24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kutana na kabila linalotunza utamaduni wake wa kale

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

PICHA mpya za karibuni zinatoa taswira ya nadra ya maisha ya moja ya makabila yaliyojitenga kabisa katika sayari hii.

Watu wa kabila hilo liishilo porini la Dani, kutoka Bonde la Baliem nchini Indonesia katika nyanda za juu za Papau Magharibi walikutwa na mpiga picha wakicheza ngoma ya kimila ya kivita wakati wa tamasha lao la kitamaduni la wiki moja.

Wanaume wa kabila hilo lienzilo  utamaduni wao wa kale waliendesha ibada na matambiko, ambapo wanaume walionekana wamevalia kifuniko cha mfano wa ala kijulikanacho kama koteka.

Kifaa hicho hufunika sehemu zao za siri huku wanawake wakionekana wakipika nguruwe mwitu kwenye uwanja wa wazi.

Koteka hutengenezwa kwa matunda yaliyokauka na hushikiliwa na kamba ziliozozunguka kifuani na nyingine kuzunguka korodani.

Watu mara nyingi hudhani koteka ni ishara ya hadhi lakini ukweli ni kwa ajili ya kufunika sehemu za siri za mvaaji, kitu ambacho ni cha kawaida kwa wanaume waishio katika makundi fulani ya kikabila katika eneo zima la New Guinea.

Mapema miaka ya 1970, Serikali ya Indonesia ilizindua kile kilichoitwa ‘Operasi Koteka’ au Operesheni ya Kifuko cha Uume’ katika jaribio la kujaribu kuwaingiza watu hao katika utamaduni wa kisasa na kuwahamasisha wavae kaptura badala ya koteka lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Mwanazoolojia wa Marekani na mhisani Richard Archbold ndiye aliyeliibua kabila hilo la Dani kwa dunia ya Magharibi kwa bahati tu mwaka 1938.

Watu hao wa Dani pia wanafahamika kwa kitendo cha kuogofya kwa wanawake wa kabila kukata vidole vyao vya mwisho kuadhimisha kifo cha ndugu zao.

Picha hizo zilichukuliwa na mpiga picha wa Indonesia, Hariandi Hafid (30) wakati wa tukio hilo la wiki moja katika Bonde la Baliem kuonesha utamaduni wao na mila za ajabu, ambalo lilikuja fahamika kwa dunia katika karne ya 20.

Hariandi kutoka Makassar nchini Indonesia, anasema: “Tamasha hili linahusu kufanya ibada za kuheshimu mababu zao.

“Ngoma zimechochewa na vita zilizofanyika huko nyuma kuwakumbuka mashujaa wao na bado zinaendelea kutokea miongoni mwa makabila ya Dani.

“Kinachovutia kuwatazama zaidi ni namna wanavyovalia, kuna wengi wao bado hutumia koteka katika maisha yao ya kila siku.”

Ijapokuwa kitendo cha kukata vidole vimelaaniwa na kuharamishwa na Serikali ya Indonesia, Hariandi aliona ushahidi wa uwapo bado miongoni mwa wanawake wazee wa kabila hilo.

Tamasha la kila mwaka huhusisha uchezaji wa ngoma na muziki wa Papua, urushaji wa mkuki, upikaji ardhini na kusherehekea karamu ya kula nyama ya nguruwe.

Kwa kawaida wakazi hao wa Bonde la Baliem ni mashujaa wasio na hofu yoyote.

Hariandi alisema: “Baadhi ya mila na desturi za ajabu ajabu zinazidi kutoweka ikiwamo ya ukataji vidole, mwelekeo ambao unahusishwa na ukuaji wa dini za kigeni eneo hilo.

“Lakini koteka bado imeenea mno miongoni mwa wanaume. Inashangaza namna wanavyoweza kutunza urithi wao huo wa kale.”

Watu hao wa kabila hilo la Dani hujiita wenyewe kama ‘Ndani’ na kuna lugha zisizopungua nne zinazozungumzwa na jamii kutegemeana na mahali wanapoishi katika bonde hilo lao kubwa.

Kinachoshangaza zaidi kuhusu lugha ya Dani ni kwmba rangi zote huelezwa kwa maneno mawili tu.

‘Mili’ humaanisha rangi nyeusi, zenye kivuli kilichotulia kama vile bluu, kijani na nyeusi huku ‘mola’ ikihusisha rangi angavu kama vile nyeupe, njano, nyekundu na kadhalika.

Aidha, kabila hilo lina kwaida ya kuhifadhi miili ya mababu zao kwa kuikausha kwa namna ambayo huweza kukaa hivyo kwa mamia ya miaka.

Ukaushaji wa mabaki hayo ya mwili kwa sasa haufanyiki tena, lakini kabila la Dani bado linahifadhi mabaki ya kale lililo nayo kama alama ya heshima kwa mababu zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles