24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri Maalim, ‘tutazimis’ siasa za kibabe zenye vionjo vya utu

Na Hassan Daudi


Taarifarifaa kifo cha Maalim Seif zimeniacha kinywa wazi. Ni kama ambavyo ingemshitua mfuatiliaji yeyote wa siasa za Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Angalikuwa ni kiongozi wa dini, basi angekuwa ameacha alama kwa mafundisho yake aidha kwenye madhahabu ya kanisa au mimbari ya msikiti.

Kwa kuwa hakuwa upande huo, basi itoshe kusema tutamkumbuka kwa dhima yake kubwa katika ulingo wa siasa za nchi hii. Ndiyo, huko ndiko ulikolowea na kujizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania (Visiwani na Bara).

Maalim Seif Sharif Hamad enzi za uhai wake.

Katika uwanja huo wa siasa, Maalim ameondoka akiwa ameacha alama isiyofutika, hasa kwa namna ulivyojipambanua kuwa ni mwanasiasa mwenye sura mbili tofauti lakini zenye mvuto wa aina yake.

Mosi, machoni mwa wengi alitafsiriwa kuwa ni mfuasi wa siasa za kibabe na kuna wakati wakosoaji wake walimvika jina la dikteta. Uzuri ni kwamba hilo la udikteta halikuweza kuthibitika kwa namna yoyote ile hadi zinaibuka taarifa za kifo chake.

Bila shaka nitaeleweka zaidi nikitolea mfano namna macho yalivyokuwa yakimtoka kila ulipopata wasaa wa kuzungumzia suala la Muungano. Mara zote alisema wazi, kwamba havutiwi nao.

Niwe muwazi tu, kwamba misimamo yake juu ya ‘ishu’ hiyo ilifanya kuonekana mtu hatari, hata wengine kuhisi ungevunja Muungano endapo ungepata nafasi ya kuwa Rais wa Zanzibar.

Huenda hilo nalo lilichangia kwa kiasi fulani kumuweka mbali na mlango wa Ikulu?

Ukiacha hilo, hata namna ulivyoliendea suala la mgogoro wake na ‘swahiba’ Prof. Ibrahim Lipumba na hatimaye akang’atuka CUF, lilitafsiriwa kuwa ni sehemu tu ya misingi yake ya kutoyumbishwa katika kile unachokiamini. Hapo pia ikaja taswira yake ya ubabe.
Tuiache taswira hiyo…

Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad

Pili, pasi na kupishana na taswira ya siasa za kibabe, pia wengine tuliziona ni zenye kuheshimu misingi ya utu na kutanguliza masilahi mapana ya watu waliokuwa wakimfuata nyuma.

Unajua kwanini nimesema hivyo?

Kutokana na ushawishi mkubwa uliokuwanao Zanzibar, Maalim alikuwa na jeuri ya kusababisha matukio ya umwagaji damu Visiwani humo katika kila kipindi cha Uchaguzi Mkuu. Hilo nalo linahitaji ushahidi?

Sitakosea nikisema wafuasi wake, hasa kule Pemba, walikuwa tayari kwa lolote, nikimaanisha machafuko, kila matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa na kuipa ushindi CCM.

Hapo ndipo taswira ya utu kwa Maalim ilipokuwa ikijipambanua wazi kwa namna alivyokuwa mstari wa mbele kuhimiza utulivu kwa wafuasi wake, busara zilizoendelea kuilinda amani ya Zanzibar kwa vipindi vingi vya uchaguzi.

Kama Maalim angetawaliwa zaidi na taswira ya siasa za kibabe, ni jambo lisilofikirika juu ya ambacho kingekuwa kimeikuta Zanzibar miaka mingi iliyopita. Itoshe kusema kwaheri Maalim, tutazimis sana siasa zako za kibabe lakini zilizotawaliwa na utu…

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ni ubabe wa Maalim au wa wale walioiba kura na kuwaua raia wasio na hatia? Acha unafiki

    Unafiki mwengine ni serikali kutotaja ugonjwa uliomchukua. Siri ya nini?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles