ya vyama vingi. Manispaa ya Moshi watafute mtaa ulio bora, ikiwezekana waupe jina la Dk. Ndesamburo ili kumuenzi, lazima tumuenzi kwa kuenzi demokrasia,” alisema Zitto.

 

MBATIA

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi, James Mbatia, alisema wanamageuzi wote waliohudhuria watakutana mjini Moshi kumuenzi Dk. Ndesamburo.

 

MEYA MOSHI

Akizungumza uwanjani hapo,  Meya wa Manispaa ya Moshi,  Raymond Mboya, aliwataka madiwani wa Moshi Mjini kuanza mchakato katika vikao wa kubadilisha jina la Uwanja wa Majengo na kuupatia jina la Ndesamburo ili iwe kumbukumbu ya kuthamini mchango wake katika jamii.

“Limetoka wazo hapa la kuenzi jina la mzee wetu, sioni kama ni heshima, mitaa mingi tunayo ina majina mpaka ya ambao si viongozi, alivyofanya Gambo amefungua macho, nawaagiza madiwani wafanye mchakato wabadili jina la uwanja huu uitwe Ndesamburo na kama Gambo ana uwezo wa kulipinga aje kupinga,” alisema Mboya.

 

Habari hii imeandaliwa na JANETH MUSHI, UPENDO MOSHI, SAFINA SARWAT NA ELIYA MBONEA (MOSHI)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here