Kwaheri Krismasi, karibu mwaka mpya na majukumu mapya

0
1242

Na ANDREW MSECHU

WAKATI tukielekea kumaliza mwaka, wengi walielekeza nguvu katika kuhakikisha sikukuu za mwisho wa mwaka, Krismasi na Mwaka Mpya zinafana.

Sikukuu ya Krismasi imeshamalizika, kwa wale wenye desturi ya kusafiri na kwenda kusherehekea sikukuu hii kwao, wameanza kurejea mijini. Wengine wanaendelea kusubiri kupokea mwaka mpya huko waliko.

Sherehe ya mwaka mpya haina mbwembwe kama ilivyo ile ya Krismasi, lakini ina alama muhimu ya kurejea majukumu ambayo kidogo yaliwekwa kando kwa mwezi wa Desemba, ili kupisha ujio wa Krismasi na mwaka mpya.

Kwa kuanza kwa mwaka mpya, majukumu yalioyowekwa kando yanarejea pale pale, kwa kuwa kuanza kwa mwaka kunachochea kuendelea kwa maisha, katika sura mpya.

Januari inakuja na ndiyo mwezi ambao miongoni mwa mambo muhimu ni kufunguliwa kwa shule na vyuo ambavyo vilifungwa kwa ajili ya kukamilisha mwaka na kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kuanza kwa mwaka mpya kunaendeleza majukumu ya wanafunzi shuleni na vyuoni, kunarejesha majukumu ya wazazi kuhakikisha wanafunzi wanarejea masomoni wakiwa wameandaliwa vyema kumudu maisha ya shule na vyuo.

Ni wakati mwingine wa wazazi na walezi kusahau kuhusu majukumu ya sikukuu ambazo tayari zinayoyoma, kurejea katika majukumu ya kulipa ada kwa wakati na kuandaa vifaa kwa ajili ya watoto na vijana wanaorudi shule na vyuoni.

Kwa kuwa wengi miongoni mwao wameona kuwa shule za Serikali ambazo wanataja kutoa ‘elimu bure’ ni gharama, kwa kupeleka watoto katika shule binafsi na zile zinazoitwa za kimataifa au ‘English medium’ zinazotoa mahitaji yote muhimu kwa wanafunzi, sasa wakati ni huu, kuandaa mazingira ya kulipa ada kwa wakati.

Ni kwa mukhtadha huu kwamba, elimu ina gharama zake, kwa wanaotambua gharama ya elimu ya bure, wanatambua pia adha ya elimu ya kulipia gharama kubwa, ndiyo maana walichukua uamuzi huo mapema, ili kuepuke ‘gharama ya elimu bure’ ambayo inaonekana kuwa kubwa, kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa mfumo wa elimu katika shule za Serikali.

Ni wazo langu katika kuuaga mwaka na kuuanza mwaka mpya, kwamba jukumu la sherehe na maadhimisho ya Krismasi na mwaka mpya limemalizika, tuyapokee vyema kwa uhakika majukumu ya Januari, hasa kwa kuhakikisha watoto wanarejea shule na vyuoni, wakiwa na uhakika wa maisha katika kipindi cha mwanzo wa mwaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here