25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kwa nini wasomi wako pembeni!  (1)

wahitimuMOJA ya kauli zinazojirudia rudia ukisikia matamshi ya wanasiasa na kilio cha wananchi kwa ujumla ni kuhusu wasomi kutoa au kutotoa mchango wao kikamilifu katika nyanja mbalimbali za maendeleo na maisha ya Taifa.

Ningetaka kuzungumza, japo kwa ufupi kwa nini wasomi, sio katika Tanzania tu bali Afrika yote, hawawezi kuwa watu wa msaada sana!  Nianze kwa kusema kuwa mtu anapoitwa msomi maana yake ni kuwa anatumia muda mrefu kujiongezea maarifa kwa njia ya kusoma soma au kufanya utafiti wa ugunduzi na kuusambaza ugunduzi huo kwa wengine.

Na kuwa hata kama hafanya utafiti msomi ni mtu anayetumia muda mwingi kutafakari juu ya eneo lake la weledi, maeneo mengine na jamii kwa ujumla ili kuona kama anaweza kutoa majibu ya yale yanayokinza maendeleo.

Ili kuwe na wasomi lazima kuwa na taasisi za vyuo vya kati na vyuo vikuu, ingawa msomi anaweza kuwa mtu yeyote yule ambaye anafanya kama ninavyosema na anatoa majibu yake kwa jamii kwa tafakuri na utafutaji majibu (reasoning) ambayo ni ya kiyakinifu na sio kwa uzushi, tuhuma na kuiga kinachosemwa na wengine. Msomi ni muasili –original, katika kufikiri kwake.

Tatizo la watu ambao ni waasili (original) ni kuwa hawafuati mkumbo. Wao huangalia kweli na isiyo kweli, inayowezekana na isiyowezekana na kusema kilicho sahihi. Siasa ni sanaa ya kusema inawezekana pale isipowezekana na kuzungumza ambacho wanataka kusikia na sio kinachowezekana. Hili pekee linaweza kuwafanya wasomi wasitangamane na wanasiasa.

Wanasiasa  wanatafuta njia ya kufikia pale wanapotaka wao, yaani ushindi na kukukubalika, kwa hiyo huwa hawajali matokeo ya kile wanachokifanya, wao wanajali ushindi, msomi atataka kutafakari juu ya madhara yake na msomi atakayekubalika ni yule ambaye anajua ukweli, anajua madhara, lakini ananyamaza, au anasema kuwa hakuna haja na awe ameshika kipakio cha rangi nyeupe kinachomwosha mwanasiasa. Na wasomi wengi sio watu wa kushika kipakio cha rangi nyeupe.

Hawataki, hawawezi, hawataki kuwa sehemu ya mfumo wa mawazo ya kikampeni, propaganda. Kwa sababu hiyo wasomi wanajitenga na siasa. Na hata wale ambao wamejitenga na siasa na kusema kwa kadri ukweli ulivyo hutengwa, hawatakiwa, wanaweza kukosa kazi na wale ambao wameamua kuwa washauri wa wanasiasa na vyama, wakaamua kuwapaka rangi nyeupe wanasiasa na vyama vyao, mambo yao yanaweza kuwa poa.

Unapokuwa na mfumo wa siasa na wa kivyama ambao haujali elimu ila ukada na ushabiki, sidhani kama msomi na usomi vinaweza kuwa na fursa na dhima yoyote muhimu kwa wanasiasa na jamii. Wenzetu, kwa mfano, Iran, kama huna digrii ya pili huwezi kugombea ubunge. Kwa hiyo wanaoingia huko ni wasomi, ambao wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua masuala, miswada na hoja.

Ukiangalia Bunge letu, moja ya udhaifu mkubwa ni kuwa kila mmoja anaweza kuwa mbunge na uwezo wake wa kuchambua hoja, kutafakari juu ya masuala – reasoning capacity and ability, haiangaliwi. Elimu haiangaliwi ili mradi uwe na uwezo wa kusoma na kuandika na kutia saini.

Sijui kama hili limekwisha, lakini kuna wakati nikiwa Mwandishi wa Bunge… hansard records zilikuwa zikiwekwa wazi…  hakuna aliyekuwa akizichukua isipokuwa wabunge wachache… tena ziko kwa Kiswahili.

Bunge likiisha utakuta kwenye vyumba vya hoteli makabrasha na miswada imezagaa…! Kwa nini ujihangaishe na kusoma! Na kama mbunge anaweza kusema zidumu fikra za Mwenyekiti na kama mbunge anaweza kuzungumza dakika zote kumi na tano kuwatukana wapinzani wake na Spika asiseme kuwa hiyo ni non-issue, azungumze hoja ya zenye msingi na mashiko –substantive argumentation, basi mbunge huyo atajua kuwa kumbe ukitukana unakubalika kwa Spika na kwa watu wa kwenu- chama chenu.

Usomi unakuwa wa kazi gani sasa? Na ndio maana wale wabunge ambao wanatumia muda wao mwingi kusoma kila kitu, huwa ndio wazungumzaji wakuu na huonekana wakorofi na wanafukuzwa bungeni. Kinachowachongea ni kusomasoma, kusoma kila kitu, hawasubiri msimamo wa chama na kuanza kuimba kama kasuku kuurudia msimamo wa chama!

Usomi sio kupata vyeti au kuhitimu katika fani! Usomi ni jukumu la kudumu na la kuwa na fursa ya kudumu ya kufanya utafiti ili kuweza kuzalisha maarifa mpya, kama hakuna utafiti hakuna msomi; atakuwa amehitimu digrii yake ya kwanza, ya Uzamili au Uzamivu, akapata cheti basi.

Kama kweli Taifa linalilia wasomi kuwa watu wenye mawazo mapya na kuweza kutoa mchango, lazima kuwawezesha kufanya utafiti.

Kama hawana fedha na taasisi zinazowawezesha kufanya utafiti maana yake unakuwa kama umenunua kisu dukani halafu hukinoi. Kinakuwa butu. Msomi asiyefanya utafiti ni kisu butu.

Tanzania ni nchi ngumu sana kwa msomi, kwa sababu hana mahali pa uhakika pa kupata fedha kwa ajili ya kufanyia utafiti, kufanyia machapisho na kusambaza matokeo ya utafiti.

Kuna watu wana mawazo lakini yameshindwa kufikia kuwa utafiti kwa vile hakuna pa kupata fedha, kuna watu wanatafiti tayari ili ziwe vitabu hawana fedha za kumalizia au kuchapisha kuwa vitabu, kuna watu wamefanya tafiti lakini hawana fedha za kupanua wigo wa majaribio ili kuthibitisha na kukamilisha taratibu fulani ili tafiti hizo zikakubalika… wamekwama, wamekosa fedha.

Bajeti yetu nasikia ilikuwa na 0.5 ya fedha kwa ajili ya utafiti na huo sio kwa ajili ya wasomi wa vyuo, bali ndani ya Serikali.

Wasomi hawana mradi huo! Ungedhani mamlaka zilizopewa jukumu hilo lingekuwa na fedha nyingi sana kwa kila msomi kwenda kuomba, au kuitisha tafiti kuweka mawazo yao na wale wenye mawazo bora wangepewa msaada. Lakini hakuna.

Msomi anawezaje kuwa wa msaada! Ndio maana wengi wanapomaliza shahada huwa ni mwisho wa kazi na hasa kama atatoka nje ya mfumo wa chuo kikuu na wale walioko vyuo vikuu kama hakuna nafasi ya kushirikiana na watu na taasisi kutoka nje, unaweza ukachina! Ni lazima uwe mbunifu wa kuandika miswada ya kuomba ufadhili na mashirika ya ndani hayatoi  fedha kwa ajili ya usomi, wengi wanatoa ufadhili huko kwenye bongofleva  na mambo kama hayo! Nimeona rafiki zangu wengi na mimi mwenyewe nikiwamo, tukiwa na mawazo, miswada na mikakati lakini huna pa kuipeleka wala pa kupokelewa ikaweza kutelekezwa.

Nitaendelea na hili wiki ijayo!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles