25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri Ben

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KIFO cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kimeshtua na kuumiza wengi ndani na nje ya nchi.

Taarifa za kifo cha Mkapa zilitangazwa na Rais Dk. John Magufuli usiku wa kuamkia jana pasipo kusoma mahala popote tofauti na ilivyokuwa wakati Taifa lilipopata misiba mingine kama ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine. 

Taarifa hizo ambazo Rais Magufuli alizitoa saa 6:25 usiku na kusambaa mara moja, hazikueleza sababu cha kifo cha Mkapa zaidi akisema taarifa nyingine zitaendelea kutolewa.

Rais Magufuli alisema Mkapa alifariki dunia akiwa amelazwa katika hospitali ambayo pia hakuitaja.

Viongozi ndani na nje ya nchi na watu wa kada mbalimbali  wameonekana kushtushwa na kifo hicho  hasa kutokana na Mkapa kuonekana kwenye vikao vya CCM, Dodoma zaidi ya wiki moja iliyopita akiwa mwenye afya njema.

Mkapa ambaye kabla ya kuwa Rais wa Tanzania  kati ya mwaka 1995 -2005, na hapo kabla Balozi na Waziri wa Mambo ya Nje, katika tawala za Nyerere na  Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, amefariki dunia huku akiwa ameandika historia yenye urithi nyuma yake.

Urithi huo amejaribu pia yeye mwenyewe kuuhifadhi au kuelezea kupitia maandishi aliyoyaweka kwenye kitabu chake cha My Life, My Purpose (Maisha yangu, Kusudi Langu) alichokizundua Novemba 12, 2019.

Katika kitabu hicho ambacho tangu akizindue imepita miezi nane sasa, Mkapa ambaye ana miaka 81 akiwa amezaliwa mwaka 1938  mbali na kuelezea historia ya maisha yake, ameelezea pia namna alivyoingia kwenye urais, mambo aliyoyafanya, mazuri, makosa, anayojutia lakini zaidi yale ambayo hakuyafanya  na anayotamani yafanyike na ametoa ushauri. 

Pamoja na yale aliyoyaweka kwenye kitabu hicho, Mkapa ambaye anatambulika kwa kauli mbiu yake ya ‘Ukweli na uwazi na Mtaji wa Maskini ni Nguvu zake Mwenyewe’ wengi wanamkumbuka kwa kufanya mageuzi makubwa ya sera ambazo zilibadilisha uchumi wa nchi.

Mkapa ambaye mwaka 1995 wakati akiingia madarakani akiwa na ndoto ya kuinua uchumi na kurudisha misaada iliyopotea, anakumbukwa kwa kujenga mifumo na kufanya mageuzi makubwa.

Miongoni mwa mifumo iliyowekwa chini ya utawala wa Mkapa ni ule pamoja na ulipaji kodi.

TAASISI ALIZOUNDA

Chini ya utawala wake ilianzishwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa sheria ya Bunge Na.11 ya mwaka 1995, ambayo ilianza kufanya kazi katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi yaani Julai 1,1996. 

Katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria, TRA iliwekewa meno, ikipewa jukumu la kusimamia kwa uadilifu kodi mbalimbali za Serikali Kuu.

Mamlaka nyingine ambazo Mkapa anakumbukwa kwa kuunda ni Tanroads, Taasisi ya kudhibiti rushwa wakati huo ikitambulika kama PCB au Takuru ambazo baadae ziliboreshwa zaidi na warithi wake.

Nyingine ni Taasisi za udhibiti, Taasisi na mifuko ya kuinua Wananchi kama ya  Mkukuta, Mkurabita,Mifuko ya Hifadhi ya jamii na nyinginezo.

FEDHA

Mageuzi aliyoyafanya Mkapa katika utawala wake yaligusa pia Taasisi za Fedha, na kwa uchache taasisi ndogo ndogo za mikopo, benki, taasisi za kubadilisha fedha ni miongoni mwa matokeo ya hayo.

SEKTA BINAFSI

Mageuzi ya sera  uchumi  ambayo yalikwenda pamoja na kubana matumizi, hali iliyosababisha pia kipindi fulani mifuko ya wananchi kukauka hata kubatizwa jina la ‘ukapa’ yaliwezesha pia kunyanyua sekta binafsi.

Pia  kuvutia wawekezaji na ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambao ulikuwa na changamoto zake.

Mikakati ya Mkapa kuinua sekta binafsi ilikuwa dhahiri ambapo hata katika hotuba yake ya Sikukuu ya Wafanyakazi aliyoitoa Mei 1, 2001 alisisitiza na kwa maneno yake mwenyewe alisema;

“Kamwe msisahau kuwa Serikali, na sekta ya umma kwa ujumla, sasa si mwajiri mkubwa kama ilivyokuwa zamani. Wanachama wenu wengi sasa watakuwa kwenye sekta binafsi. 

“Na kwa kadri sekta binafsi inavyotwaa majukumu mengi zaidi ya kiuchumi na utoaji wa nafasi za ajira, ndivyo wajibu na kazi za vyama vya wafanyakazi zinavyoongezeka. 

“Jiandaeni vizuri kuubeba mzigo huo, na Serikali itawasaidieni kwa Dhati,”.

MISAADA /MSAMAHA DENI

Mkapa pia anakumbukwa kwa kurudisha misaada lakini kujenga uhusiano mzuri na nchi nyingine zikiwmao Taasisi zake Kama zile za fedha.

Wakati anaingia madarakani pamoja na kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa ameacha uhusiano mzuri na nchi za Nordic ambao walikuwa wafadhili lakini inaelezwa kwa wakati huo walikuwa wameacha kutoa misaada.

Mkapa mwenyewe kupitia kitabu chake anasema baada ya kuingia madarakani kazi kubwa ilikuwa ni kuwashawishi wahisani kuwa mambo yatabadilika. 

“Nchi ilikuwa na madeni makubwa sana. Deni letu lilikuwa dola bilioni saba, tulisamehewa bilioni tatu, hii ilikuwa hatua kubwa sana na ilimfurahisha Mwalimu (Julius Nyerere) ambaye  wakati huo alishaanza kuumwa.

Kupitia kitabu chake Mkapa alisema aliamini kama nchi walihitaji kujiangalia upya na kujifikiria kimkakati upya.

 “Matokeo yake ni kwamba mapato yaliongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 mwaka 1995 kufikia dola 1,796,862 miaka kumi baadae.

“Fedha za kigeni ziliongezeka kutoka uwezo wa kununua bidhaa za mwezi mmoja na nusu kufikia uwezo wa kununua bidhaa za miezi 12 mitano na theluthi moja. 

“Riba za benki ilishuka kutoka asilimia 36% kufikia asilimia 15% mwaka 2005.

Mkapa alifichua jinsi ambavyo Mwalimu alikuwa hapendi IMF na Benki ya Dunia lakini  anasema wakati huo walikuwa wameanza kuonesha namna ya kusaidia katika kuinua Uchumi,  licha ya wakati huo kutokuwa na imani na Serikali.

katika mabadiliko aliyofanya Mkapa matokeo yake yakawa ni kuungwa mkono na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), na kujenga msingi madhubuti wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa miaka iliyofuata hata baada ya kutoka madarakani.

Kwa upande wa mahusiano ya Kimataifa pamoja na IMF na Benki ya Dunia kwa mujibu wa Mkapa mwenyewe alifanya vizuri na kwamba alikuwa na mahusiano ya karibu ya kikazi na viongozi wa taasisi hizo kiasi kwamba mwaka 2001 Horst Kohler na James Wolfensohn  ambao walipata kufanya mkutano na wakuu wa nchi za ukanda wa  Tanzania.

Pia waliendelea kufadhili miradi mkubwa kama barabara.

Ni wakati huo wa Mkapa pia inaelezwa mapinduzi makubwa ya miundombinu ilianza kufanyika, waziri wake wa ujenzi akiwa Magufuli.

Mikoa ya Kusini ambayo ilikuwa shida kufikika hatimaye ilishuhudia ujenzi wa daraja kubwa la Mkapa na katika maeneo mengine ya nchi barabara zilijengwa.

Katika eneo la uwekezaji Mkapa anatakumbukwa kwa kuwajengea imani wawekezaji katika maeneo mbalimbali kama madini licha ya kujitokeza udhaifu wa mikataba.

ELIMU 

Mkapa pia ameacha historia kwenye sekta ya elimu japo mara kadhaa baada ya kuondoka madarakani amesikika akilaumu sekta hiyo.

Miaka miwili iliyopita Mkapa alitahadharisha akisema kuna janga katika elimu nchini, akiinyooshea kidole Serikali  kwamba ilikuwa haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu nchini.

Aliipa ushauri wizara husika akisema ina wajibu wa kutoa vitabu vinavyoendana na mabadiliko ya mitalaa.

Chini ya utawala wake, Mkapa  alifanya  mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu.

alianzisha mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MEM) Mpango wa maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MES) na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA).

UBINAFSISHAJI

Pamoja na mafanikio, yapo baadhi ya mambo ambayo hayakwenda vizuri katika utawala wake.

Mkapa mwenyewe amekiri kupitia kitabu hicho akiorodhesha mambo hayo kama  ubinafsishaji, mauaji ya Zanzibar, pamoja na wizi wa EPA.

Sera yake ya ubinafsishaji ambayo ilikosolewa vikali wakati fulani yeye mwenyewe alipata kukiri  makosa katika moja ya kongamano  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hata katika kitabu chake.

Aliwahi kukiri kuwa pamoja na kwamba jambo hilo lilikuwa jema na mafanikio kupatikana lakini sera hiyo ilikuwa na mapungufu.

Alipata pia kukiri kwamba hata Mwalimu Nyerere hakupenda sera hiyo  na hasa uamuzi wa uuzaji wa benki ya NBC.

Mashirika mengine yaliyoguswa na baadae kurudishwa baada ya kelele nyingi ni pamoja na Tanesco ambayo iliuzwa kwa Net Group Solution pamoja na Shirika la ndege Tanzania (ATC).  

Ingawa alijitetea kwamba Mwalimu baada ya kueleweshwa alielewa na hakuwa na neno na Ubinafsishaji wa NBC. 

Pamoja na hayo alikuwa akiamini kuwa ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma ulikuwa wa lazima na kuwa hakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuyapiga mnada wa jumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles