KWA USAJILI HUU, TUTASIKIA MNANUNUA MECHI

0
612

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

DIRISHA la usajili limefunguliwa rasmi Juni 15 mwaka huu kwa kuziruhusu klabu kusajili, kuuza wachezaji na kuwapeleka kwa mkopo wachezaji ambao wanatakiwa kuongeza uwajibikaji katika timu ili kuakisi ubora unaotakiwa

Tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara Mei 20 mwaka huu kumekuwa na harakati za usajili kwa klabu za ligi mbalimbali ili kuhakikisha zina jiimarisha katika msimu ujao.

Moja ya sababu ya kufanya usajili ni kuboresha kikosi katika maeneo korofi ambayo kwa maoni ya benchi ya ufundi akiwamo kocha mkuu, yanatakiwa kufanyiwa maboresho ili kuleta uimara wa kikosi utaosababisha kuwapo kwa ushindani.

Katika kutekeleza wa hilo, zipo klabu zinazotumia fedha nyingi kulingana na aina ya wachezaji wanaowataka kuwatumia katika vikosi vyao wakiamini wataleta ushindani wa hali ya juu.

Baadhi ya klabu kama  za Singida United, Azam FC, Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, na Mbeya City zimeoneakana kusajili kwa ushindani kuimarisha vikosi vyao.

Lakini moja ya mambo ya ajabu na aibu katika soka letu nchini ni kitendo cha klabu kununua matokeo kwa klabu nyingine, licha ya kuwapo wachezaji waliosajiliwa kwa  gharama kubwa.

Mwaka jana yalikuwapo malalamiko lukuki ya upangaji matokeo yakiwamo yale yalihusisha timu za daraja la kwanza za Polisi ya Tabora na Geita Gold Sport na kusababisha kupewa adhabu ya kushushwa daraja.

Katika Ligi kuu zipo taarifa za wachezai au viongozi klabu husika kupewa fedha na viongozi wa klabu pinzani ili kupooza makali ya ushindani ndani ya uwanja na kupata pointi tatu kiulaini bila ya kutoka jasho.

Kutokana na sababu hiyo, kuna wakati klabu zinalazimika kubadili wachezaji wa kikosi cha kwanza kutoka na kukosa uaminifu kwa kuhusishwa na kupokea rushwa.

Vitendo hivyo vinafanya klabu kulemaa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau ambapo mwisho wa yote lawama huenda kwa Shirikisho la Soka (TFF) ambalo ndio muhimiri mkuu wa soka nchini.

Nguvu hiyo ya fedha uwakumba pia waamuzi pamoja na baadhi ya viongozi wa TFF ambapo kwa nafasi zao uchangia kuvuruga kabisa mchezo wa soka na maana nzima ya kutumia fedha nyingi kwa kufanya usajili bora.

Ni  Bara la Afrika tu hasa Tanzania unaweza kukuta klabu inatumia zaidi ya milioni 500 kusajili wachezaji na  kutenga shilingi milioni 100 za kuhonga timu pinzani na shilingi milioni 50  za kufanya ushirikina ili kuloga wakiamini watafanya vizuri.

Kama hatutaweza kujifunza kwa wenzetu waliotupita katika mchezo huu na tukaendelea kufanya tuliyoyazoea, hakutakuwa na sababu za kufanya sajili za mbwembwe wakati tunazonjia mbadala za kupata pointi tatu.

Lazima mchezo wa soka uheshimiwe na kupewa adhi yake ya kujitawala wenyewe bila ya kuingiza mambo yetu ya ajabu ambayo hayapo katika utaratibu wa mchezo huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here