Na Mwandishi Wetu,
KATIKA mkutano wa Umoja wa Kampuni za Simu uliomalizika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, ilibainishwa kwamba maisha ya wanawake wengi nchini hususani wale wanaoishi maeneo ya vijijini yanaweza kubadilishwa kwa kiwango kikubwa na kuwa mazuri kama watakuwa wameunganishwa vizuri kidijitali.
Mtazamo huo uliungwa mkono na utafiti uliofanywa na Kampuni ya Simu ya Tigo na Kampuni ya Kidogo Kidogo inayojishughulisha na ujasiriamali jamii yenye makao yake nchini Marekani. Kampuni hii ilianzishwa kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la pengo la kidijitali katika simu kwa hatua za taratibu kwa kusaidia kutoa simu za bure kwa wanawake walio na kipato cha chini.
Katika jaribio lililofanywa simu za mkononi ziligawiwa kwa washiriki kupitia warsha iliyotoa mafunzo ya teknolojia ya simu. Washiriki walipokea maelezo kuhusu namna ya kutumia simu mpya aina ya Nokia 105 kupitia huduma zilizotolewa na Tigo.
Utafiti huo uliofanywa kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la CARE International, Shirika la Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa) ambalo linaongoza kwa utafitri katika Nyanja hiyo Tanzania na watafiti kutoka Chuo cha William and Mary na Chuo Kikuu cha Brigham Young nchini Marekani ambao ulijumuisha zaidi ya wanawake 400 kutoka wilaya za Rufiji, na Kilwa katika ukanda wa pwani ya Tanzania.
Aidha, utafiti huo ulikuwa na kipindi cha miezi sita ya kufanya tathmini ukiwa na mtazamo katika kumiliki na kutumia simu ya mkononi na kuangalia matokeo yake katika ustawi na uwezeshwaji kwa mtu binafsi.
Makundi hayo matatu ya utafiti yalijipanga na jumla ya washiriki 150 walipokea simu pamoja na kadi za simu za Tigo zikiwa na salio la kutosha wakati wa kuanza kwa utafiti Desemba 2015 wakati washiriki 100 walipewa fedha taslimu kwa uwiano sawa na hawakupewa simu.
Kundi jingine la washiriki 150 wakiwa ni kundi lililokuwa chini ya udhibiti walipokea simu baada ya kumalizika kwa utaifi Julai 2016.
Warsha za ufuatiliaji wa utafiti ziliendeshwa na mdau wa ndani ambao ni Chama cha waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Hakuna aliyekuwa anamiliki simu wakati utafiti huo ulipokuwa unaanza na wengi wao walikuwa ni wakulima wadogo, wakiwa na umri kati ya miaka 18 hadi 79. Miongoni mwao asilimia 35 ya washiriki walikuwa hawana weledi wa aina yoyote kwa kuwa walikuwa hawajui kusoma wala kuandika, asilimia 24 angalau walikuwa na weledi kidogo na asilimia 38 walikuwa ni weledi.
Asilimia 91 ya washiriki awali walisema kuwa gharama za kifedha kwa ajili ya kununua simu zilikuwa kubwa na hivyo kuwa kikwazo kwao kumudu kununua simu. Hivyo, kwa kupata simu za bure mabadiliko chanya yameonekana.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya utafiti, wamiliki wa simu za mkononi walipata matokeo kadhaa chanya miongoni mwa wanawake ambayo yalijumuisha kuweza kuifikia mitandao ya kijamii, taarifa za kifedha na kuongeza kipato cha wiki na mwezi katika biashara zao ndogondogo.
Hali halisi
Hali inayofahamika baya na ni kwamba mwanamke wa kawaida barani Afrika yupo nyuma kidijitali katika enzi hizi ambapo wanawake katika mabara mengine wapo katika mkondo sahihi wa sekta hiyo na wanakimbia, hata hivyo ubunifu wa kubadilisha maisha ulioletwa na simu za mkononi kama vile zana za huduma ya afya, kuhamisha fedha.
Kutokana na hali hiyo ni muhimu kufikiria jinsi kujumuishwa kidijitali, huduma za fedha kwa simu za mkononi kama vile huduma ya Tigopesa itakavyoibadili Afrika kwa ujumla, hususani kwa Tanzania. Inatakiwa kukumbuka kwamba kupata taarifa imetajwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Diego Gutierrez alipongeza matokeo chanya ya teknolojia ya simu ambao umeletwa Afrika na kubainisha maeneo manne ambayo yanatakiwa kushughulikiwa ili kuongeza ujumuishwaji kidijitali.
“Kuna vikwazo vikubwa katika kuridhia, hususani kwa makundi ya jamii ambayo ni maskini kama vile maeneo ya vijijini, wanawake walio na kipato cha chini na vijana,” alisema.
Kama mdau katika sekta hiyo kwa haraka alidokeza simulizi kadhaa za mafanikio ikiwa ni pamoja na kukua kwa huduma za simu, ikiwmao fedha, afya (mHealth) nakilimo (mAgri).
Maeneo ya mtandao yanaweza kuboreshwa kwa kupanua mitandao ya simu yenye uwanda mpana kuyafikia makundi ya jamii ambayo ni maskini. Hadi hapo ndipo kampuni imeweza kuondokana na adha hiyo kupitia uendeshaji wa pamoja na mitandao mingine na moja kwa moja kuinunua Zantel ili kuwafikia watu wa Zanzibar na Mkoa wa Pwani.