Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Serikali imeshauriwa kuanzisha mafunzo ya ualimu wa viziwi wasioona ili kukabili upungufu wa walimu wa kada hiyo.
Ushauri huo umetolewa Novemba 25,2022 na Mkuu wa Kitengo cha Wenye Ulemavu wa Uziwi Wasioona katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Mwalimu Maura Adriano, wakati akizungumza na Mtanzania Digital.
Amesema wamekuwa wakiletewa walimu lakini wakishafika na kuona mazingira ya ufundishaji yalivyo wengine hushindwa kuendelea.
“Kwa sasa tunawachukua hapa hapa na kuwapa mafunzo, lazima awe mwalimu anayefundisha wasioona au viziwi, akisema hawezi tunamuambia arudi katika darasa lake la awali.
“Wanaotoka vyuoni wana changamoto lakini wanaotokea kazini kwa sababu hali wameshaiona inakuwa rahisi, hata kama amesoma elimu maalumu kikubwa awe na moyo,” amesema Mwalimu Maura.
Mwalimu Maura amesema walimu wawili ambao walipata mafunzo ya kufundisha viziwi wasioona ndiyo waliowapa ujuzi huo lakini kwasasa wamestaafu.
Mwalimu mwingine katika kitengo hicho, Edith Dosha, amesema alihamia mwaka 2003 akitokea Shule ya Msingi Mchikichini alikokuwa akifundisha wanafunzi wasio na ulemavu.
“Nilikwenda kusoma elimu maalumu Chuo cha Patandi kisha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, na baadaye nilipata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani,” amesema Mwalimu Dosha.
Takwimu kutoka Kitengo kinachoshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu, zinaonyesha katika kada ya elimu maalumu Serikali imeajiri walimu 648 kati ya ajira za ualimu 24,646 zilizotangazwa kati ya mwaka 2020 hadi 2022.
Kulingana na takwimu hizo mwaka 2020 waliajiriwa walimu 242 kati ya 8,000 wakati mwaka 2021 waliajiriwa 145 kati ya 6,946 na mwaka 2022 waliajiriwa 261 kati ya 9,700.