29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Kuwa makini, tatizo hili limevunja mahusiano mengi

ZAIDI ya asilimia 60 ya watu waliopo katika uhusiano hawana furaha na maisha yao. Kwa mujibu wa utafiti wangu binafsi ni chini ya asilimia 40, miongoni mwa watu walio katika uhusiano wa kimapenzi ndiyo wenye furaha timilifu. Unajua tatizo ni nini?

Mahusiano mengi yana ombwe (vacuum). Wahusika wanashindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu wawapo katika mahusiano ndiyo maana wengi hawana furaha.

Tuanze na wewe unayesoma makala hii leo, unamfanya vipi mwandani wako kuwa na furaha na amani? Ni mara ngapi umekuwa chachu au sababu ya tabasamu ama raha ya mwenzako?

Rafiki yangu Nizihrath Ntani siku moja alipata kuniuliza, kwanini watu wengi walio katika uhusiano ni wepesi kuanzisha mahusiano mengine kuliko ambaye hayuko katika uhusiano kuanzisha mahusiano?

Jibu lilikuwa jepesi sana. Binadamu ni kiumbe mwenye kuhitaji raha, furaha na amani. Japo hawezi kupata vitu hivi kila siku ya maisha yake kutokana na mfumo wa maisha ila kimsingi anataka uzani wa furaha katika maisha uwe mzito zaidi kuliko uzani wa huzuni na karaha.

Sasa bahati mbaya ya maisha ya ndoa,  wengi yamejaa ubinafsi, mazoea na kujisahau. Athari ya mambo haya ni kufubaza upendo uliopo miongoni mwa wapendanao na hatimaye kuanza kukerana na kusumbuana.

Hali hii inapozidi, unadhani ni kwanini mahusiano ndani ya yatashindwa kuanzishwa hapa?

Moja kati ya njia za uhakika za kudhibiti usaliti, ni wahusika kujiuliza ni kwa kiwango gani kila mmoja anakuwa furaha na raha ya mwenzake?

Kama mwenzako hajisikii raha wala furaha kwa uwepo wako, unadhani hali hiyo mwisho wake ni nini?

Watu wengi katika uhusiano wanalala pamoja kwa sababu ni wajibu kufanya hivyo.

Hakuna bashasha, uchangamfu wala ubunifu miongioni mwao. Kuna wakati japo wapo katika ndoa ila wanajihisi kama wako singo.

Kumbuka kama humfanyi mwenzako akajisikia vizuri ama raha kwa ajili yako, basi hata yeye atakuwa na mwamko mdogo wa kukufanya uwe na furaha katika maisha yako.

Nimewahi kuandika katika makala zangu zilizopita kwamba, njia nzuri ya kupata furaha na raha kutoka kwa mwenzako ni wewe kuanza kumpa furaha na raha.

Kila mmoja aliye katika uhusiano inabidi ajue kwa makini kwamba, mwenzake aliamua kuwa na yeye kwa sababu aliamini kwa kuwa wapo pamoja atakuwa na furaha, amani na kupata raha ambazo amekuwa akiziota ama kuzitamani kwa muda mrefu.

Hivyo unaposhindwa kumfanya mwenzako kupata raha na furaha unakuwa unaenda kinyume na matarajio na matamanio aliyo kuwa nayo kwako.

Sasa jiulize, kama mwenzako anapata kitu ambacho sicho alidhani atakikuta kwako, ataendelea kuwa na wewe mpaka lini?

Kusalitiwa ni kitu kibaya na hakuna anayependa ila  wengi wanasalitiwa kwa sababu wameamua kuishi katika mahusiano kimazoea bila kujali wala kuzingatia matakwa ya hisia za wenzao.

Unaposhindwa kutimiza majukumu yako ipasavyo kwa mwenzako, kama vile kumjali, kumthamini na kumfanya kuwa na furaha ujue unaacha uwazi katika uhusiano wako.
Na kawaida asili huwa haivumilii uwazi (Nature doesn’t tolerate the vacuum) ni lazima kitu kifanyike ili uwazi huo uzibwe. Kama wewe hutoamka mapema na kujua kuna makosa unafanya na kuhangaika kuziba uwazi huo, basi yupo mjinga mmoja kutoka mbali huko atakuja kufanya kazi ambayo umeshindwa kuitekeleza.

Kwa maslahi ya furaha na amani ya uhusiano wako, hakikisha unaziba kila mwanya. Hakikisha mwenzako anakuwa mchangumfu kwa ajili yako na anapata angalau robo tatu ya anayotamani kupata kutoka katika mahusino yenu.

Ni vema kila mmoja akajua hakuna kazi katika kuanzisha uhusiano ila inahitaji akili iliyotulia na umakini katika kuishi katika misingi sahihi ndani ya uhusiano husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles