ANDREW MSECHU na PATRICIA KIMELEMETA –dar es salaam
MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi (75), amefariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa Dubai alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hadi jana jioni, familia ya bilionea huyo ilikuwa haijaeleza kwa undani kilichokuwa kikimsumbua, badala yake walisema vikao vinaendelea na vikiisha taarifa rasmi itatolewa.
Taarifa za kufariki dunia Mengi, zilianza kusikika jana asubuhi na baadaye taarifa iliyotolewa na kituo chake cha televisheni – Independent Television (ITV) ilithibitisha.
Maandalizi ya mazishi ya mfanyabiashara huyo maarufu ndani na nje ya Tanzania, yameendelea nyumbani kwake Ada Estate, Kinondoni ambako tangu jana asubuhi wanafamilia, ndugu na jamaa walikuwa wakifika kutoa pole.
MTANZANIA lilishuhudia baadhi ya ndugu na wanafamilia wakiwasili nyumbani hapo kuanzia asubuhi huku shughuli mbalimbali za kuweka mazingira sawa zikiendelea.
MBOWE AZUNGUMZIA MSIBA
Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema yeye ni mmoja wa wanafamilia kwa kuwa Mengi ni ndugu yake na wanatokea katika eneo moja.
Alisema amepokea taarifa za kifo cha mzee Mengi kwa mshtuko mkubwa, hasa ukizingatia alikuwa mtu muhimu kwa jamii zote za Watanzania, baba na rafiki wa faida.
“Mengi alikuwa mtu mwenye sifa za pekee, alikuwa rafiki wa watu wote, alikuwa rafiki wa wenye dini na wasio na dini, alikuwa rafiki wa walemavu, alikuwa rafiki wa wafanyabiashara na wawekezaji. Kwa watu wa makundi yote kila mtu anajua namna alivyoguswa naye.
“Nawapa pole wanafamilia wote na wafanyakazi wote wa kampuni zake. Ni kweli mzee Mengi aliwagusa wengi, kifo chake ni pengo na hasara kubwa kwa taifa,” alisema.
Mbowe alisema hilo litadhihirika na kujiweka wazi baada ya kuondoka kwake, kwa kuwa itachukua miaka mingi kupata mtu wa aina yake.
Alisema pamoja na kifo chake, ni jambo jema kuendelea kumshukuru Mungu kuwa alimleta mtu wa aina ya Mengi, aliweka sifa ya pekee ndani yake, hivyo kumfanya mtu wa kipekee.
Mbowe alisema pamoja na kugusa maisha ya watu wengi, Mengi alikuwa mtu muhimu katika uwekezaji na biashara, pia mlezi wa vyombo vya habari, sehemu ambayo alifanya uwekezaji mkubwa.
“Mengi alikuwa mwekezaji mwenye mchango mkubwa nchini na alikuwa akiendelea kupanua uwekezaji wake,” alisema.
Mbowe alisema yeye akiwa miongoni mwa wanafamilia, wanaendelea na vikao kwa maandalizi ya awali kuangalia namna mwili wa Mengi utakavyowasili nchini kutokea Dubai, hadi utakavyohifadhiwa.
Alisema msiba huo pia unawagusa watu wa Jimbo la Hai, hivyo alitoa salamu za rambirambi kwao kwa kuwa nao ni sehemu ya watu waliokuwa wakisaidiwa kwa kiasi kikubwa na marehemu Mengi.
“Kwangu marehemu ni ndugu yangu pia, na ni mtu wangu katika familia, ninatoa salamu za rambirambi kwani watu wote wa Jimbo la Hai kwa kuwa nao wanaguswa moja kwa moja na mtu wa muhimu kwao,” alisema Mbowe.
WAFANYAKAZI WA IPP
Mara baada ya kutolewa taarifa za msiba wa Mengi, hali ya huzuni ilitawala katika ofisi za IPP, ikiwemo zile za ITV na The Guardian Tanzania Limited.
Wafanyakazi wa kampuni hizo walionekana kukaa katika vikundi kujadili msiba huo huku wakishindwa kujua cha kufanya.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi ambao hawakupenda kutajwa majina yao, walisema wanasubiri taarifa za familia ya mzee Mengi ili waweze kujua taratibu za mazishi na mahali atakapozikwa.
“Tumesikitishwa sana na kifo cha mzee wetu Mengi, kwa sababu alikuwa kiongozi mahiri na aliyeweza kusikiliza kero za wafanyakazi wake, kwa sasa hatuwezi kuzungumza lolote kwa sababu sisi sio wasemaji wa familia, ila tunasubiri taratibu za mazishi ili tujue atazikwa lini na wapi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Alisema licha ya Mengi kuwa karibu na wafanyakazi wake, alikuwa na utaratibu wa kushirikisha waandishi wa kampuni yake wakati alipokuwa akifanya shughuli mbalimbali za kijamii zikiwamo za kuwafanyia sherehe walemavu pamoja na kutoa tuzo.
“Katika shughuli hizo, aliwataka wafanyakazi kuwa karibu na matukio yote ili waweze kuona umuhimu wa kuwasaidia jamii,” alisema.