31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kutokujiamini kwa wanawake bado ni kikwazo kufikia usawa wa kijinsia

Na Faraja Masinde Mtanzania Digital

Ukosefu wa kujiamini na kutokujengewa uwezo imetajwa kuwa sababu zinazochochea wanawake wengi kubaki nyuma katika usawa wa kijinsia na ufanyaji wa maamuzi.

Hayo yameelezwa Dar es Salaam leo Septemba mosi, 2022 na Mtaalamu wa Vyombo vya Habari kutoka Shirika la Internews Tanzania, Alakok Mayombo katika warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu masuala ya Jinsia.

Amesema ukosefu wa maarifa na kujiamini miongoni mwa wanawake ndiyo imekuwa sababu ya kundi hilo kubaki nyuma.

“Suala la jinsia ni muhimu sana katika jamii kwa sababu kunapokuwa na mahusiano ya jinsia katika jamii yanaifanya isonge mbele, kila mtu anapata nafasi sawasawa.

“Leo tumeshirikisha waandishi wa habari kwani unakutaka kwamba ndiyo kuna wanaume na kuna wanawake, lakini unakuta kwamba wanaume ndiyo wengi katika ngazi za maamuzi.

“Tunaamini kwamba hii inaweza kuleta mabadiliko siku za usoni iwapo tu wanawake wataendelezwa kitaaluma ili wawe na uwezo kwani wakipata uwezo na mazingira yakawa ni rafiki kwa maana ya sera na mifumo wanaweza kufika kwenye ngazi ya 50/50,” amesema Alakok na kuongeza kuwa:

“Pia waandishi wa habari watumie nafasi zao katika kuhakikisha kuwa sauti za wanawake zinasikika kuanzia wakawaida hadi wale wanaotazamwa kama mfano kwani kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba sote tutakwenda pamoja na jamii itafikia kwenye mabadiliko,” amesema Alakok.

Amesema lengo la Internews ni kuhakikisha kuwa inawajengea uwezo waandishi wa habari ili jamii iweze kusonga mbele katika nyanja mbalimbali.

“Ni bayana kwamba katika jamii yetu siyo wanawake wote wanaweza kuzungumza kwenye vyombo vya habari kutokana wakati mwingine na mila na desturi, jambo la msingi ni kwa wanahabari kuangalia mbinu sahihi ili kuweza kupata sauti zao,” amesema Alakok.

Mhadhiri Msaidizi wa Shule ya Uhandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(SJMC), Zuhura Selemani.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mhadhiri Msaidizi wa Shule ya Uhandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(SJMC), Zuhura Selemani amesema kuwa ili kuimarisha usawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali kuna umuhimu wa kufanya maboresho ya kisera kwa kutunga sheria itakayokuwa inalazimisha usawa kwenye vyombo vya maamuzi.

Amefafanua zaidi kuwa jinsia ya kiume kuendelea kushika nafasi kwenye mamlaka za taasisi mbalimbali inatokana na udhaifu wa sheria zilizopo kushindwa kulazimisha asilimia 50/50 kwenye vyombo vya maamuzi.

Ametolea mfano amesema kuwa ni muhimu kama taifa kujifunza katika mataifa yaliyofanikiwakama Rwanda ambao walishinikiza kushinikiza usawa kuzingatiwa.

“Utafiti unaonyesha kuwa bado jinisia ya kiume wapo kwenye vyombo vingi vya maamuzi lakini likufanikiwa kutengeza usawa tunaoutaka ni muhimu kuangalia namna ya kuangalia sera zetu kutunga sheria itakayokuwa inalazimisha usawa uzingatiwe,” amesema Zuhura.

Amesema hata kwenye vyombo vingi vya habari nchini kwenye bodi zake wajumbe wengi ni jinsia ya kiume hivyo kutatua suala hilo kiuhalisia ni vyema sheria na elimu zikaendelea kutolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Transformative and Intergrative Build out for All(TIBA), Marcela Lungu.

Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Transformative and Intergrative Build out for All(TIBA), Marcela Lungu amesema usawa wa kijinsia ukizingatiwa kwenye nafasi mbalimbali itakuwa ni chachu kubwa katika kuchangia maendelea ya Taifa.

“Tatizo linaloonekana mtazamo na makuzi ndiyo imekuwa sababu kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika maeneo mengi ya kazi na ikichukuliwa katika historia jinsia ya kiume ilikuwa inapewa nafasi kubwa kwenye maamuzi,”amesema Marcela.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ya siku moja, Tuzo Mapunda kutoka Gazeti la Mwananchi ,alisema mafunzo waliyopata ni muhimu kwani yanawasaidia wanahabari kuchochea usawa wa kijinsia pale wanapotekeleza majukumu yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles