29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kutana na mwanamke aliyeutamani uhandisi tangu akiwa mdogo

WANAWAKE wengi wamekuwa waoga wa kujiunga na fani ya uhandisi kwa imani waliojijengea kwamba masomo yake ni magumu na hivyo hawawezi kuyamudu.

Hii ni dhana potofu iliyojengeka kwa wasichana wengi, hali inayochagia kuwa na wahandisi wachache wanawake.

Sasa basi, Serikali inakiri kuwapo kwa upungufu mkubwa wa wahandisi wanawake unaochangia kuongeza changamoto katika sekta ya uhandisi nchini.

Idadi ya wahandisi wanawake ni ndogo ukilinganisha na wanaume, hali inayosabbaisha changamoto kubwa katika kuongezea idadi yao ili kuendana na mahitaji ya sekta zinazotegemea wahandisi.

Licha ya Serikali kutambua mchango wa wahandisi nchini hasa wanawake, bado kunahitajika juhudi na mikakati madhubuti ili kuongeza idadi ya wahandisi.

Kwa kutambua umuhimu wa wanawake kwa maendeleo ya nchi hasa katika sekta za nishati, madini, barabara, maji na kilimo, Serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ikiwamo kuongeza vyuo vya uhandisi na kufikia tisa.

Licha ya idadi hiyo ya vyuo, ni vema kuongeza ushawishi kwa watoto wa kike kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati na kudahiliwa katika vyuo vinavyofundisha fani ya uhandisi.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, elimu hapa nchini imekuwa ni sehemu muhimu ya ajenda ya Serikali. Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwapo usawa katika upatikanaji wa elimu ya msingi.

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa ni katika suala zima la ubora wa elimu na umuhimu wa wanafunzi kupatiwa ujuzi utakaowezesha kufikia Tanzania ya viwanda hatimaye kukuza uchumi.

Ni dhahiri kuwa uchumi wa viwanda ambayo ndiyo kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano, hauwezi kufikiwa kama nchi haitazalisha wahandisi wa kutosha kufanya kazi katika viwanda ili kuchochea ufanisi na hatimaye maendeleo ya nchi.

Ajitosa kusomea uhandisi

Wakati wasichana wengi wakikimbia kujiunga na masomo ya sayansi, hali ilikuwa tofauti kwa Ghati Mwita, binti aliyezaliwa na kulelewa katika familia ya kipato cha kati huko wilayani Tarime, mkoani Mara.

Tangu akiwa mdogo, Ghati siku zote alitamani kuwa mhandisi.

Anasema: “Baba yangu alizoea kuniletea vitabu vingi ili vinipe hamasa ya kazi nitakayofanya baadae, nami nilihamasika zaidi na wazo la kuunda vitu.

Uhandisi ikiwa ni kazi isiyopendwa na wanawake wengi nchini, kwa upande wa Ghati hali ni tofauti.

Anasema anamshukuru mno baba yake kwa kumfungulia njia kuelekea kuwa mhandisi, kazi ambayo anaipenda kwa moyo wake wote.

“Baba alihakikisha anafanya chochote ili watoto wake tutimize ndoto zetu,” anasema.

Ghati anasema baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya uchakataji madini katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), aliomba na kufanikiwa kupata ufadhili kupitia mradi wa ANTHEI.

Alimaliza shahada yake ya uzamili kwa mafanikio mwaka 2014 na akawa mhitimu wa kwanza kuajiriwa na Equinor Tanzania kwa nafasi ya mafunzo kwa vitendo.

ANTHEI ni nini?

Ni mradi unaoendeshwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Norway (NTNU) huku ikifadhili wanafunzi 10 wazawa kila mwaka kwenda kusoma shahada ya uzamili ya uhandisi.

Wanafunzi hawa hutumia mwaka mmoja NTNU huko Trondheim na mwaka wa pili huumalizia Dar es Salaam wakifanya tafiti.

Ghati Mwita alikuwa miongoni mwa duru ya kwanza ya wanafunzi waliofadhiliwa na Equinor Tanzania katika kujenga uwezo kwa kuwalipia masomo kupitia mradi maalumu uitwao Angola Tanzania Higher Education Initiative (ANTHEI).

Ghati anasema huu ndio ulikuwa mwanzo wa safari ya yeye kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi. Japokuwa aliingia kama mfaidika wa ufadhili wa masomo.

Kutoka mwanamafunzo hadi mhandisi mzalishaji

Baada ya kufanya kazi ofisi ya Equinor Dar es Salaam, baadae alipelekwa Oslo kufanya kazi kwa miezi mitatu. Akiwa mbioni kumaliza muda wake wa mafunzo kwa vitendo, mwaka 2016, ofisi ya Equinor Tanzania ilimwajiri kusaidia shughuli za uwezeshaji wa uchimbaji zilizokuwa zikifanyika wakati huo.

“Nilipewa nafasi, niliifurahia kwa sababu ilinisaidia kuukomaza ujuzi wangu na taratibu nilianza kuona ndoto yangu ikitimia,” anaeleza Ghati.

Baada ya kukaa kwa takribani mwaka mmoja hapa nchini, alipata fursa nyingine na mara hii ilikuwa ni kwenda Harstad, Norway kufanya kazi ya mhandisi mzalishaji, kwenye mradi wa gesi wa Snøhvit na Aasta Hansteen.

“Utafiti wangu kwa ngazi ya shahada ya uzamili ulijikita katika maendeleo ya miradi kwa kutumia mbinu mchanganyiko,” anasema Ghati na kuongeza:

“Kwa kweli ujuzi ule ule ndio hasa ninaoutumia kwenye miradi ya Aasta Hansteen na Snøhvit.”

Kuleta ujuzi wa Hammerfest nchini

Ghati pamoja na wafanyakazi wengine wa Equinor, ni mfano wa jinsi kampuni ya Equinor inavyozidi kujitanua kimataifa huku ikiakisi na kuthamini mchango wa wazawa mbalimbali katika kuendesha dhana ya kampuni hii kuwa kimataifa.

Hii huipa sifa kubwa kampuni kukidhi vigezo vya kuwa ya kimataifa.

“Ni muhimu kuakisi mawazo na utendaji kazi kimataifa katika kuhakikisha ushindani bora na umakini kwenye maeneo yote ambayo kampuni ya Equinor inafanya shughuli zake,” anasema Ghati.

Mwezi huu Ghati alimaliza kazi maalumu aliyopewa huko Aasta Hansteen ambapo alitumia miezi 18. Hata hivyo, huu si mwisho wa safari; Ghati amepata nafasi nyingine ya kuwa mhandisi katika mradi wa Snøhvit, kazi atakayoianza rasmi Julai mwaka huu.

“Natarajia kuongeza ujuzi zaidi nitakapokuwa nikifanya kazi kwenye kiwanda cha kuchakata gesi cha Melkøya huko Hammerfest, na kinachofurahisha zaidi mpangilio wa mradi huu unashabihiana na ule unaopangwa kujengwa Tanzania kwa siku za usoni ili kuendeleza rasilimali za kitalu namba mbili kinachomilikiwa na Equinor Tanzania. “Baadae nitafurahia kurudi nyumbani Tanzania na kufanya kazi chini ya mradi huo mkubwa,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles