26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

KWA TRUMP NCHI ZA KIAFRIKA ZIJIPANGE

Na JUSTIN DAMIAN,

NOVEMBA 8, mwaka jana Wamarekani waliamua kufanya tukio lililoishangaza Marekani kama si dunia nzima. Waliamua kumchagua Rais wao mwenye msimamo mkali na kauli tata ambazo kwa siasa za Marekani zilikuwa hazijazoeleka.

Yawezekana ni wachache sana waliofikiria kuwa Donald Trump angeweza kuwa Rais wa 45 wa Marekani.

Nilipata bahati ya kushiriki kipindi cha lala salama cha kampeni za Uchaguzi Mkuu nchini Marekani uliokuwa na ushindani mkubwa. Pamoja na ushindani uliokuwepo kwa hakika Wamarekani wengi hawakutarajia kama bilionea huyo angeshinda. Wengi walionekana kukata tamaa kutokana na sera zake.

Yote kwa yote, Trump sasa ndiye Rais wa taifa hilo kubwa duniani. Kiongozi huyo tayari ameshaweka wazi kuwa kila ambacho nchi yake itakifanya, kikubwa itatanguliza masilahi mapana ya watu wake pasipo kupepesa macho.

Siku chache baada ya Trump kuingia madarakani, tumeona akianza kwa mwendo kasi na sera zake za kutaka kuijenga Marekani mpya na kuongeza ajira.

Kwa wanaofuatilia mwenendo wake, watakumbuka kuwa ameilazimisha Ujerumani kujenga kiwanda cha magari nchini Marekani badala ya Mexico vinginevyo atapandisha kodi kwa magari ya Ujerumani yatakayoingia Marekani. Hata hivyo, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, alipingana na wazo hilo.

Nchi za Kiafrika ambazo zimekuwa zikitegemea misaada mbalimbali kutoka Marekani, zinatarajiwa kuathirika kwa kiasi kikubwa kulingana na wachambuzi wa mambo wanavyoona. Kihistoria, nchi za Afrika hazijawahi kuwa kipaumbele kwenye sera za nje za Marekani japokuwa mambo yamekuwa yakibadilika kulingana na mtawala wa nchi hiyo.

Mwaka 2000 aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bill Clinton, alisaini mkataba wa AGOA ambao ulitoa unafuu kwa nchi za Kiafrika zinazofanya biashara na Marekani kwa kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazoingia Marekani. Kwa kuonyesha kuwa Afrika haikuwa kipaumbele cha Marekani, kipindi cha utawala wa Clinton mauaji ya kimbari yalitokea ambapo Wanyarwanda takribani 800,000 waliuawa.

Pamoja na kwamba utawala wa Clinton na Umoja wa Mataifa ulilifahamu hilo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Kama nilivyosema awali, kipaumbele juu ya Afrika inategemea nani yupo Ikulu. Utawala wa George W Bush, pengine ndio unaweza kusema ulikuwa na manufaa makubwa kwa Afrika. Bush alisaidia kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa nchi kama DR Congo, Angola, Sudan, Siera Leone pamoja na Liberia.

Katika awamu yake ya pili alizindua mipango mbalimbali ya kutoa misaada ya kuziinua nchi za Kiafrika kiuchumi na kutoa misaada ya kibinadamu. Tanzania ilikuwa moja ya nchi iliyofaidika na msaada wa Akaunti ya Milenia (MCC) chini ya utawala wa Bush ambao ulikuwa ndio msaada mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na Marekani kwa nchi moja ya Afrika.

Alipoingia Rais Obama, aliendelea kutoa ufadhili kwa nchi za Kiafrika. Aliendelea kufadhili miradi ya Ukimwi na kuongeza namba ya watu wanaoishi kwa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi kufikia milioni 6.7 kutoka milioni 1.7. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na watu 688,600 waliokuwa wakiishi kwa dawa za kurefusha maisha. Tayari Tume ya Taifa ya Kupambana na Ukimwi (TACAID), imekiri tishio hilo na kuahidi kujipanga kukabiliana na hali itakayotokea.

Obama pia alianzisha mradi wa Power Africa unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme ambao aliuzindua hapa Tanzania wakati alipofanya ziara yake ya kiserikali mwaka 2013.

Rias mpya Trump, ni tofauti na watangulizi wake. Japokuwa ni jambo lililo wazi kuwa sera za nje za nchi yoyote ni kwa manufaa ya nchi husika, Trump anakwenda mbali zaidi. Sera yake inakwenda na kaulimbiu ‘Marekani Kwanza’ na anaonekana kumaanisha anachokisema.

Katika kipindi cha kampeni, Trump aliwahi kuwatuhumu viongozi wa nchi za Kiafrika kuwa ni wezi akitolea mfano wa Kenya na Nigeria. Kiongozi huyu mwenye kauli tata alisema viongozi wa Kiafrika huiba fedha nchini mwao na kuzificha kwenye akaunti za nje ya nchi zao. Alikwenda mbali zaidi na kusema Afrika inakosa uongozi mzuri na ustaarabu na kusisitiza kuwa inastahili kutawaliwa upya.

Mwenendo unaonyesha wazi kuwa Trump ana mtizamo hasi sana juu ya Afrika na Waafrika. Kwa mtizamo wake anaona matatizo ya bara hili yanatengenezwa na watu wake na kwa hiyo haoni kama kuna haja sana ya kujiingiza wakati wananchi wake wanakabiliwa na matatizo kama ukosefu wa ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles